POLISI mkoani Rukwa inamshikilia Bakari Kessy ambaye ni mmiliki wa gari aina ya Fuso lililopinduka na kusababisha vifo vya watu 15 na wengine tisa kujeruhiwa.
Mmiliki huyo wa gari hilo lenye namba za usajili T 425 BFF, ni mtoto wa kiume wa mwanasiasa machachari, Ally Kessy (CCM) ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Lori hilo lilikuwa limebeba magunia ya nafaka yakiwemo mahindi, lilipinduka na kuua watu 15, wakiwamo wanawake 10 na wanaume watano huku mwenye umri mdogo akiwa mtoto mwenye umri wa wiki mbili na mwenye umri mkubwa akiwa na miaka 84.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema wanamshikilia mmiliki wa gari hilo kwa kuwa dereva wake amekimbia, hivyo ni jukumu lake kueleza alipo, na akishindwa atafikishwa mahakamani kwa kosa la uzembe wa kutotunza kumbukumbu za dereva wake.
Inasemekana devera wa gari hilo anayetafutwa na polisi baada ya kubaini kuwa gari limemshinda, aliruka kupitia dirishani na kulicha likiwa na abiria likienda kwa mwendo kasi na kugonga mwamba kisha kupinduka.
“Kweli tunamshikilia mmiliki wa gari lililosababisha ajali Bakari Kessy ili atuoneshe alipo dereva kwa kuwa yeye ndiye anayetunza kumbukumbu zake akishindwa basi tutamfikiza mahakamani,” alieleza Kamanda Kyando.
Aidha, alieleza kuwa maiti 14 kati ya 15 zimetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya maandalizi ya maziko yao isipokuwa mwili wa marehemu Abuu Amani (37) mkazi wa mkoani Kigoma haujachukuliwa na ndugu zake.
Miili iliyotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao ni Domona Tenganamba (41), Emmanuel Rashid (84), Restuta Sunga (35), Salula Revana (64), Felisia Tenganamba (1), Prisca Madeni (45), mwalimu wa shule Richard Chikwangara (24), Yusta Somamabuto (36), Grace Ramadhan (24), Odetha Madirisha (46), Megi Nalunguli (52), Nyandindi Batrahamu (35) na mtoto mwenye umri wa wiki mbili ambaye alikuwa hajapewa jina.
Kwa mujibu wa Kamanda Kyando, ajali hiyo ilitokea Oktoba 3, saa tisa alasiri na gari hilo lilikuwa likitokea Sumbawanga Mjini kwenda Kijiji cha Wapembe wilayani humo. Alisema dereva huyo ambaye jina lake halikufahamika amekimbia kusikojulikana muda mfupi baada ya ajali hiyo, huku chanzo kikielezwa kuwa ni mwendokasi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amepiga marufuku magari ya mizigo kubeba abiria huku akimwagiza Kamanda wa Polisi kufuatilia kwa karibu. Alishauri kuwa kama tatizo ni uhaba wa magari ya abiria, basi magari maarufu kama “chai maharage” yaanze kutoa huduma za kusafirisha abiria vijijini
No comments:
Post a Comment