Wednesday, October 25, 2017

NEMC WAPEWA SIKU MOJA KUPELEKA MAELEZO KWA WAZIRI LUGOLA KWANINI HAWAJAVUNJA NYUMBA YA MCHUNGAJI RWAKATARE

NAIBU Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kufikisha mezani kwake maelezo ni kwa nini nyumba ‘kasri’ ya mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Getrude Rwakatare (CCM) haijabomolewa.
Related image
Lugola ametoa muda kwa Nemc hadi kesho Alhamisi Oktoba 26,2017 saa 10:00 jioni awe amepata taarifa ya maandishi ili aweze kutoa uamuzi iwapo ibomolewe au la. Naibu waziri ametoa agizo hilo leo Jumatano Oktoba 25,2017 wakati Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipokutana na watendaji wa NEMC.

Lugola amefikia uamuzi huo baada ya Nemc katika taarifa yake kueleza serikali imeshindwa kuivunja nyumba hiyo kutokana na zuio lililopelekwa mahakamani na Mchungaji Rwakatare tangu mwaka 2012. Nemc imesema kesi ikiisha na uamuzi kutolewa hakutakuwa na shaka wala kigugumizi katika kuivunja nyumba hiyo.

Kwa kauli hiyo, Naibu Waziri Lugola amesema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba, hatima ya jengo hilo lazima ijulikane mapema ili kuondoa sintofahamu iliyopo.

“Rais Magufuli ameniteua kufanya kazi hii na anajua kwa nini alinichagua mimi. Naamini anajua uwezo wangu na utendaji kazi wangu, siko tayari mtu wa nafasi yoyote kuniangusha na kunifanya nishindwe kutimiza malengo yangu. Sitaki migongano ya aina yoyote inayoweza kuniangusha, hakuna jiwe litakaloachwa kusalia juu ya jiwe,” amesema.

Awali, wajumbe wa kamati walihoji uhalali wa nyumba hiyo kubaki bila kuguswa licha ya kujengwa eneo lisiloruhusiwa kisheria. Nyumba hiyo ipo Mtaa wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambayo iliamriwa kubomolewa lakini hilo halikufanyika kutokana na Rwakatare kuweka zuio mahakamani.

Akizungumzia suala hilo, mjumbe wa kamati, Khatibu Haji (Konde -CUF) amesema kumekuwa na hali ya kulindana katika jengo hilo, huku serikali ikiendelea kuwaonea wanyonge.

“Tunashuhudia Watanzania wanyonge wengi wakipoteza makazi yao na kuishi kwa mahangaiko baada ya kuangushiwa nyumba zao, lakini hakuna kitu chochote kinachoendelea kuhusu nyumba ya Mchungaji Rwakatare na jambo hili linaibuliwa na kuzimwa kuna nini huko,” amehoji Khatibu.
Amesema haileti picha nzuri kwa serikali kuonyesha inawaonea wanyonge na kuwatetea wenye uwezo jambo linalosababisha kuwagawa watu kwa matabaka.

Khatibu hakuwa peke yake, Martha Mlata (Viti Maalumu – CCM) alitaka hatua kali zichukuliwe kwa waliomruhusu Rwakatare kujenga katika eneo lisiloruhusiwa kisheria.

“Huu ni uonevu ambao haupaswi kuvumiliwa. Macho na masikio ya Watanzania yamechoka kusikia nyumba za wanyonge zikivunjwa lakini serikali inaendelea kulinda hekalu la mtu mmoja ambalo limejengwa mahali pasipohusika. Haikubaliki hata kidogo, kuna nini katika nyumba ya Mchungaji Rwakatare,” amehoji Gimbi Masaba (Viti Maalumu -Chadema).

No comments: