Tuesday, October 10, 2017

ZITO KABWE AFUNGUKA HAYA BAADA YA OFISI YA TAKWIMU KUTOA TAARIFA ZA KUSHUKA KWA SHILINGI

Jana Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilitoa taarifa yake juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, taarifa iliyolewa inaonyesha hali si nzuri, uchumi wa nchi yetu unaonyesha kusinyaa na kudidimia, mfumuko wa bei unaonyesha kupanda na thamani ya shilingi kudidimia.
     Picha inayohusiana
Taarifa hiyo inaonyesha namna hali ya uchumi wetu inavyozidi kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wa hali ya chini , kwa mfumuko wa bei umepanda mno tangu kuanza kwa utekelezaji wa bajeti ya 2017/18, ongezeko ambalo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula (bidhaa ambazo wananchi wengi zaidi wanazitumia).

Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni dagaa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi kwa (3.1), viazi vitamu kwa (3.0), mchele (1.5) na ndizi (1.5). Bidhaa nyingine zilizochangia ni mkaa kwa asilimia 4.0, dizeli (2.4) na petroli (0.6). Ukizitazama bidhaa zote hizi ni zile ambazo zinatumiwa zaidi na wananchi wa kawaida kabisa. Hivyo gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida zimepanda mno, ufukara kutopea na familia zitakazoweza kupata angalao milo miwili kwa siku kupungua zaidi.

Taarifa imeonyesha thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka, uwezo wa Tsh. 100 kununua bidhaa umeshuka hadi Tsh. 92.18. Maana yake ni kuwa mwaka 2016 shilingi 100,000 ilikupa bidhaa za shilingi 100,000. Mwaka huu 2017 shilingi 100,000 inakupa bidhaa za shilingi 92,000. Kwa hiyo ili upate bidhaa za shilingi laki moja inakubidi uongeze shilingi elfu 8 zaidi. Kiuchumi, ili kulinda hali za wananchi, mishahara ilipaswa kupanda kwa asilimia 8 ili kuwapunguzia maumivu ya gharama za maisha.

Lakini hali hiyo inatokea katika wakati ambao mishahara haijapanda, na Rais wa nchi yetu kasema Serikali anayoingoza haitapandisha kabisa mishahara. Hali ni mbaya mno mtaani, mijini uzalishaji wa bidhaa za viwanda umeshuka kwa zaidi ya nusu, kutoka trilioni 1.5 mpaka bilioni 700 tu. 

Siku za karibuni tumeshuhudia makampuni yakipunguza wafanyakazi na mengine kufungwa. Pia Serikali yenyewe ilipunguza watumishi iliyowaita hewa na wenye vyeti feki. Hivyo hivi sasa kuna Watanzania wengi mtaani ambao hawana shughuli zinazowaingizia kipato, tayari Wawekezaji wakubwa nchini wameshaitaka Serikali kutazama upya utendaji wake ili kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ambao unashuka mno.

Vijijini tunashuhudia ushukaji wa sekta ya Kilimo kuliko wakati wowote ule tangu baada ya Uhuru. Wakulima wa Korosho hawajapewa pembejeo, hivyo uzalishaji wa zao linalotuingia mapato ya Kigeni zaidi nchini utashuka msimu huu wa mavuno, Tumbaku (zao la pili Kwa kuingiza Fedha za kigeni) tayari wakulima wanalia, mazao ya choroko na kunde bei imeshuka kwa zaidi ya 500%, Pamba uzalishaji umeshuka Kwa 63% kati ya mwaka 2015 na 2017 (miaka miwili ya awamu ya tano), Karafuu nayo mauzo yameshuka zaidi, na mauzo Nje ya dhahabu kuanza kushuka na hivyo kupelekea shilingi kushuka thamani na hivyo mfumuko wa bei kupanda Kwa kasi. 

Nini Kifanyike?

1. Serikali itazame namna inatekeleza mipango yake ya Maendeleo. Uwekezaji kwenye miradi mikubwa ni jambo jema sana nchini kwani miradi mikubwa huingiza fedha kwenye mzunguko na hivyo kuchochea uchumi. Hata hivyo maarifa yanatakiwa kwenye miradi hii. Hapa nchini kwetu miradi mikubwa inaondoa Fedha kwenye uchumi na kupeleka Nje ya Nchi, tena Kwa Fedha za kigeni. Mfano Reli na Ndege ni miradi inayoondoa Fedha Nchini kwa dola na sio kwa madafu. Badala ya miradi hii kuwa ahueni inakuwa hasara kwa Nchi yetu.

2. Serikali isikilize na kufanyia kazi mawazo ya sekta binafsi katika kuweka sawa mazingira ya Uwekezaji bila kupoka haki ya Nchi kufaidika na rasilimali zake. Kwa mfano hoja aliyotoa Ndugu Dangote sio ya kupuuza kwani kwa kawaida Mitaji huona aibu (capital is shy). Serikali ijiondoe kwenye mentality kuwa Uwekezaji ni kupata kodi tu, la hasha. Kwa demografia ya Tanzania, ambapo watu milioni 1.6 huingia kwenye soko la ajira kwa mwaka, Ajira yapaswa kuwa lengo kubwa la Serikali katika kuvutia mitaji kutoka nje na vile vile ndani.

3. 3 Serikali ifanyie kazi haswa uchumi wa vijijini kwa kurekebisha mapungufu yote yanayoshusha uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, kuanzia pembejeo, masoko na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya mazao (agro processing industries).

Kwa Watanzania wenzangu,

Kama Kiongozi wa watu hali hii ya kudidimia kwa uchumi wetu inaniumiza sana, nayaelewa maumivu mnayoyapata wananchi, wajibu wangu ni kupaza sauti ili Serikali ichukue hatua kupunguza makali haya ya hali mbaya ya uchumi. Mimi na chama ninachokiongoza, ACT Wazalendo, hatutaacha wajibu huo wa kuyasemea masuala yenu wananchi, hiyo ni ahadi yetu kwenu wananchi, tutaendelea kuwasemea.

No comments: