Thursday, November 2, 2017

RC MAKONDA ATOA MAAGIZO HAYA KWA TANESCO KUTOKANA NA KUKATIKA OVYO KWA UMEME DAR ES SALAAM

Wafanyakazi wa shirika la kuzalisha na kusambaza umeme nchini  Tanesco wametakiwa kujipanga imara ili kuweza kukabiliana na maafa  yatokanayo na mvua kubwa zinazonyesha kwa kipindi hiki.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh. Poul Makonda alipofanya mkutano na waandishi wa habari pamoja na Wakurugenzi wa Tanesco lengo likiwa ni kuwatoa hofu wakazi wa jiji la Dar es salaam ya kukatika kwa umeme kutokana na mvua zinazonyesha kwa sasa.

Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa alilitaka shirika hilo kuwa na kauli thabiti zinazoendana na ukweli kwa wateja wao ili kupunguza matatizo makubwa ya watu kufariki kutokana na umeme kuingiliana na mvua.
Endapo itatokea nguzo imedondoka au kunahitirafu basi wafike mapema eneo la tukio kabla tatizo halijawa kubwa, na kama itatokea tatizo likakaa kwa zaidi ya siku mbili au tatu na taarifa wanazo basi wananchi walete taarifa hizo katika ofisi yake na yeye atalishughulikia mara moja tatizo hilo.

Aidha mkuu wa mkoa huyo alilitaka shirika hilo kuhakikisha usalama unakuwepo kwa wakazi wa mabondeni na kwa wale ambao hawastaili kuwepo na umeme kwa kipindi hiki cha mvua basi wakatiwe na kwa wale wa maeneo mengine wanaohitaji huduma hii wapewe kama inavyostahili.

Lakini pia kwa upande wake Meneja muandamizi wa  Tanesco Kanda ya Dar es salaam na Pwani  Bw.  Mahende Mgaya alisema kuwa kwa takribani wiki mbili zilizopita kulikuwa na tatizo la kukatika kwa umeme na hii ilitokana na Gridi kubwa kudondoka na kusababisha hitilafu moja ni ya Ubungo na ya pili ni ya Kidatu.
Mkurugenzi huyo aliendelea kwa kusema kuwa kwa mitambo yao iliyopo maeneo ya Segerea ilikuwa na tatizo la kuvuja kwa mafuta hivyo kusababisha watu kukosa umeme kwa takribani siku tatu, na hii ilifanya mafundi kufanya kazi usiku na mchana na mpaka sasa hali ni shwari na tatizo hilo limekwisha kabisa.

Kutokana na mvua kubwa zinazonyesha kwa sasa “Tumefanya matengenezo makubwa ikiwa ni kuondoa miti yote iliyokuwa karibu na line lakini pia tumetengeneza magenge maalum ambayo yatakuwa standby kwa kusaidia endapo litatokea tatizo la kuhitaji msaada wa haraka”.alisema Mahende

Na mwisho kabisa alisema kuwa kwa wakazi wa wilaya za Kigamboni na Temeke wakae tayari kwani mradi wao wa kuweka kituo pale Mbagara unaendelea vizuri na karibu utakamilika na wakandarasi wanasema mpaka mwezi wa 12 mtambo huo utawashwa rasmi.

No comments: