- Mfumo mpya unawapa wakulima wa korosho uhakika, usalama na urahisi wa kupata malipo yao na kuweka akiba.
- Zaidi ya vyama vya ushirika vya msingi 40 katika mikoa ya Lindi na Mtwara vyaingia mkataba wa kuanza kupokea malipo ya korosho kupitia Tigo Korosho
Mtwara, 16 Novemba, 2017.
Wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameanza kufurahia uhakika, usalama na urahisi wa kupata malipo kwa mavuno yao ya korosho baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Tigo, utakaowawezesha kupokea malipo kwa msimu wa korosho wa mwaka 2017/2018 kupitia huduma mpya ya kutuma na kupokea pesa ya Tigo Korosho, inayopatikana kama sehemu ya mfumo wa Tigo Pesa.
Tigo Tanzania, kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali nchini imezindua huduma mpya ya kipekee ya ‘Tigo Korosho’, itakayowezesha wakulima wa korosho kupata malipo ya mazao yao moja kwa moja kwenye simu zao za mkononi. Kwa kuanzia, Tigo imeingia mkataba utakaowezesha wanachama wa vyama vya ushirika vya msingi 40 kuanza kupokea malipo ya mazao yao ya korosho kwa msimu wa 2017/2018 kupitia huduma ya Tigo Korosho.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini na kuzindua huduma ya Tigo Korosho iliyofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara leo mchana, Mkurugenzi wa Tigo – Kanda ya Pwani, George Lugata alisema kuwa huduma ya Tigo Korosho inawapa wakulima wa korosho uhakika wa kupokea malipo yao kwa muda muafaka, usalama wa kupokea malipo kwenye simu zao za mkononi hivyo kuondoa hatari inayotokana na kutembea na pesa taslim, urahisi wa kupokea pesa zao wakiwa sehemu yoyote ile nchini, pamoja na uwezo wa kuweka akiba au kuzitumia fedha zenyewe kupitia mtandao mpana wa mawakala wa Tigo pesa uliosambaa nchi nzima.
‘Tunayo furaha kubwa kuwaunganisha wakulima wa korosho kupitia vyama vyao vya ushirika vya msingi na huduma yetu mpya ya Tigo Korosho ambayo ni sehemu ya huduma ya fedha ya Tigo Pesa. Hii ni suluhisho muafaka na rahisi kwa mahitaji yao ya kila siku ya kifedha,’ Lugata alisema.
Ikiwa na zaidi ya mawakala 80,000 waliosambaa katika kila kona ya nchi, huduma ya Tigo Pesa huhamisha zaidi TZS 1.481 billioni kila mwezi. Huduma hii imechangia kukuza upatikanaji wa huduma za kifedha na kukua kwa uchumi wa nchi.
‘Kufikia sasa, zaidi ya shilingi 330 milioni zimeshalipwa kwa vyama vya ushirika vya msingi, hivyo kuwapa wakulima usalama, uhakika na urahisi wa kupokea fedha zao kupitia mtandao wetu wa mawakala,’ Mkurugenzi huyo wa kanda alisema.
Akielezea jinsi mfumo huo wa Tigo Korosho unavyofanya kazi, Mkurugenzi huyo wa Tigo alisema kuwa kwanza wakulima wa korosho wanapaswa kujiunga na vyama vya ushirika vya msingi, na kisha kujisajili kupokea fedha zao kupitia huduma ya Tigo Korosho. Ifikapo kipindi cha mauzo ya korosho, watapokea taarifa za makusanyo, usafirishaji, mnada na mauzo ya korosho zao kupitia vyama vyao vya ushirika vya msingi. Punde tu hela za mauzo ya korosho zinapoingizwa kwenye akaunti husika ya chama cha ushirika cha msingi, Tigo Pesa kupitia huduma ya Tigo Korosho itahamisha stahiki za wakulima moja kwa moja kwenye akaunti zao za simu, ambapo mkulima atapokea ujumbe mfupi wa maneno (SMS) utakaomtaarifu kuhusu kukamilishwa kwa muamala wake wa fedha. Hapo mkulima ana uhuru wa kutoa, kuhamisha au kutumia fedha zake kwa uhuru kupitia mfumo wa Tigo Pesa na mtandao wake mpana wa mawakala.
Mapema mwaka huu, Tigo Tanzania na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT) kwa baraka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitia saini makubaliano yaliyowezesha kuunda, kufanya majaribio na kujifunza kuhusu huduma za kifedha kwa njia ya mtandao kama suluhisho mojawapo ya kero zilizokuwa zinawakabili wanachama wa vyama vya ushirika vya msingi.
Mkuu wa Kilimo na Huduma za Kifedha Kijijini wa FSDT, Mwombeki Baregu amesema kuwa huduma ya Tigo Korosho ni matokeo ya ushirikiano wa wadau mbali mbali wa maendeleo na huduma za kifedha waliokutana na kujadili changamoto, fursa na mapungufu ya upatikanaji wa huduma za kifedha pamoja na huduma ya stakabadhi ghalani. Lengo kuu lilikuwa ni kupata suluhisho muafaka kwa kero zinazowakabili sio wakulima wa korosho tu, bali wadau wengine wa kilimo kwa ujumla.
‘Tumejadiliana na wadau muhimu katika sekta ya korosho na mikoa inayozalisha korosho ili kushugulikia kero ya malipo kwa wakulima. Matokeo yake ni mfumo huu wa kipekee utakaowezesha malipo ya korosho kwa msimu wa 2017/2018 kuwafikia wakulima moja kwa moja kwenye simu zao za mkononi kupitia huduma ya Tigo Korosho,’ alisema.
Katika utekelezaji wa huduma hii, kila chama cha ushirika cha msingi kinatakiwa kuingia katika mkataba wa moja kwa moja na kampuni ya MIC Tanzania Ltd – inayomiliki mtandao wa Tigo, ambapo mpango huu unaanza kutekelezwa kupitia vyama 40 vya ushirika vya msingi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa alisema kuwa lengo kuu la mradi huu ni kushugulikia kero ya muda mrefu ya kupata malipo kwa muda muafaka iliyokuwa inawasumbua wakulima wa korosho, pamoja na kutatua tatizo la upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo ya vijijini.
‘Ningependa kuwahakikishia wakulima wote kuwa mpango huu una baraka zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kabla ya kuanza kutekelezwa, mikataba yote kati ya MIC Tanzania Ltd na Vyama vya Ushirika vya Msingi kwanza lazima ipitiwe na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kama msimamizi wa vyama vya ushirika Tanzania. Pia tumehakikisha kuwa viongozi wote wa vyama vya ushirika vya msingi wanajengewa uwezo na wana uelewa wa kutosha kuhusu mfumo huu wa Tigo Korosho na jinsi ya kuutumia kwa manufaa ya wanachama wote na Taifa kwa ujumla,’ alisema.
Mpango huu unatekelezwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Tigo, Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Benki Kuu ya Tanzania na Serikali kupitia Tawala za Mikoa ya Lindi na Mtwara.
No comments:
Post a Comment