Wajasiriamali wa nchi za Afrika ya Mashariki wametakiwa kuitumia ipasavyo fursa ya kuenea na kukua kwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya mapinduzi ya biashara duniani kote.
Hayo yalisemwa kwenye semina kuhusu “Biashara za Mtandaoni” ikiwa na lengo la ‘kuongeza ufikiaji wa soko na kukuza mbinu za kibiashara kupitia mtandaoni,’ katika mkutano wa pili wa Maonyesho ya Afrika ya Mashariki ya Biashara na Ujasiriamali mwaka 2017 (EABECE) uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 14 mpaka Novemba 16.
Akizungumza kama mmojawapo wa jopo la wazungumzaji wakati wa semina hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Jumia Tanzania, kampuni ambayo inajihusisha na biashara ya manunuzi na uuzaji wa bidhaa mtandaoni, Bw. Albany James amesema kuwa changamoto kubwa wanayopambana nayo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba inawashawishi wafanyabiashara wote kuhamia kwenye mfumo wa mtandaoni ili kuwafikia wateja wengi zaidi.
“Kikubwa tunachokifanya ni kuwakutanisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali na wateja mtandaoni. Kupitia uwekezaji mkubwa wa teknolojia tulioufanya, tumedhamiria kuwapatia wauzaji na wanunuaji urahisi mkubwa sawasawa na kama wanavyokwenda madukani,” alisema na kuhitimisha Bw. James, “Tunafahamu kwamba kwenye biashara ili kufikia soko kwa urahisi ni lazima uwajue wateja wako na namna ya kuwafikia ambapo mara nyingi ni kwa njia ya matangazo. Lakini sio wafanyabiashara wote wanaweza kulimudu ukizingatia wengi ndio wanaanza na hawana mitaji au faida kubwa ya kuwekeza kwenye matangazo. Hivyo basi, Jumia tunachokifanya ni kuwapatia fursa ya kujitangaza kwa njia ya mtandao bila ya gharama yoyote kwani ndipo kwenye idadi kubwa ya watu kwa hivi sasa.”
Naye kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Umma na Masoko wa Jumia Travel Tanzania, Bw. Kijanga Geofrey, kampuni dada ya Jumia Tanzania ambayo yenyewe inajihusisha na utoaji wa huduma za hoteli mtandaoni nchini na barani Afrika kwa ujumla, ameongezea kuwa fursa iliyopo kwa wafanyabiashara kuhamia mtandaoni ni kubwa na haina gharama kama wengi wanavyofikiri.
“Wafanyabishara wengi bado ni waoga wa kutumia teknolojia kwenye kukuza na kurahisisha biashara zao. Ripoti zinaonyesha kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi 20 zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani ambao kwa kiasi kikubwa unachangiwa na sekta za utalii, ujenzi, fedha na biashara ukiacha na nyinginezo. Lakini kikubwa zaidi ni ukuaji wa TEHAMA ambapo takwimu zinaonyesha 40% ya watanzania wamefikiwa na mtandao wa intaneti ambapo wameongezeka na kufikia milioni 19.86 mwaka 2016 kutoka milioni 17.26 mwaka 2015. Takwimu hiyo pia imechochea kuongezeka kwa watumiaji wa simu za mkononi na kufikia milioni 40.17 mwaka 2016,” alisema Bw, Geofrey.
“Hilo ni sawa na ongezeko la 0.9% kwa mwaka na ukuaji wa ueneaji kwa 83% kwenye nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 50. Hii ni dhahiri kwamba kuna mustakabali mkubwa kwa ukuaji wa biashara za mtandaoni kwenye sekta mbalimbali. Kwa sasa mawasiliano ya simu ni mojawapo ya sekta zinazokua kwa kasi nchini Tanzania na inatoa mchango mkubwa katika kuwaunganisha watanzania kwenye mfumo wa kifedha. Kwa kuongezea, idadi ya watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu nayo imeongozeka na kufikia milioni 18.08 mwaka 2016 kutoka milioni 17.63 mwaka 2015. Hizi zote ni ishara kwamba watanzania wapo tayari kwa biashara za mtandaoni kitaalamu na kisaikolojia,” alihitimisha Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma na Masoko wa Jumia Travel Tanzania.
Akitoa maoni yake wakati wa semina hiyo mmoja wa washiriki, Bi. Isabella Mwampamba ambaye mbali na kuwa ni mjasiriamali lakini pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Upendo Friends iliyopo jijini Arusha, amesema kuwa wanawake wengi ni waoga wa kutumia teknolojia za mtandaoni zilizopo sasa kitu ambacho kinawaacha nyuma na kuwanyima fursa nyingi.
“Mimi kama mmojapo wa wanawake wajasiriamali nchini Tanzania ningependa kusema kuwa wengi miongoni mwetu ni waoga wa kutumia teknolojia za kisasa. Kwa mfano, wengi tunaogopa hata kutumia simu za kisasa ambazo ni rafiki na mifumo ya mtandaoni! Lakini kwa upande mwingine sio makosa yetu kwani tunakosa mafunzo ya kitaalamu ya namna ya kuzitumia,” alisema Bi. Mwampamba na kuhitimisha, “Hivyo basi ningependa kutoa wito kwa wanawake na wajasiriamali wenzangu kwamba tuanze kuzitumia teknolojia hizi zilizopo sasa kwani zitatufungua zaidi na kuongeza tija kwenye biashara zetu. Lakini pia natoa wito kwa makampuni ambayo yanajihusisha na sekta hii kuwakusanya na kutoa mafunzo ya mara kwa mara juu ya namna biashara za mtandaoni zinazofanya kazi.”
Mkutano wa Maonyesho ya Afrika ya Mashariki ya Biashara na Ujasiriamali mwaka 2017 (EABECE) unalenga kutoa fursa kwa kuzikutanisha sekta za biashara na wenzao kwenye biashara pamoja na serikali na sekta za biashara. Ni jukwaa linalowakutanisha kwa pamoja wafadhili wa kifenda na wavumbuzi kwa lengo la kuimarisha ujasiriamali katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambapo mwaka jana ulifanyika Oktoba 10 mpaka 13 jijini Nairobi, Kenya.
No comments:
Post a Comment