Wakazi wa
jiji la Dar es salaam wametakiwa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika
mikutano inayoitishwa na serikali zao za mitaa hasa katika kipindi hiki cha
kuahinisha vipaumbele katika bajeti kuu ya taifa.
Hayo
yamesemwa mapema jana jijini Dar es salaam na muwezeshaji ambae pia Mchumi
kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bi. Lucy Kayombo alipokuwa akiwasilisha
mada katika semina ya jinsia na maendeleo iliyofanyika makao makuu ya mtandao
wa jinsia Tanzania(TGNP).
Bi. Lucy
alisema kuwa ni vema kwa wananchi kujitolea kushiriki kwa wingi kwani ni haki
yao ya msingi na mfumo wa sasa siyo kama wa zamani ambapo kila kitu kilikuwa
kinaamuliwa na serikali kuu na huku chini zinakadiliwa fedha kwa ajili ya
utekelezaji tu.
Lakini kwa
sasa mfumo huo umekuwa shirikishi kwa kuwapa wananchi fursa ya kupanga
vipaumbele vyao kuanzia ngazi ya mtaa, kata, halmashauri mpaka serikali kuu na
kuhoji kwa viongozi wao pale wanapoona vipaumbele vyao vinapuuziwa au hawapewi
nafasi ya kushiriki katika mipango ya kuunda bajeti.
Aidha mchumi
huyo aliwataka washiriki wa semina hiyo kwenda kuuliza katika ofisi za mitaa
yao kuwa wataanza lini zoezi hilo kwani muda ndio huu kuanzia mwezi novemba
mpaka februari zoezi hilo linatakiwa kuwa katika ngazi ya mitaa na baada ya
muda huo linaama na kwenda ngazi ya kata hivyo wanatakiwa kuhoji lini litaanza.
Na mpaka
kufikia mwezi marchi zoezi hilo linahama kutoka serikali za mitaa na kwenda Kata
na kufikia april linaondoka kutoka kata na kwenda katika ngazi ya Halmashauri
ambapo wananchi muda wao unakuwa umekwisha wanachosubiri ni kuona vipaumbele
gani vilivyopitishwa na kusubiri waone bajeti ya mwaka husika imetenga kiasi
gani katika kutatua matatizo yao.
Muwezeshaji
huyo aliendelea kusema kuwa tatizo kubwa na hasa kwa maeneo ya mijini ni kwamba
kila mtu anajikuta ana mambo mengi hali inayosababisha kutohuhuria na walio
wengi ukiwauliza mchakato umeanza hawajui au kwa mwaka uliopita mliweka
vipaumbele gani anakosa jibu kutokana kwamba hana muda wa kushiriki katika
zoezi muhimu kama hilo.
Lakini pia
washiriki wa semina hiyo wamedai kuwa swala la uwajibikaji kwa viongozi wao
limekuwa ni dogo kwani hawaitishi mikutano kama hii kwa kuwa wanajua watu wa
mijini hawana utamaduni wa kuhoji, lakini pia hata wakiitisha hawatoi taarifa
vizuri watu wote wakajua na kwamba wakiitisha vikao basi unakuta ni mchango wa
taka taka au ulinzi shirikishi.
Na jambo
lingine lililoonekana kuwa tatizo kubwa ni kuhama hama, kwani unakuta mtu kwa
mwaka amehama kata mbili au zaidi hali
inayofanya ashindwe kwenda kuhoji katika mtaa aliotoka na kuwa vipaumbele vyao
vimefanyiwa kazi au wasubiri katika awamu ijayo ya fedha.
No comments:
Post a Comment