Friday, April 13, 2018

UJUMBE WA SHEIKH JALALA KWA WATANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MERAJI

Watanzania wametakiwa kupendana kushirikiana na kushikamana bila kuangalia itikadi ya dini zao ili kuendelea kuenzi amani na upendo uliopo nchini kwa sasa.
Kiongozi  Mkuu wa Dhehebu la Shia nchini Maulana Hemed Jalala akiongea na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam, pembeni yake ni Sheikh Muhammad Abdu ambaye ni Kaimu Mkuu wa chuo cha Kiislam Hawzat Imam Swadiq(AS)
Hayo yamesemwa mapema leo jijini Dar es salaam na Kiongozi Mkuu wa Dhehebu la Shia nchini Maulana Hemed Jalala, ikiwa leo maadhimisho ya siku ya Meraji duniani kote.

Sheikh Jalala alisema kuwa siku ya Meraji ni siku ya kuhamasisha amani na upendo vilivyopotea katika nchi Palestina, kwani mitume wote walioishi katika ardhi hiyo walikuja kwa lengo moja la kuleta amani katika nchi hiyo na dunia kwa ujumla.

Aidha Maulana huyo aliendelea kusema kuwa siku ya Meraji ni siku ya mshikamano kwa watu wa dini zote ikiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi kwa pamoja kuendelea kutetea na kulinda amani na mshikamano vilivyopotea ndani ya nchi ya Palestina.
Mkutano ukiendelea.
Pamoja na hayo Sheikh huyo alisema kuwa nchi ya Palestina ni nchi ya kihistoria kwa kuwa mitume wengi waliotumwa na mungu waliishi hapo akiwemo Isaka, Yakubu Mtume Mohamad (S.A.W) na hata Ibrahimu Baba wa mataifa yote alizikwa katika ardhi hiyo.

Lakini pia vitabu vinavyotumiwa na dini zote kubwa ikiwemo Injiri, Torati, Zaburi, na hata Quran vilishuka katika nchi hiyo na vinaimiza Amani Upendo na Ushirikiano, hivyo basi kama binadamu tunajukumu kubwa la kuhakikisha vitu hivyo wanavipata wananchi wanaoishi Palestina”. alisema Sheikh Jalala

Akiongea kwa upande wa Watanzania alisema kuwa Watanzania tukiwa na sifa ya kuwa kisiwa cha Amani tunapaswa kuilinda na kuitetea Amani yetu tusikubali Amani hii ikapotea kirahisi rahisi na tuzidi kuwaombea viongozi wetu watuongoze katika haki na usawa ili kuendelea kuilinda Amani yetu.

"katika kuangalia haya yote yanayotokea nchini ya Palestina kwa sasa sisi kama watanzania tunajifunza kwa namna gani tuilinde na kuitetea amani na yetu na tusikubali kuipoteza kwani ni Tunu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu" alisisitiza Sheikh Jalala
Baadhi ya waandishi wa habari na wageni waliohudhuria mkutano huo.
Na mwisho kabisa Maulana Jalala alitoa wito kwa jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa mataifa na jumuiya mbalimbali za kimataifa kuliangalia tatizo la Palestina kwa jicho la ukaribu zaidi kwa kutetea maslahi na haki za wakazi wa nchi hiyo wanaoteseka kwa sasa wakiwa katika nchi yao.

No comments: