Friday, September 9, 2022

TALGWU yaiomba Serikali kufanya Mabadiliko Tozo Miamala ya Kibenki

Na Isaac Thadeo

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeiomba Serikali kufanya mabadiliko katika sheria ya tozo za miamala ya kibenki ili kuepuka malipo ya mara mbili kwenye mshahara wa mtumishi wa umma. 
Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Shani Kibwasali akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Ombi hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa-TALGWU Shani Kibwasali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chama kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2022.

Shani amesema tozo hizo zinazidi kumbebesha mzigo na kumkandamiza mfanyakazi huku ikizingatiwa mishahara wanayopata haikidhi mahitaji ya kila Siku na familia zao. 

“Pia naomba nizungumzie suala la tozo za kibenki lililoanza kutekelezwa hivi karibuni. Tozo hizi zinawaathiri sana wanachama Wetu. Ikumbukwe kwamba watumishi wa umma kila mwezi wanalipa Kodi kwa kukatwa katika mishahara yao,” amesema Kibwasali na kuongeza kwamba,

“Lakini sasa kuanza kuanza kutekelezwa kwa tozo ya Serikali kwa miamala ya kutoa na kuhamisha fedha katika benki inamfanya mtumishi wa umma kutozwa zaidi ya mara mbili katika Pato moja kwa mwezi,”.

Kuhusu suala la nyongeza ya mishahara, amesema ni ukweli usiofichika kwamba wanachama wao ambao ni wahanga wakubwa kwani bado wanamanung’uniko na TALGWU kama msemaji wao hawajaridhika kabisa kwa jinsi nyongeza ya mshahara ilivyofanyika.

“Ila naomba niwatoe hofu wanachama wetu kwamba suala hili linashughulikiwa na Chama kwa kushirikiana na shirikisho la vyama huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA),” ameeleza Kibwasali.

Akizungumzia kuhusu mafanikio ya TALGWU kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, amesema kwamba hadi kufikia Juni 2022 walikuwa na jumla ya kesi 140 ambapo mawakili wa Chama wanasimamia kesi 100, mawakili wa nje wanasimamia kesi 13, na rufaa zilizopo Tume ya Utumishi wa Umma ni 27.

Kwamba Chama kiliandaa utetezi kwa watumishi 12 waliokuwa wamepewa mashataka na waajiri. Hivyo amesema kati ya kesi 140 walizonazo zilizoisha zilikuwa ni 39 na chama kimeshinda jumla ya kesi 35 na kushindwa kesi nne huku kesi nyingine zikiendelea Mahakamani.

Kibwasali amebainisha kuwa katika kipindi hicho pia TALGWU ilikuwa na jukumu jingine kubwa la kushughulikia haki na stahiki za wanachama ambazo kimsingi zipo kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

Hivyo amesema TALGWU inajivunia kuona Serikali imetekeleza maombi yao katika maeneo ya upandiahaji vyeo na mishahara, malipo ya malimbikizo ya mishahara na utawala Bora.

No comments: