Friday, October 12, 2012

Hatua alizochukua Mnyika (Mb) kuhusu matatizo ya maji Goba



          NIMECHUKUA HATUA YA KUWASILISHA  KWA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA SUALA LA MATATIZO YA MAJI KATIKA  KATA YA GOBA ILI HATUA ZA HARAKA NA ZA KUDUMU ZICHUKULIWE
Kazi ya mbunge ni kuwakilisha  wananchi, kushiriki katika kutunga sheria na kuisimamia serikali ili kuwezesha  maendeleo kwa pamoja na mambo mengine kuhakikisha huduma za kijamii ikiwemo  upatikanaji wa maji zinaboreshwa.
    Tarehe 10 Oktoba 2012 ikiwa ni sehemu  ya kufanya kazi hiyo nimekwenda kwa niaba ya wananchi Tume ya Haki za Binadamu  na Utawala Bora na kuwasilisha malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu za  kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika uendeshaji  wa miradi ya maji kwenye kata ya Goba katika Manispaa ya  Kinondoni.
Tatizo la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi  cha miaka  mingi kabla ya mimi kuchaguliwa kuwa mbunge, pamoja na kwamba  serikali inaowajibu wa kuhakikisha inalinda haki ya kupata maji lakini  Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeshindwa kulinda haki hii kwa wakazi wa  Goba.
Ifahamike kuwa miongoni mwa haki za kijamii  kwa mujibu  wa  Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni  (“The International Covenant on Economic, Social and  CulturalRights”,  ICESCR ) wa 1966 ni pamoja na haki ya  kupata maji safi na salama.

       Hata hivyo  katika nchi yetu   inaonekana haki ya kupata maji safi na salama haitiliwi mkazo pamoja na Tanzania  kutambua na kuridhia mkataba huo hivyo malalamiko haya ya lengo la kuwezesha  tume kusimamia haki za msingi za binadamu na utawala bora katika sekta ya  maji.
Ikumbukwe  kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya  Mwaka 1977, toleo la mwaka 2005 Ibara ya 130 (b)  na (c) inaeleza majukumu  ya Tume ya Haki za binadamu na utawala bora kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko  ya uvunjaji wa haki za binadamu  na kufanya uchunguzi juu ya mambo  yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa utawala  bora.Izingatiwe kuwa Sheria ya Haki za binadamu na Utawala  Bora  namba  7 ya mwaka 2001 kifungu cha 22(1) kinaruhusu malalamiko  kwa njia ya maandishi ;

Na Irejewe kuwa kuwa kifungu cha 15(1) (b)  (iii)  cha Sheria ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, sheria namba 7 ya  mwaka 2001, kinaipa nguvu Tume kuchunguza uvunjaji wa Haki za Binadamu   ikiwa itapokea malalamiko kutoka kwa mtu anayefanya hivyo kwa niaba ya kundi la  watu.

Kwa kutumia  mamlaka na matakwa ya Ibara ya 130 ya Katiba ya  Nchi na vifungu vya 15 na 22 vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na utawala  bora na kwa kuzingatia mikataba ya haki za binadamu ambayo nchi yetu imeridhia  nimetaka tume ichukue hatua zifuatazo:

      Mosi;  Ichunguze na kuchukua  hatua dhidi ya waliohusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi  kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kushindwa  kushughulikia matatizo ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji,  kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti  iliyopitishwa na tuhuma za ufisadi, uzembe na udhaifu wa kiutendaji katika  kamati za maji, ngazi ya kata na kwenye idara ya maji ya Manispaa ya  Kinondoni.

      Pili; Pamoja na kuchukua hatua kwa wahusika waliosababisha  uvunjaji wa haki ya msingi ya wananchi kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa  haki za binadamu; Tume ya Haki za Binadamu ipendekeze hatua za haraka  zinazopaswa kuchukuliwa na Manispaa ya Kinondoni kuwezesha huduma ya maji  kurejea kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa maji kwa  wananchi wa Kata ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa upangaji,  utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji katika Manispaa ya  Kinondoni.

           Tatu; Aidha, zaidi ya hatua za dharura Tume ya Haki za  Binadamu ipendekeze hatua za ziada ya kuchuliwa na Manispaa ya Kinondoni  kuwezesha kata ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya  Kinondoni na badala yake ihudumiwe na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es  salaam (DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam  (DAWASCO) ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu kwa ajili ya ufumbuzi wa  kudumu.

            Nne, Tume ichunguze na kupendekeza masuala mengine ya  kushughulikiwa na mamlaka zingine zinazohusika ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa  Nishati na Maji (EWURA), Wizara ya Maji na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu  masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa misingi ya utawala bora  katika miradi ya maji kwenye kata ya Goba pamoja mfumo wa upatikanaji wa maji  kwa ujumla.
Wenu katika kuwakilisha wananchi,

No comments: