Friday, October 12, 2012

Umoja wa Ulaya watunukiwa Nishani ya Amani ya Nobel



      Umoja wa Ulaya umetunukiwa tuzo ya mwaka huu ya amani ya Nobel baada ya Kamati ya Nobel nchini Norway kuridhika kwamba Umoja huo umekuwa katika mstari wa mbele kupigania na kueneza demokrasia Ulaya na duniani kwa jumla.    


Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Nobel, Thorbjorn Jagland  amesema cha msingi kilichowafikisha katika uamuzi wa pamoja wa kutoa tuzo hiyo kwa Umoja wa Ulaya ni juhudi za Umoja huo za kuleta amani na maridhiano pamoja na demokrasia katika Umoja huo baada ya vita vya pili vya dunia

Tuzo hiyo inaonekana kama hatua ya kuupa nguvu na mori muungano huo wakati ukiwa katika mapambano ya kuutatua mgogoro wake wa madeni. Kamati hiyo imezipongeza nchi wanachama 27 kwa kuujenga upya umoja wao baada ya Vita vya Pili vya Dunia pamoja na kazi iliyoifanya  katika kueneza utulivu katika nchi zilizokuwa za Kikomunisti baada ya kuangushwa ukuta wa Berlin mwaka 1989.

Tuzo ya Amani ya Nobel inayoambatana na zawadi ya fedha dola milioni 1.2 itakabidhiwa rasmi kwa Umoja huo katika sherehe itakayofanyika mjini Oslo, Norway, hapo tarehe 10 Disemba

No comments: