Friday, October 12, 2012

Mapigano na mauaji zaidi nchini Syria

 Waasi wa Syria

      Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria linasema waasi nchini humo wamewauwa wanajeshi 14, katika shambulizi kwenye ngome ya jeshi mjini Daraa hii leo asubuhi.    


Katika tukio hilo la leo asubuhi waasi sita pia waliuwawa kwenye kizuizi kimoja cha kijeshi katika eneo la Khirba. Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu nchini Syria pia limesema kwamba kwa sasa mapigano yanazidi kupamba moto katika miji ya kaskazini Idlib na Aleppo.

       Shirika hilo lililo na makao yake makuu jijini london, awali lilitoa taarifa kwamba jana Alkhamisi kulishudiwa mapigano makali zaidi kuwahi kutokea nchini Syria, tangu kuanza kwa ghasia miezi 19 iliopita, ambapo watu 240 waliouwawa wakiwemo wanajeshi 92, waasi 67 na raia 81. Kati ya wanajeshi waliouwawa hapo jana 36 waliuwawa katika mapigano mjini Idlib. Mji huu umeshuhudia ghasia zaidi katika miezi mitatu iliopita.

               Hii leo ndege mbili za kivita za utawala wa Rais Bashar Al Assad zilishambulia majengo mawili katika mji wa Idlib tangu waasi walipoushikilia mji huo baada ya mapambano makali na vikosi vya serikali kwa takriban saa 48. Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo la kutetea haki za binaadamu Rami Abdel Rahman, waasi walikishambulia kikosi cha jeshi la anga katika barabara kuu inayounganisha mji wa Allepo na Raqa.

No comments: