Wednesday, February 27, 2013

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU ZANZIBAR KULAANI MASHAMBULIZI NAMAUAJI YA VIONGOZI WA DINI PAMOJA NA KUPINGA KAULI ZA UCHOCHEZI DHIDI YAZANZIBAR



Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu Mlezi wa Viumbe. Sala na salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake waongofu na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.

Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar lililokaa Jumapili tarehe23/2/2013 katika kikao cha kutathmini matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini yakiwemo ya karibuni ya kupigwa risasi na kuuliwa Padri Mushi pamoja na kupigwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje na kuendelea kutolewa kwa kauli za uchochezi dhidi ya Zanzibar linatamka ifuatavyo:

1. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani vikali na kwa nguvu zote matukio ya kushambuliwa na kuuliwa viongozi wa Dini likiwemo tukio la karibuni la kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi kulikofanywa na wahalifu wasioitakia mema Zanzibar.


2. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linapenda kuweka wazi kuwa uhai ni tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyotunukiwa binaadamu hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa haki hiyo isipokuwa yeye mweyewe Mwenyezi Mungu. Kutokana na ukweli huu ndio maana Sheria za Kiislamu zimeweka wazi mtu mwenye kumuuwa mwenziwe naye auliwe kama inavyoelezwa katika Kitabu kitufu cha Quran kama ifuatavyo:

“Na humo (katika Taurati) tuliwaandikia ya kwamba mtu (huuwawa kwa sababu yakuuwa mtu) kwa mtu, ……….” (5:44)

Hivyo, vitendo vya kiharamia vya kushambuliwa viongozi wa Dini kulikoanziakwa kumwagiwa tindikali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje kwa dhulma kulikofanywa na wahalifu ni jambo lisilokubalika na Uislamu na Waislamu wenyewe. Aidha wahusika wa matendo haya wawe wafuasi wa Dini yoyoteile bado watahesabika ni wahalifu kwani vitendo vya kihalifu na kiharamia kamwehaviwezi kunasibishwa na Dini fulani.

3. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombohusika kufanya upelelezi wa kina kuhusu matukio haya kwa kuzingatia uadilifu namisingi ya kazi zao ili kuwabaini wahalifu na kufikishwa katika vyombo vyakisheria. Aidha Baraza linavitahadharisha vyombo hivyo kuepuka kufanya kazi yaokwa kusukumwa na matashi binafsi, jazba, chuki, matashi ya baadhi ya wanasiasana viongozi wa Dini pamoja na shindikizo la baadhi ya vyombo vya habari.

4. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani na kupinga kwa nguvu zake zote kauli aliyoitoa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na baadhi ya vyombo vya habari kuihusisha Zanzibar na ugaidi kutokana na tukio la kuuliwa Padri Mushi. Kauli hii inaonesha kuwa Mheshimiwa Waziri anaibagua Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu tunavyoelewa sisi suala la usalama wa nchi ni suala la Muungano hivyo huwezi kuihusisha Zanzibar pekee na suala la ugaidi. Hivyo, Baraza linaona kuwa kauli hizi zinazotolewa ni mbinu za makusudi za kuichafua Zanzibar katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na chuki binafsi dhidi ya Zanzibar na watu wake.

5. Aidha Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linamtaka Mheshimiwa Waziri kwa kulinda heshima yake kuwajibika kwa Watanzania kwa kujiuzulu kutokana na kushindwa kulinda usalama wa wananchi wakiwemo viongozi wa Dini ambao ndio walezi wa jamii.

6. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linalaani kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari zinazochochea chuki, uadui, uhasama na mtafaruku kati ya Waislamu na Wakristo na kusahau kuwa Waislamu wameishi na Wakristo kwaamani, mapenzi na mashirikiano hapa Zanzibar karne na karne. Baraza linaona kuwa vyombo hivyo vya habari vinatekeleza ajenda ya kuivuruga Zanzibar kwa kuchochea vita vya kidini ili kufikia malengo yao wanayoyajua wenyewe. Hivyo, Baraza linaiomba Serikali kuvidhibiti kwa kuvichukulia hatua vyombo vyote vinavyotumia matukio haya kuchochea uadui na chuki kati ya Waislamu na Wakristo.

7. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaviomba vyombo vya habari vya Zanzibar kuwajibika kwa Wazanzibari wanaolipa kodi kwa kuwapasha taarifa sahihi juu ya matukio muhimu yanayotokea katika jamii yao badala ya wananchi kutegemea kupokea taarifa za upotoshaji na uchochezi kutoka katika vyombo vya habari visivyotutakia mema.

8. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linaziomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwasilisha kwa Watanzania taarifa ya wazi ya matokeo ya uchunguzi wa matukio haya kwa kuanzia na lile la kumwagiwa tindi kali Sheikh Soraga, kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda, kuuliwa Padri huko Musoma, kupigwa risasi na kuuwawa Padri Mushi na kushambuliwa kwa mapanga na kuuliwa Sheikh Ali Khamis Bin Ali Khatibu wa Mwakaje.

9. Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar linawaomba Wazanzibari wote kuwa watulivu katika kipindi hichi ambapo upelelezi wa matukio haya ukiendelea. Aidha Baraza linawasihi Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti zao za kidini kulinda umoja wao na kudumisha amani pamoja na kukataa kugawanywa ilikuwatoa katika ajenda yao ya msingi ya kudai Mamlaka Kamili ya Zanzibar katikaMuungano.

MOLA WETU MTUKUFU TUNAKUOMBA UINUSURU ZANZIBAR NA WATU WAKE DHIDI YA MAADUI WANDANI NA NJE WASIOITAKIA MEMA NCHI YETU

Imesainiwa na:

Sheikh Ali Abdalla Shamte
Amir wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Zanzibar

No comments: