Wednesday, June 19, 2013

BONGO STAR SEACH YAANZA TENA SOMA MIKOA ILIYOPATA BAHATI MWAKA HUU



Kampuni ya simu za mikononi ya Zantel, leo imezindua msimu mpya wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search, mwaka huu ikiwa imejipanga kuwapa vijana wengi zaidi fursa ya kuonyesha na kuendeleza vipaji vyao.
       Msimu huu mpya,ambao utakuwa msimu wa saba toka shindano hilo lianzishwe mwaka 2006, unatarajiwa kujumuisha wadau wakubwa wa muziki, hivyo kusaidia kuwajenga washiriki kwa kuwapa ujuzi zaidi pamoja na kuwajengea ushirikiano utakaowasidia kuendeleza kazi zao za muziki baada ya mashindano.
           Shindano la mwaka huu litakuwa na kauli mbiu ya ‘KAMUA’ ikimaanisha kutumia uwezo wako wote katika kufanya kile unachopenda, litaenda kufanya usaili kwenye mikoa sita ya Mbeya, Arusha, Zanzibar, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.
         Kwa mwaka jana shindano la Epiq BSS lilipata mafanikio makubwa hasa kwa idadi kubwa ya vijana kujitokeza kufanya usaili, na kubwa zaidi ikiwa ni vijana wote walioingia kumi na mbili bora kufanikiwa kutoa nyimbo zao ambazo zimefanya vizuri.
           Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shindano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benchmark Production, Rita Paulsen amesema mwaka huu wana mpango wa kuwafikia vijana wengi zaidi lakini pia kutengeneza wasanii nyota wengi zaidi ukiacha mshindi. “Sote ni mashahidi wa namna shindano hili lilivyopata mafanikio toka ilipozinduliwa miaka saba iliyopita, na hakika kila mwaka tumekuwa tukisogea mbele zaidi, na mwaka huu mpango wetu ni kuzalisha wanamuziki watakaofanikiwa wengi zaidi’
           Shindano la mwaka huu pia litakuwa na vitu vingi vipya, ikiwemo ongezeko la jaji mmoja katika usaili wa mikoani, ambapo jaji huyo atakuwa ni mdau wa mziki kutoka mkoa husika. ‘Kwenye kila mkoa tutakakoenda kufanya usaili tutakuwa na jaji mwenyeji ambaye tunaamini atasaidia kuongeza ladha ya machaguo ya vipaji na hivyo kuhakikisha tunapata vipaji aina tofaouti’ alisema Paulsen.
          Naye Afsa biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan amesema uzinduzi huu wa leo ni furaha kubwa kwa kampuni ya Zantel kwani unaashiria ufunguzi wa milango ya kuwasaidia vijana wengi wa kitanzania kutimiza ndoto zao.

           Kwa mwaka jana pekee Epiq BSS ilifanikiwa kusaili vijana zaidi ya elfu hamsini, jambo ambalo linaonyesha kitu kimoja, kuna uhitaji wa kuwekeza zaidi katika kuwaendeleza vijana’ alisema Khan.
           

            Ikitekeleza ahadi yake ya kuwasaidia vijana baada ya shindano, kampuni ya Zantel iliwarekodia wimbo mmoja mmoja washiriki wote waliongia kumi na mbili bora, ikiwa ni pamoja na kuwapa ziara ya kujitangaza kwenye mikoa mitatu.  ‘Tumefanikiwa kuwajengea vijana hawa msingi wa kazi yao ya muziki, na tuna furaha kusema wengi wao hadi sasa wanafanya vizuri, na huu ndio aina ya udhamini kampuni ya Zantel inapenda kujihusisha nao’ alisisitiza Khan.
         Mshindi wa mwaka huu pia atajinyakulia milioni hamsini pamoja na mkataba wa kurekodi. Katika kuwapa fursa vijana ambao hawatafikiwa na majaji, Zantel pia itafungua laini za kurekodi kwa simu toka siku ya kwanza ya kuanza usaili mikoani, ambapo washiriki watapiga namba 0901551000 ili kujirekodi kwa njia ya simu, au kutuma neno KAMUA kwenda 15530 kupata maelezo zaidi.
         Usaili utaanzia Dodoma tarehe 29 and 30 ya mwezi huu katika ukumbi wa Maisha Club, ikifuatiwa na Zanzibar tarehe 5 na 6 mwezi wa saba katika hoteli ya Bwawani. Mbeya usaili utakuwa tarehe 10 hadi 11 mwezi wa saba pale club Vybes, Mwanza tarehe 14 hadi15 mwezi wa saba Club Fussion, na Arusha itakuwa tarehe 20 hadi 21 mwezi wa saba Club Tripple A ikimalizikia na Dar es Salaam tarehe 26  hadi 28 pale Uwanja wa Taifa.

No comments: