Kwa wiki kadhaa, Mtandao huu,tumekuwa tukiandika taarifa tulizozifanyia
uchunguzi wa kina zikiihusu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Mhusika kwenye sakata hili ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande,
pamoja na viongozi wengine katika Mamlaka hiyo, Wizara ya Uchukuzi na sehemu
nyingine.
Hatuna sababu ya kurejea tulichoandika kwa kuwa ni imani yetu kuwa
wasomaji wameweza kuujua ukweli na uchungu mzito uliofichika ndani ya TPA,
ambayo ni mali ya umma.
Tumeshupalia suala hili si kwa sababu nyingine, bali ni kwa kutambua
dhima yetu kama chombo cha habari, juu ya kuwaeleza ukweli wananchi ili
watambue namna fedha zao zinavyofujwa na genge la wateule wachache.
Tunayaandika haya tukitambua hatari inayotukabili, lakini kwa kuwa
tumedhamiria kulisaidia Taifa letu kupitia taaluma hii, tumejikuta hatuna namna
nyingine, isipokuwa kutekeleza wajibu huo ambao tunaamini ni wajibu halali
kabisa.
Wakati tukiendelea kuanika ufisadi na ubabe wa kutisha ndani na nje ya
TPA, Mkurugenzi Mkuu, Kipande, pamoja na wapambe wake kadhaa wanajitahidi
kutaka kuonesha kuwa maovu mengi yanayofanywa, ukiwamo ufujaji wa mabilioni ya
shilingi, una baraka za Rais Jakaya Kikwete! Tunamuomba Mkurugenzi Mkuu pamoja
na wafuasi wake wote, waache kabisa kumhusisha Rais katika madhambi haya ambayo
ni wao wenyewe walioyaunda.
Tunaweza kutofautiana na Rais Kikwete
katika masuala mengine, lakini kamwe hatutakubali kuona jina la Rais
aliyechaguliwa kwa ridhaa ya Watanzania, anatumiwa na kundi la watuhumiwa wa
uhujumu uchumi na ufisadi kama ngao yao.
Rais Kikwete ameliongoza Taifa hili wakati
ambao kuna mambo mengi mno. Anakabiliwa na changamoto za kutekeleza ahadi zake
na za chama chake kwa wananchi, anakabiliwa na maandalizi ya kuwa na Katiba
Mpya; anahangaika kuboresha mishahara na huduma mbalimbali za kijamii. Haya na
mengine, tunaamini yanamtosha kabisa.
Kwa sababu hiyo, tunamuomba Kipande atambue
kuwa uongozi wake mbovu, si mbovu kwa sababu ya mtu mwingine yeyote, bali ni
yeye mwenyewe. Anastahili kukabiliana na yote mabovu aliyoyafanya kwa sababu
hakutumwa na Rais Kikwete.
Tena basi, kama ambavyo amenukuliwa
akisema, asithubutu kufanya makosa akidhani atakuwa na ngao ya ukaribu wake wa
kieneo na Rais Kikwete. Rais Kikwete tunayemfahamu hana ubia na wanaotumia
vibaya madaraka yao.
Tumeshuhudia namna alivyokataa kubariki
uamuzi tata wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wa kuwang’oa
wakurugenzi wawili. Kipande asivurunde akadhani Rais Kikwete atamuacha salama.
Haya tunayoyasema kwa Kipande tunayasema
kwa wengine wote wanaotumia vibaya jina la Rais Kikwete na viongozi wengine
kama ngao kwa dhambi zao. Tunaomba jamii kwa ujumla wake iendelee kutuunga
mkono ili hatimaye tuweze kuiokoa TPA ambayo sasa imegeuzwa shamba la bibi
No comments:
Post a Comment