Kurugenzi ya
Mawasiliano na Uhusiano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
imepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha mmoja wa waandishi
wa habari za picha (mpiga picha) mwandamizi nchini, Maximillian John Ngube
aliyefariki siku ya Ijumaa baada ya kuugua muda mfupi.
Kwa masikitiko makubwa
kurugenzi, kwa niaba ya chama, inatuma salaam za pole kwa familia ya marehemu
Maximilian kwa kuondokewa na baba na mpendwa wao, katika wakati ambao tunaamini
walikuwa bado wakimhitaji sana kama moja ya nguzo za familia.
Kurugenzi pia inatoa
salaamu za pole kwa wafanyakazi wa Mlimani Media House, (inayomiliki Mlimani
Tv, Radio Mlimani na Gazeti la The Hill Observer), ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, ambako
Maximilian alifanya kazi na kutimiza wajibu wake kwa jamii kama mwandishi wa
habari, hadi mauti yalipomkuta.
Salaam hizi za
rambirambi pia zinatolewa kwa waandishi wa habari nchini, kwa kumpoteza
mwandishi mwenzao, mmoja wa wapiga picha wakongwe, katika wakati ambao uhodari
wake na utayari wa kujituma kwa ajili ya ubora wa kazi yake na chombo chake,
hatimaye tasnia nzima ya upashanaji habari, ulikuwa bado ukihitajika kweli
kweli.
Tunajumuika pamoja na
familia, waandishi wa habari nchini na wengine wote waliowahi kufanya kazi
naye, bila kusahau Watanzania wote walioguswa na kifo cha Maxi (kama
alivyojulikana kwa watu wengi), ambao tunajua hata kama hawakuwa wakimjua Maxi
kwa sura, lakini wamenufaika na matunda ya kazi zake nzuri katika vyombo vya
habari mbalimbali nchini alivyowahi kuvifanyia kazi.
Kifo cha Maxi, si
kwamba kimeacha pengo kubwa kwa familia yake na kazini kwake pekee, bali kwa
tasnia nzima ya uandishi wa habari nchini.
Maxi alijulikana sana
miongoni mwa waandishi na ‘sources’ wake na hatimaye jamii nzima, atakumbukwa
zaidi kwa mambo matatu, uhodari (ubora) wa kazi zake, ucheshi na alivyokuwa
mwalimu wa vijana wengi ambao kwa kupitia mikononi mwake, wamekuwa watangazaji
wa habari au wapiga picha wazuri na hodari kama alivyokuwa Maxi, ambao
wamesambaa kwenye vyombo mbalimbali nchini.
Hakuna mtu aliyemjua
Maxi asiujue ucheshi wake! Hakuna mtu aliyewahi kumshuhudia Maxi akiwa kazini,
ambaye asingejua ndani ya muda mfupi kuwa yule aliyekuwa mbele yake,
akihangaika huku na kule, hapa na pale, kutafuta ‘angle’ au ‘shot’ nzuri,
alikuwa ni mwandishi anayeipenda taaluma na kuithamini kazi yake.
Kwa watu waliofanya
kazi na Maxi katika majukumu yake, kama waandishi au vyanzo vya habari au
waliomfahamu kupitia maisha yake ya kawaida, hakuna maneno yatatosha kumalinza
simanzi ya ghafla waliyoipata kwa kuondokewa na ‘mpiganaji’ huyu, ambaye pamoja
na kufa kimwili, sifa na matendo yake katika tasnia ya habari yataendelea
kudumu.
Tunawaombea wote
walioguswa na msiba huu, Mwenyezi Mungu awatie nguvu na kuwapatia moyo wa
subira wakati huu wa majonzi mazito ya kuondokewa na mpendwa, Maxi.
Mwenyezi Mungu amlaze
mahali pema peponi Maxi.
Imetolewa leo
Jumamosi, Mei 24, 2014 na
Tumaini Makene-Ofisa
Habari Mwandamizi
Kny; Mkurugenzi wa Mawasiliano
na Uhusiano- CHADEMA
No comments:
Post a Comment