WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
(PRESS RELEASE)
Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto inalaani vikali tukio la ukatili na udhalilishaji dhidi
ya mtoto Nasra (4) mkazi wa mjini Morogoro ambaye alifichwa chumbani
ilhali amefungiwa ndani ya kasha na mama yake mkubwa kwa muda wa miaka
nne, baada ya mtoto huyo kufiwa na mama yake mzazi.
Kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki
za mtoto. Wizara inasisitiza kwamba mzazi au mlezi yeyote anayekubali
jukumu la kulea mtoto anaowajibu wa kuhakikisha kuwa anampatia mahitaji
yote muhimu ya kumwezesha mtoto kukua hadi kufikia utimilifu wake.
Wizara inakemea vikali kitendo hicho na vingine vingi vya aina hiyo
ambavyo vinaendelea kufanyika katika familia zetu na jamii kwa ujumla.
Wizara inaziomba mamlaka
zinazohusika na udhibiti wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria
ili haki iweze kutendeka na kuwa fundisho kwa wanaoendeleza ukatili
dhidi ya watoto. Jamii inahimizwa kubadilika na kuhakikisha kuwa familia
ambayo ndio kitovu cha jamii panakuwa ni mahala salama; na
kuwahakikishia watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi,
kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Wizara inapongeza Uongozi wa
Manispaa ya Morogoro hasa Afisa Ustawi wa Jamii, Jeshi la Polisi kupitia
Dawati la Jinsia na Watoto na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha
Ndege kwa kufuatilia suala hili kwa karibu. Vile vile, Wizara inapongeza
majirani na vyombo vya habari kwa uzalendo wao mkubwa wa kufichua
ukatili aliofanyiwa mtoto huyu maana taarifa zao zimesaidia kunusuru
uhai na maisha ya mtoto Nasra.
Wizara inamwelekeza Afisa
Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Morogoro awasiliane na Afisa Ustawi wa
Jamii husika kuona uwezekano wa kumkabidhi mtoto Nasra kwenye taasisi
zinazohusika na matunzo ya watoto ili awe kwenye mikono salama, wakati
taratibu za kisheria zikifanyika dhidi ya wanaohusika na ukatili huo.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
23 Mei, 2014
No comments:
Post a Comment