.

NANI ANAJALI KWA UFISADI HUU WA WAKUBWA

Na Karoli Vinsent

         Tanzania ni nchi ya ajabu kwa mwanadamu makini kuweza kuishi. Ni nchi inayoshangaza sana, ingawa raia wake hawaonyeshi kushangazwa na matukio kadhaa yanayotokea. Naizungumzia Tanzania nchi niliyoishi kwa miongo kadhaa tangu nizaliwe. Baada ya nyimbo nyingi za matatizo, dhiki, wizi, rushwa, tabu, magonjwa na kila aina ya shida ambayo mwanadamu wa kawaida anapitia, jawabu kubwa linapatika kwa swali; nani anajali?


              Ndio, nani anajali? Hili ni swali ambalo kila Mtanzania anapaswa kuulizwa. Ni kwa kiasi gani, mwananchi wa kawaida, kiongozi au muhusika yeyote wa nchi hii anajali matatizo ya nchi yetu.Nimejaribu kwa kiasi kikubwa kutazama sura za viongozi wetu, mawaziri, wabunge, Wakurugenzi, Mameneja na kila kiongozi. Sioni anayejali.Wengi wanaongea wasichofikiria kukifanya kwa dhati na nchi imezidi kuoza. Akili zao ziko katika wizi kwa sababu na wananchi wenyewe wala viongozi wengine hawajali.Nchi inatafunwa kila jua linapochomoza na kuzama.

           Hakuna anayejali na kila mtu anaangalia maisha yake. Msukuma mkokoteni haoni ni kwa namna gani anahusika na Waziri mwizi wala Mkurugenzi wa Manispaa mla rushwa. Atajihusisha vipi? Kwa nini atumie muda wake mwingi kujali? 


         Kama watu wanaomzunguka hawajali kula yake kwa nini na yeye awe anajali maisha ya wengine.Siwezi kusema nilifaidi matunda ya utawala wa Mwalimu Nyerere. Sijui mengi yaliyotokea wakati wa Utawala wake, lakini tangu nilipopata akili timamu sijawahi kusikia Rais wa nchi yangu akimfukuza kazi Waziri wake kwa               rushwa wala wizi. Je ni kweli kwamba marais wangu hawawaoni Mawaziri wezi na wala rushwa? Kama wangekuwa watiifu na waadilifu basi nchi yetu ingekuwa mbali. Lakini naamini wanawaona, kikubwa ni kwa vile hawajali kinachotokea.

            Hawajali kwa sababu hawana sababu ya kujali. Kwa kuwa wananchi hawajali basi na wao hawajali kama ambavyo wananchi hawajali. Wanaendelea kutojali na daima tunaendelea kupata vizazi vya Watanzania wasiojali. Kwani tukifungua mikataba ya ajabu ya Madini hatuwaoni walioweka saini hizo? Tunawaona, lakini nani anajali? Nchi inasonga mbele na maisha yanaendelea. Huyu anajaribu kuandika gazetini kwa uchungu na yule anatamka lile katika kipindi cha redio kwa uchungu, lakini nani anajali? Kina mama na watoto wanafungulia michezo ya maigizo ITV na kwingineko. Nani atawalaumu wakati watu makini wenyewe hawajali? Si afadhali naowasijali!Kwani yuko wapi yule Waziri aliyesema yuko tayari kuona wananchi wanakula majani ili ndege ya Rais inunuliwe? Ndege ambayo ni mbovu!. Si amechaguliwa tena kuwa Waziri? Nani anajali kama Rais wa sasa hakujali? Mimi nitajali nini?

        Ni mwananchi gani anajali? Walio wengi wanafanya maaandamano katika mikasa ya kidini au ile ya kumpongeza Rais aliyefutiwa madeni ambayo fedha zake zilitumiwa kununua mashangingi. Kuna anayejali kwenda katika maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya umeme? Kuna anayejali kuandamana baada ya kusikia Nesi amesababisha kichanga kufa sekunde chache baada ya mama mjamzito kujifungua? Hakuna anayejali kwa sababu hata akiandamana kwa uchungu mkubwa,Rais hawezi kumwajibisha Waziri wa Afya!. Ndivyo nchi ilivyo na watu wengi wamekwenda jela baada ya kutoa taarifa njema kwa jeshi la Polisi. Lakini nani anajali kuwepo kwao jela? Ukitoa taarifa kuhusiana na mkubwa fulani anayepokea rushwa, kesho yake Kamanda wa Polisi wa Mkoa anakuonya na kukwambia uachane naye.Kwa nini niendelee kujali kwa watu ambao hawajali?

         Watu wangapi walishikwa na madawa ya kulevya katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam lakini wapo nje kwa madai kwamba uchunguzi unaendelea? Uchunguzi upi wakati madawa yalitolewa tumboni na tukaonyeshwa katika taarifa za habari za Televisheni mbalimbali? Kwa nini niendelee kujali kuwepo nje kwa mtuhumiwa wakati Kamanda wa Polisi wa mkoa haonyeshi kujali? 
           
Yuko wapi dada machachari Mbunge wa kike aliyedai kwamba ana majina ya wauza madawa wa kulevya? Ni kweli kwamba alizungumza jambo jipya katika jamii yetu ya watu wasiojali? Tunao watu wengi wanaouza madawa na kwa bahati wanajulikana, lakini nani anajali? Dada yule ‘alionyesha’ kujali, lakini baada ya hapo nani amejali? Mbona hatujasikia mtu amekwenda ndani kutokana na mdomo wake?Tangu baada ya ‘mauaji’ ya basi ya Buffalo, magari yanazidi kwenda kasi barabarani. Nani anajali? Si mpaka watu wengine wafe ndio tusikie tamko jingine la kinafiki?Kuna meli ngapi mbovu pale Ziwa Victoria na sehemu nyingine zenye vyombo vya usafiri wa majini? Kwa sababu hakuna anayekufa kwa sasa wahusika na wananchi hawajali mpaka litokee janga.

          Ili mradi asubuhi inafika, mchana unapita na jioni inawadia basi hakuna anayejali mpaka litokee janga. Nani anajali?Mchele mbovu unahalalishwa, watu wanatengeza maji ya ‘kufoji’ na kuuza, nani anajali?
Nikienda kusema Polisi wananitazama kwa jicho la chuki lakini tayari nimeshawaachia mianya ya rushwa.

      Keshokutwa nakutana na mkubwa wa Polisi niliyemshtua akiwa pamoja na mkuu wa Kiwanda nilichokishtaki. Wanakula ‘kitimoto’ pamoja na wanacheka vilivyo, nani anajali?Kuna watu wachache walikiweka mikononi Chama cha soka nchini FAT,enzi hizo. Nani alijali? Kama si kuvurugana wenyewe kwa wenyewe wangeweza kuwepo mpaka leo.Ndio, Rais wa nchi alikuwepo, lakini hakuwa na muda wa kujali. Kipaza sauti kilikuwa kinamwambia asijali mambo hayo ila aelekeze macho katika Utandawazi. Ndio, utandawazi ambao unaruhusu tupeleke makontena ya mchanga uliochanganyika na dhahabu nje ya mipaka yetu. Nani anajali?Wachache wanajaribu kujali lakini nani anawasikia?
        
      Wenyewe wanakutana Golden Tulip wakila firigisi na kupeana ruhusa hizo. Mimi na wewe tujali nini wakati hatuna uhakika wa kesho? Tukipata watoto nao wanaingia katika mkumbo huo huo wa kutojali. Kizazi hiki ambacho watoto wengi wamegeukia hisia za kimagharibi ni yupi kati yao anaweza kujali?Wa kiume anakazania kusuka, wa kike anatamani kuvaa kama Beyonce. Hakuna hata mmoja mwenye hisia na nchi. Hawezi kujali kwa sababu hajafundishwa kujali.

              Ukisikiliza maoni ya wengi kuhusiana na kesi ya Justine Kasusura, wengi wanamlaumu kwa nini hakutoweka nje ya nchi. Hakuna anayesikitika kwa kitendo chake cha kuiba fedha. Kwa nini?Watu hawajali alichokifanya. Yeye alifanya hadharani lakini kuna wanaoiba kwa karatasi? Hawa akina ‘Kasusura’ wa mezani nani anawazuia? Nani anawajali? Iko wapi Kampuni ya Richmond? Mbona kimya? Nani anajali? Kwa sasa umeme upo na watu hawajali tena. Wanataka ije ‘Richmond’ nyingine ya Maji au huduma za Afya. Nani anajali?

           Ndio, sijawahi na wala sitaki kupiga kura. Yupo atakayesema napoteza haki yangu ya msingi. Simuoni wa kunijali na hata kama akiamua kunijali basi mfumo hauwezi kumsapoti anijali.Wakati wananchi wengine wakipiga kura mimi naangalia vipindi vya soka katika Televisheni, kwa nini uniambie sijali wakati atakayechaguliwa hatanijali?

           Katika kituo cha wapiga kura chenye wakazi 1000 lakini mshindi ameshinda kwa kura 1200, kwa nini nijali kusumbuka juani huku FFU wakinighasi wakati waliopanga matokeo hawaijali kura yangu? Nijali nini hasa kwa kutompigia kura mtu atakayekwenda bungeni kupitisha sheria ya Takrima? Acha nifuatilie Ligi kuu ya England na utamu wake.

         Soma magazeti yetu ya leo. Watu wameamua kuandika mambo laini ambayo si sehemu ya mapambano yetu.Makala za leo ni zile zile zinazoelezea kwa undani Habari za Theolojia, Ulokole,na mambo mengine. 

Mwananchi asiye na uhakika na machweo ataelewa nini na kupata tumaini jema katika makala hizi? Wanaoziandika hawajali kinachotokea kwa sasa. Kwetu, kiongozi kutajwa anamiliki hiki na kile kwa jina la mwanae, si kashfa. Kwetu, mtoto wa mkubwa au mkubwa mwenyewe kuua si jambo la ajabu sana. Nani anajali? Wao na Kamanda wa Polisi wanakutana Kilimanjaro Kempsky katika dhifa mbalimbali, unajua wanaongea nini? Kwa nini ujitie kimbelembele cha kujali? Ili mradi unapumua, iangalie siku yako ya kesho.Tanzania ya leo imejaa watu wanaozijali familia zao. Nani atawalaumu watu hawa? Kwani viongozi wetu wanawajali kina nani?

        Si wanajali elimu za watoto wao pale Oxford, Havard na kwingineko? Kama unabisha, mbona sasa hivi ndio wanatuongoza? Nani anajali? Tuna uhakika gani kama baadaye wajukuu hawataongoza? Si ndio wanapewa ukamanda wa vijana wakijiandaa kumtawala mwanangu ambaye ni mnyonge wa baadaye? Nani anajali?Sina hasira na mtu. Nina furaha na maisha yangu kwa sababu napata ninachokitaka kwa uhalali. Kama maisha yataendelea kuwa hivi basi nisilaumiwe kwa kutojali. Nina uhakika gani kama wenzangu wanajali? Kilio kama changu kimetamkwa mara ngapi na watu makini? Nani amejali?

         Kelele za mchanga wa dhahabu nani amezijali? Waliongia mikabata mibovu ya madini nani anawajali? Wangekuwa Chini,Japan, Uingereza na kwingineko, wangekuwa wapi watu hawa kama si katika kuta za Gereza? Hapa kwetu nani anajali?Lakini nijali nini zaidi wakati Rais wa nchi aliwahi kuwatamkia watu walioelezea hisia zao kwa Waziri Mkuu wake kuhusu umilione wake wa mashaka, kwamba wana wivu? Kama yeye mtu wa juu kabisa hakujali, nani atajali? Utawala ule ulikumbana na migomo ya wanafunzi, huu nao unakumbana na migomo hiyo hiyo, nani anajali? Kuna njia za kudumu za kumaliza migomo hiyo ambayo nimeisikia tangu utotoni mwangu?

          Huyu anakabiliana nayo leo, akihamishiwa anahama na hisia zake. Yule anakuja na hisia nyingine na wala hajali kutazama alipoishia mwenzake. Leo, kuna watu wengi wanapiga kelele kuhusiana na hatari ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nani anawasikiliza? Mimi naweza kuwa sehemu ya maamuzi hayo? Wanaotoa tahadhari ni watu wasomi. Afadhali ingekuwa kwangu mtu nisiye na elimu,
lakini wanaotoa tahadhari hizi ni watu wanaoheshimika kwa elimu na upeo wao.

            Najua hawasikilizwi lakini nani anajali? Kama wenzao hawajali, nani atanisikiliza mimi nisiye nalolote? Acha waamue nami nitatii kwani waliamua mangapi ya hatari na nimeendelea kutii? SijaliLakini kwa nini nimewang’angania wasiojali wakati hata wenyewe wakifa au kuondoka madarakani hakuna anayewajali? Wako wapi waliojali ambao familia zao zinaishi kama vile baba zao hawakujali? Ndio, familia za akina Edward Sokoine. Nina uhakika watoto wao watajuta kwa kitendo cha baba yao kujali sana wakati wa utawala wake.Ndio, na hata ninapomaliza kuandika makala hii, wengi wataelewa ninachomaanisha. Wakubwa wengi na watu wa kawaida wataisoma na kuielewa. Lakini nani atajali?

              Kwa kutokujali huko, mafisadi ya CCM yanazidi kunawili, ilhali Watanzania wanateseka kwa umasikini wa kutisha na kuteketea mahospitalini mbali na utajili Taifa hili iliokuwa nao. Ni muhimu sana Watanzania tubadilike tujali Taifa letu kwa kutokukubali CCM kuendelea kuongoza kwa kuibia Watanzania, kutengenezea mafisadi mianya ya kurithishana madaraka kwa gharama ya uhai wa Watanzania. Chukua hatua sasa za kivitendo, kwa kuelimisha Watanzania kuwa CCM ndio maadui wa Watanzania, wajiandikishe kupiga kura, wapige kura siku ya uchaguzi, na walinde kura zao hadi viongozi wa CCM watakapoangushwa kwa masilahi ya Watanzania wote

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.