Kamishna wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam SULEMAN KOVA akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam mapema leo |
Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam linakanusha vikali juu ya uvumi unaoendelea
jijini Dar es Salaam kuhusu utekaji nyara wa watoto wadogo wanaosoma shule.
Hivi karibuni umezuka uvumi kutoka kwa watu mbalimbali hasa wazazi ambao uvumi
huu umewafikia kwamba kuna kundi la wahalifu wanaotumia gari aina ya NOAH rangi
nyeusi ambao kazi yao ni kuteka nyara wanafunzi kwa nia ya kutenda uhalifu
ikiwa ni pamoja na kuwachuna ngozi na madhara mengine.
Mpaka sasa Jeshi la
Polisi halina taarifa yoyote ya mtoto kutekwa au kufanyiwa madhara yoyote kwa
mtindo wa utekaji nyara. Pia Jeshi la Polisi limegundua kwamba huu ni uvumi
ambao haujulikani chanzo chake hivyo wananchi wanaombwa kuachana na uvumi huo
na kuupuuza kwani unaleta hofu katika jamii bila sababu za msingi.
Aidha, uvumi huu
umeanza kuleta usumbufu ambapo mnamo tarehe 03/10/2014 saa tatu asubuhi huko
vingunguti mtu mmoja aitwaye PROSPER MAKAME miaka 34, mfanyakazi wa The
Guardian Ltd, mkazi wa Tabata akiwa na mkewe MARYSTELLA MUNIS, Miaka 30,
mfanyabiashara wa vyombo vya nyumbani walifika maeneo ya shule ya msingi Kombo
iliyopo Vingunguti kwa ajili ya kuchukua pesa za vyombo wakiwa na gari aina ya
NOAH yenye namba T252 DAY rangi nyeusi.
Ghafla walikuja watu wanaokadiriwa
kufikia mia moja (100) na kulizingira gari hilo kwa makelele wakidai kuwa ndilo
linalowateka wanafunzi. mtoa taarifa alipoona hali inakuwa tete alipiga simu
Polisi na hatimaye watu hao waliokolewa na Polisi kisha kufikishwa katika kituo
cha Polisi Buguruni wakiwa salama pamoja na gari lao.
Wanahabari mbalimbali wakimsikiliza kwa makini |
Pia mnamo tarehe
13.10.2014 majira ya saa 10:00 hrs huko katika kituo cha polisi Tabata uliibuka
uvumi kuwa gari namba T548 BUN aina ya Noah rangi nyeusi ambayo ni mali ya
askari polisi aitwaye A/INSP ESTAR wa kikosi cha usalama barabarani kituoni
hapo ndani yake kuna vichwa vitano vya watoto wa shule ya msingi Mtambani na
kusababisha wazazi wa watoto wanaosoma shuleni hapo na wananchi wengine
kukusanyika kituoni hapo ili kushuhudia na kuona hivyo vichwa vitano,na ndipo
mkuu wa kituo hicho cha Polisi Tabata aliamuru gari hilo kufunguliwa na
kuwathibitishia wananchi kuwa habari hizo ni za uwongo na uvumi.
Jeshi la Polisi Kanda
Maalum Dar es salaam linasisitiza kuwa uvumi huu wa kuwepo kwa kikundi cha
wahalifu ambao wamekuwa wakiwateka watoto/wanafunzi hao si wa kweli hata kidogo
na hivyo wananchi wanatakiwa kuepukana na taarifa hizo ambazo kwani zinaweza
kusababisha uvunjifu wa amani.
Aidha,uchunguzi wa
kubaini ni nani aliyeeneza uvumi huo ulifanyika na kubainika kuwa uvumi na
habari hizo zimeenezwa na mtu aitwaye GILBERT s/o STANLEY,(32) mhehe,mkulima,na
mkazi wa Tabata ambaye alikamatwa muda mfupi tu baada ya tukio hilo na
alipohojiwa alikiri kweli kueneza habari hizo na yeye aliambiwa na mtu mwingine
ambaye hata hivyo alisema hamkumbuki.
STORY NYINGINE KALI KUTOKA POLISI LEO ZIPO HAPO CHINI
WATANO WAFARIKI, 16 WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA
MOTO BAADA YA LORI LA KUBEBA MAFUTA (PETROLI) KUPINDUKA.
Kamishana wa Polisi
Kanda maalum Dar es Salaam Suleiman H.Kova amethibitisha kutokea kwa vifo vya
watu watano na wengine kumi na sita kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea
juzi mnamo tarehe 13/10/2014 majira ya saa tano usiku huko Charambe round about
Mbagala,baada ya lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 347 BXG mali ya
MOIL TRANSPORTER lililokuwa likisafirisha mafuta kuelekea Kampala Uganda,
kuanguka likiwa na kemikali aina ya petrol lita 38,000 thamani yake inakadiriwa
kuwa dola 36,000.
Watu hao waliofariki ni
1.Masoud s/o Masoud (33) mkazi wa Charambe, 2. Hassan s/o Mohamed (25) mkazi wa
Mbagala Kibangulile, 3.Mohamed s/o Ismail (19) mkazi wa Mbagala Charambe,
4.Ramadhani s/o Halfan (36) mkazi wa Mbagala Charambe na 5.Maulidi s/o Rajabu
mkazi wa Mbagala Charambe.
Majeruhi katika ajali
hiyo ni 1.Hamis s/o Ally (35) mkazi wa mbagala kiburugwa, 2.Rajabu s/o Selemani
(28) mkazi wa Tandika, 3.Idd s/o Said (28), 4.Janney s/o Mathayo (25) mkazi wa
mbagala kizuiani,5.Mathayo s/o Daniel(21) mkazi wa mbagala charambe,6. Askari
E.1028 CPL THOMAS alijeruhiwa na jiwe sehemu ya paji la uso wakati akijaribu
kuzuia vibaka kuchota mafuta kabla ya kulipuka, aidha askari huyo alitibiwa na
kuondoka, na majeruhi wengine 10 wamelazwa katika hospitali ya taifa ya
Muhimbili na hospitali ya Wilaya Temeke wakiendelea na matibabu huku hali zao
zikiwa si za kuridhisha.
Aidha ajali hiyo
ilisababisha pia kuungua kwa nyumba ya kulala wageni iitwayo United mali ya
Deus Kasigwa (42) mfanyabiashara na mkazi wa Mtoni Mtongani,kuteketea kwa
pikipiki saba za madereva wa bodaboda waliogesha karibu na eneo hilo pamoja na
kuteketea kwa maduka yapatayo matano
ambapo vitu vilivyokuwemo kwenye maduka hayo vinakadiriwa kuwa na thamani ya
shilingi 197,000,000/=
JAMBAZI SUGU LAUWAWA NA POLISI KATIKA MAJIBIZANO YA
RISASI LIKIWA NA BASTOLA AINA YA STAR ILIYOFUTWA NAMBA.
Jeshi la Polisi
Kanda maalum ya Dar es salaam kupitia
makachero wa kikosi kazi mkoa wa Kinondoni(Task Force)_mnamo tarehe 14/10/2014
majira ya saa 06:45 hrs huko Chanika (W) Ilala lilifanikiwa kumkamata jambazi
sugu aitwaye Paulo s/o Thomas Milanzi @Chinga,mmakonde,mkristo,hana
kazi,miaka 35,mkazi wa Chanika.
Kabla ya ukamataji jambazi huyo alianza
kuwashambulia askari polisi kwa kufyatua risasi kwa bastola huku akikimbia na
hatimaye askari polisi walijibizana nae na kumjeruhi kwa risasi maeneo ya
mgongoni na baadaye kumkimbiza hospitali ya taifa Muhimbili kwa matibabu na
baadaye madaktari walithibitisha kuwa amefariki.
Aidha jambazi
huyo alikuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu kuhusiana na matukio
mbalimbali ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha jijini Dar es salaam na
mikoa ya jirani.
Baadhi ya matukio aliyowahi kufanya jambazi
huyo ni 1. Tukio la tarehe 29/04/2014 lilitokea huko Airport kwenye taa za
kuongozea magari akiwa na majambazi wenzake ambapo walimuua kwa kumpiga risasi
Ofisa mwandamizi wa Usalama wa taifa SYLIVANUS s/o ADRIAN MZERU na kupora kiasi
kikubwa cha fedha,2.Tukio la mnamo tarehe 21/02/2014 lililotokea maeneo ya
Oysterbay katika barabara ya Haille sellasie karibu na Jackies Bar ambapo
walivunja kioo cha gari aina ya Nissan Patrol iliyokuwa inaendeshwa na
SYLIVANUS s/o ADRIAN MZERU na kupora pesa taslimu na laptop computer na wakati
wanakimbia walimuua kwa kumpiga risasi ubavuni mlinzi wa kampuni ya KK security
aitwaye FRANK s/o SILAYO,3.
Tukio la mnamo tarehe 17/02/2014 lililotokea
Kinondoni studio akiwa na wenzake ambao walishakamatwa wakitumia usafiri wa
pikipiki walimvamia mfanyabiashara LUKAS s/o MONGI ambapo walifyatua risasi
hewani kwa silaha walizokuwa nazo ambazo ni SMG na Bastola mbili kisha kumpora
kiasi cha shilling 20,000,000/=.
KUPATIKANA
KWA BHANGI GUNIA MBILI.
Jeshi la Polisi
Kanda maalum Dar es Salaam mnamo tarehe 10/10/2014 majira ya saa nane mchana
huko maeneo ya Kingugi Mbagala lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa aitwaye TREVER
s/o LUCAS (18) mkazi wa Kingugi akiwa na bhangi gunia mbili, Aidha mtuhumiwa
huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na pindi upelelezi
utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
POLISI WAKUSANYA MILIONI 336,450,000/=
KWA MAKOSA YA USALAMA BARABARANI
Jeshi la polisi kanda maalum kupitia kikosi
chake cha usalama barabarani limefanikiwa kukusanya kiasi cha T.Shs.
336,450,000.00 (shilingi milioni mia tatu thelathini na sita na laki nne na
hamsini elfu) kama tozo kwa makosa ya usalama mbalimbali
Kama ifuatavyo;
1.Idadi ya magari yaliyokamatwa
3,097
2.idadi ya pikipiki zilizokamatwa
1,463
3.daladala zilizokamatwa 4,184
4.magari mengine binafsi na
malori 2,471
5.jumla ya makosa yaliyokamatwa 11,215
Fedha za tozo zilizopatikana Tsh 336,450,000/=
Aidha madereva wa vyombo vya
usafiri wanatakiwa kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani ili
kuepukana na faini hizo ili waweze kujiendeleza katika familia zao na jamii kwa
ujumla.
KUIMARISHA
ULINZI MECHI YA YANGA NA SIMBA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum limejipanga vyema
kuimarisha ulinzi wakati wa mechi ya Simba na Yanga itakayochezwa tarehe
18/10/2014 kama ifuatavyo:-
1. Mashabiki
wanatakiwa kukaa katika sehemu zao kadiri ya tiketi walizokata
2. Ni
marufuku kwa mashabiki kuingia na silaha aina yoyote kwa mfano chupa za maji
3. Mageti
rasmi pekee yatumike kuingia uwanjani
4. CCTV
Camera zitatumika kuangalia na kutunza kumbukumbu kwa matukio yoyote
yatakayojitokeza kabla, wakati na baada ya mchezo.
5. Barabara
zote zinazopita uwanja wa Taifa zitafungwa kwa muda mpaka yatakapotolewa
maelekezo mengine.
Vitengo mbali mbali vya Polisi vitatumika
kuhakikisha kwamba Amani na Utulivu vinatawala wakati wote wa mchezo huo. Mashabiki wanatakiwa kuwa watulivu wakati
wote wa mchezo na waheshimu maamuzi ya mwamuzi na utii wa sheria bila shuruti.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment