Monday, October 6, 2014

VETA YASAIDIA TANESCO KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAFUNZO YA UENDESHAJI


Viongozi wa Shirika la Umeme nchini, TANESCO wamepata matumaini yankupunguza gharama za mafunzo na uendeshaji wa shirika baada ya kubaini nkuwa baadhi ya mafunzo waliyokuwa wakiyapata nje ya nchi yanaweza kutolewa katika katika Taasisi ya TEHAMA ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundin Stadi VETA-Kipawa jijini Dar es Salaam.

     
         Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Naibu Mkurugenzi wa Uzalishaji Umeme wa Maji, Mhandisi Anthony Mbushi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo juu ya Uendeshaji wa Mitambo kwa Njia ya Kompyuta (Programmable Logic Controller-PLC) kwa wahandisi na mafundi mchundo kutoka TANESCO, katika Taasisi ya TEHAMA ya VETA, Kipawa jijini Dar es Salaam.


          Akizungumza katika halfa hiyo, Mbushi alisema kuwa kwa kipindi kirefu,TANESCO imekuwa ikitumia gharama nyingi kupeleka Mafundi Mchundo na Wahandisi katika nchi za Ujerumani na Norway ili kujifunza mafunzo hayo kabla ya kubaini kuwa VETA inaweza kuyatoa, tena kwa ufanisi mkubwa.


       “Na tukienda huko, tulikuwa hatujifunzi kwa undani, maana mafunzo hayo yalikuwa yakitolewa na wakandarasi wa nje ambao walikuwa wakifanya kazi za shirika, kwa hivyo hawakupenda kutufundisha kwa undani ili waendelee kuhodhi kazi za kuhudumia shirika,” alisema.

     Alisema kuwa baada ya kubaini kuwa VETA ni mahali pekee nchini ambako mafunzo hayo yanaweza kupatikana, TANESCO imeamua kutumia fursa hiyo kwa kupeleka wataalam wake kujifunza kwa awamu.

        Alisema kuwa awamu ya kwanza ambayo imedhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Norway-NORAD imewahusisha wataalam 14, kati yao watatu (3) ni wahandisi na 11 ni mafundi mchundo.

        Naye Mkuu wa Taasis ya TEHAMA ya VETA-Kipawa, Lucius Luteganya alisema kuwa kozi ya PLC ina mahitaji makubwa, hasa viwandani na kwamba VETA inao\ uwezo wa kusaidia katika kufundisha wataalam kutoka katika makampuni na taasisi mbalimbali.

        Katika risala yao, wahitimu walieleza kuwa, mafunzo hayo yamewajengea uwezo mzuri ambao utawasaidia kurekebisha hitilafu mbalimbali zinazojitokeza kwenye mifumo ya umeme wa TANESCO.

       Waliahidi kutoa zawadi ya utaalam walioupata kutoka VETA kwa kufunga mtambo unaojiendesha kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya umeme (Power Control Automation System) katika jengo la TANESCO Makao Makuu, ili kupunguza matumizi ya umeme yasiyo ya lazima.

MWISHO

No comments: