Tuesday, June 16, 2015

MIKOA YA SHINYANGA NA MWANZA YAENDELEA NA UBABE MBIO ZA BAISKELI.

Mmoja wa washiriki wa mbio hizo akinywa maji wakati wa mashindano hayo.

Mshindi wa mbio za Acacia Tufanikiwe Pamoja Lake Zone Cycle Challenge, Masunga Duba aliyeinua mikono akishangilia mara baada ya kumaliza mbio hizo akiwa mbele ya wenzake. Mshindi huyo anatoka mkoa wa Shinyanga.

Makamu wa rais wa Kampuni ya Uchimbaji wa dhahabu ya Acacia, Deo Mwanyika (wa kwanza kushoto) akifurahia jambo na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni ya Acacia, Mishel Ash, (wa pili kutoka kushoto) ambaye pia ni kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu.

Washindi wa mbio za wanawake (kilometa 80). Aliyesimama katikati ni Martha antony ambaye ndio aliibuka mshindi wa kwanza, akifuatiwa na Laulensia Luzuba, (mwenye mtoto) aliyekuwa mshindi wa pili na Veronica Saimon (wa kwanza kushoto) aliyejinyakulia nafasi ya Tatu.
 

Washiriki wa mbio za Acacia tufanikiwe pamoja lake zone cycle challenge wakimenyana vikali wakati wa mashindano hayo.
 
Afisa mkuu wa uendeshaji wa kampuni ya Acacia Mishel Ash akimvisha medali mshindi wa mbio hizo Martha Antony wakati wa Hafla ya Kutoa zawadi kwa washindi.

Washiriki wa mbio za baiskeli zijulikanazo kama “Acacia Tufanikiwe Pamoja Lake Zone Cycle Challenge” kutoka mikoa ya Shinyanga na Mwanza wameendelea kuudhihirisha umma wa wakazi wa kanda ya ziwa na watanzania kwa ujumla kuwa mpaka sasa hawana mpinzani baada ya washiriki wa mbio hizo kuibuka kidedea katika fainali za kumtafuta mshindi wa kanda hiyo.

Washiriki wa mikoa hii miwili wamejinyakulia nafasi zote za juu na hivyo kuwashinda wenzao wa mikoa mingine ya Kanda ya ziwa ikiwemo Kagera, Mara, Geita na Simiyu.

Katika mbio za wanaume za umbali wa kilometa 156.6 kutoka Kahama mpaka Tinde na kisha Kurejea Kahama, mshindi wa mwaka jana Masunga Duba (Mwanza) aliibuka tena kidedea huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Lupilya Hamis(Shinyanga) na nafasi ya tatu ikimuendea Kulwa Tuki(Shinyanga), washindi hawa wamejinyakulia kitita cha pesa taslimu Sh1,500.000/- kwa mshindi wa kwanza, Sh1,200.000/= mshindi wa pili na Sh800,000/= kwa mshindi wa tatu.

Kwa upande wa mbio za wanawake za umbali wa kilometa 80, kutoka Kahama mpaka Mwakata Kisha kurejea Kahama, timu ya mkoa wa Mwanza imedhihirisha kuwa wao bado ni mabingwa kwa kuibuka tena washindi wa mbio hizo, huku mshindi wa mbio za Mwaka jana Martha Antony, akiibuka mshindi wa kwanza akifuatiwa na Laulensia Luziba na nafasi ya tatu ikienda kwa Veronica Simon. Washindi hao wamepata zawadi ya pesa taslimu Sh1,200.000/= kwa mshindi wa kwanza, Sh800,000/= mshindi wa pili na Sh600,000/= mshindi wa tatu.

Mbio hizo ambazo zimeandaliwa na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) kwa udhamini wa kampuni ya uchimbaji wa Madini ya Acacia, inayomiliki migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, yote ikiwa mikoa ya kanda ya ziwa, kupitia mpango wake wa Tufanikiwe Pamoja ikiwa ni mara ya pili sasa ambapo mashindano ya mwaka huu yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika.

Akizungumza na washiriki wa mashindano hayo Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpyesa, ambaye alikua mgeni rasmi wa fainali hizi, amesema ana imani  kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji ambavyo vitauletea sifa mkoa wa Shinyanga, Kanda ya ziwa na hata taifa kwa ujumla kwani baiskeli kwa maeneo hayo ndiyo jadi yao.

Awali akimkaribisha Mkuu wa wilaya kuzungumza na washiriki hao, Makamu wa Rais wa Acacia Deo Mwanyika amesema kampuni ya Acacia imekuwa ikifanya shughuli za uchimbaji unaojali na ndio maana iliona vyema kuweka udhamini wake pia katika mchezo wa baiskeli, “toka tuanze huu sasa ni mwaka wa pili na tunayaona mafanikio makubwa kwani hata maeneo ambapo mchezo huu ulikuwa hauchezwi sasa unachezwa, hali ambayo imeongeza hamasa na idadi ya washiriki.”

Aidha Makamu wa Rais huyo wa Acacia amesema mipango ya kampuni kwa sasa ni kuona pia inashiriki katika kuendeleza michezo mingine ikiwemo na soka.

No comments: