Thursday, June 11, 2015

POLISI DAR YAFANYA MSAKO MKALI--HAYA NDIYO MATOKEO YAKE


MAFANIKIO YA OPARESHENI YA KUPAMBANA NA MAJAMBAZI JIJINI DAR ES SALAAM KAMA IFUATAVYO.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na oparesheni kamambe ya kuwasaka na kuwakamata majambazi wa kutumia silaha pamoja na uhalifu mwingine ili kuhakikisha wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanaishi na kufanya shughuli zao za kila siku bila hofu ya uhalifu. Katika oparesheni hiyo, Jeshi limepata mafanikio yafuatayo:


KUKAMATWA SILAHA  AINA YA AK.47 NA RISASI 13
Tarehe 09/06/2015 saa 08:45hrs asubuhi maeneo ya Yombo Relini (W) kipolisi Buguruni (M) wa Kipolisi Ilala polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kukamata silaha aina ya AK47 yenye namba M73B1-130887 ikiwa na magazine yenye risasi 13.

Mafanikio haya yalipatikana baada ya majambazi watatu kumvamia mtu mmoja DHARAMPAL S/O NARALADE, Miaka 32, Mhasibu wa Kampuni ya Mohamed Enterprises mara alipotoka getini katika ghala la kampuni hiyo lililopo Kiwalani Bombom na kisha kumpora begi dogo ndani yake kulikuwa na kompyuta mpakato (laptop).

Baada ya uporaji wananchi walitoa taarifa polisi. Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliyafuatilia majambazi hayo yaliyokuwa na pikipiki mbili zenye namba MC467 AKR Boxer nyekundu na MC274 ASS Boxer nyeusi hadi maeneo ya Kiwalani relini ambako walitelekeza pikipiki hizo. Wananchi wenye hasira kali waliweza kumshambulia jambazi aliyekuwa na silaha kwa mawe na polisi waliweza kuwazuia lakini kwa bahati mbaya majeraha aliyokuwa ameyapata yalisababisha kifo chake.

Majambazi wengine walikimbia kabla hawajakamatwa. Pikipiki zinashikiliwa kituo cha Polisi Buguruni kwa uchunguzi na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Temeke.


KUKAMATWA KWA BASTOLA NA RISASI ZAKE SITA
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata bunduki nyingine aina ya BASTOLA yenye namba za usajili TZCAR 91456 ikiwa na magazine yenye risasi sita ndani yake.

Tukio hili lilitokea tarehe 08/06/2015 majira ya saa nane mchana maeneo ya Tabata Ubaya (W) kipolisi Buguruni (M) Ilala Polisi waliweka mtego kwa lengo la kukamata kundi la vijana baada ya kupokea taarifa kuwa kundi hilo linapanga kwenda kufanya tukio ka uhalifu.
Baada ya askari kanzu kuweka mtego ili kuwanasa vijana hao walistuka na kukikimbi ambapo walidondosha silaha tajwa hapo juu. Uchunguzi  unaendelea ili kujua mmiliki halali wa silaha hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watu hao.

KUKAMATWA KWA POMBE YA MOSHI (GONGO) NA BHANGI JIJINI DAR ES SALAAM
Kumekuwa na ongezeko la ukamataji wa wauzaji na watumiaji ya bhangi na pombe haramu ya moshi (gongo) katika jiji la Dar es Salaam ambapo vinaathiri maisha ya vijana wengi.
Kwa mfano kwa tarehe 08/06/2015 peke yake walikamatwa watuhumiwa 161 kwa makosa ya kuvuta bangi, kunywa gongo na kuuza vitu hizi.

Aidha, kwa tarehe hiyo hiyo zilikamatwa jumla ya lita 131 za gongo, Puli 70 za bhangi, misokoto ya bhangi 205 na kete 395 za bhangi.

Nawashauri wauzaji, watumiaji, na jamii kwa ujumla kutafuta shughuli nyingine mbadala za kujiingizia kipato kuliko kufanya biashara ya kuuza gongo na bhangi ambazo ni kinyume cha sheria za nchi. Nawashauri wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi mazuri kwa vijana ili kuwa na kizazi thabiti kwa maendeleo ya taifa la Tanzania.


S. N. SIRRO
NAIBU KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

No comments: