Friday, June 19, 2015

STORY KUTOKA DRFA MCHANA HUU


DAR ES SALAAM YAWA MABINGWA MICHUANO YA UMISETA TAIFA.

Michuano ya UMISETA ngazi ya taifa imemalizika leo asubuhi huko jijini Mwanza kwa mchezo wa fainali kati ya Dar es salaam dhidi ya Nyanda za juu Kusini wavulana, huku fainali nyingine kwa upande wa wasichana ikipigwa jana kati ya Dar es salaam dhidi ya Kanda ya Mashariki.
Katika fainali ya jana wasichana, Dar es salaam wametawazwa kuwa mabingwa  baada ya kuwatandika bila huruma Kanda ya Mashariki kwa mabao 7-1,kwenye mchezo uliokuwa na msisimko mkubwa kwa Dar es salaam kuonesha uwezo mkubwa wa kusakata kandanda.
Dar es salaama ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuisukumiza nje Kanda ya Ziwa mabao 4-1,huku Kanda ya Mashariki ikifanikiwa kutinga katika hatua ya fainali baada ya kuifunga Kanda ya Kaskazini kwa mabao 3-1.
Kwa upande wa fainali ya wavulana leo asubuhi,Nyanda za Juu Kusini wametawazwa mabingwa baada ya kuifunga Dar es salaam bao 1-0,bao ambalo ni la kujifungwa baada ya mabeki wa Dar kujichanganya katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.
Nyanda za Juu Kusini walifanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuifunga Kanda ya Ziwa kwa mabao 3-0,huku Dar es salaam wakitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Zanzibar ambao ndio walikuwa mabingwa wa tetezi kwa mabao 4-3.
Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA chini ya mwenyekiti wake Almas Kasongo,kimeelezwa kufurahishwa kwake na mafanikio yaliyooneshwa na vikosi hivyo vilivyo katika himaya yake (Dar es salaam),na kuviomba vilabu vya ligi mbalimbali kujitokeza kuangalia mashindano ya vijana ili kupata wachezaji wa baadaye kwenye vilabu vyao.
 
LIGI YA WANAWAKE DAR YASUBIRI RATIBA YA TWIGA STARZ.
Ligi ya wanawake mkoa wa Dar es salaam iliyomaliza mzunguko wake wa kwanza,ipo katika maandalizi ya kuanza mzunguko wa pili na wa mwisho kumpata bingwa wa ligi hiyo.
Kamati ya mashindano ya DRFA,imesema kinachosubiriwa kwa sasa ni ratiba ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars,ambao wapo kambini kujiandaa na michuano ya afrika (All African Games) huko Congo Brazavile,mwezi Septemba mwaka huu.
Mpaka sasa kikosi cha Mburahati Queens ndicho kinachoshikilia usukuni wa ligi kwa kuwa na pointi 18,nafasi ya pili inashikiliwa na Evergreen Queens wenye pointi 12,sawa na JKT Queens wenye pointi 12 katika nafasi ya tatu wakitofautiana magoli.

Mwisho.

No comments: