Thursday, August 20, 2015

Huduma ya Tigopesa na WorldRemit wamerahisisha uhamishaji wa fedha kimataifa kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi

 Huduma ya kifedha kwa kutumia njia ya simu ya mkononi ya Tigo ijulikayo kama Tigo Pesa inashirikiana na kampuni ya Worldremit ya Uingereza inayofanya huduma za kuhamisha fedha kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha watanzania waishio nje ya nchi kutuma fedha moja kwa moja kuja kwa ndugu, jamaa na marafiki waishio Tanzania kwa kupitia simu zao za smartphone, tablets na tarakilishi.

Akitangaza wakati wa uzinduzi huo leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa huduma ya kifedha wa simu za mkononi za Tigo Ruan Swanepoel alisema, “huduma hii imekuja na tuzo ya iPad kwa mtu atakayekuwa akipokea kiasi kikubwa cha fedha kwa wiki. Tigo itakuwa ikitoa jumla ya iPad mbili, moja kila baada ya  wiki kuanzia leo,” Ruan alisema.
Tigo Pesa sasa imekuwa ndiyo njia ya kawaida kupokea fedha kutoka nchi za nje kuja Tanzania kwa wateja wa WorldRemit, imekuwa ni zaidi ya kuchukua fedha taslimu,kuongeza muda wa maongezi na kuhamisha fedha kwenda akaunti ya benki.
Ruan alisema kuwa, “Kushirikiana kufanya kazi na WorldRemit ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuiunganisha kikamilifu huduma ya Tigo Pesa kwa mfumo wa malipo ya kimataifa. Dira yetu ni kuwafanya wateja wa Tigo Pesa kufurahia kufanya uhamisho wa fedha usiokuwa na kikomo kitaifa na kimataifa kupitia simu zao. 

Huduma ya WorldRemit sio kwamba hutoa tu ongezeko la kasi ya kuhamisha fedha bali pia hutoa viwango bora ikilinganishwa na huduma nyingine za kuhamisha fedha.”
Kuna wahamiaji wapatao 250,000 kutoka Tanzania wanaoishi nje ya Afrika. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za benki ya dunia zinanonyesha kuwa Uingereza,Marekani na Canada zina idadi kubwa ya watanzania wanaoishi huko.

Benki ya Dunia pia imeidhihirishiaTanzania kuwa ni muhimu kama soko la kupokea katika shughuli za ubadilishanaji wa fedha. Kwa mwaka 2014 Tanzania ilipokea jumla ya dola za kimarekani milioni 64 kutoka kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni. Nchi ambazo zilituma fedha nyingi kuja Tanzania ni pamoja na Kenya, Uingereza, Uganda, Canada, Marekani, Australia na Afrika Kusini.
Jeff Pietras, Makamu wa Rais wa maendeleo ya bidhaa za kimataifa katika kampuni ya WorldRemit alisema, “WorldRemit inabadilisha ulimwengu uliochoshwa na uhamisho wa fedha kupitia huduma zetu za kimitandao na simu tu. Watu kote duniani wanaweza kutuma fedha mara moja kupitia akaunti zao za Tigo Pesa kwa kubonyeza mara chache tu kwenye simu zao za smartphone na kufurahia urahisi na uwazi wa bei.”
WorldRemit ni huduma inayoongoza kwenye uhamisho wa fedha mtandaoni kwenda kwenye huduma ya kifedha ya simu za mkononi, ambayo sasa ni njia inayopendwa kwa ajili ya kupokea fedha katika nchi nyingi. Uhamishaji wa fedha kwenda huduma ya fedha za simu za mkononi umekua kwa zaidi ya asilimia 200 barani Afrika mwaka uliopita, na kuwakilisha zaidi ya asilimia 30 ya uhamisho wote wa WorldRemit ambayo asili yake ni Ulaya na Marekani.
Ili kuweza kutuma fedha moja kwa moja kwa wanafamilia au marafiki zao nchini Tanzania kwa kutumia akaunti za Tigo Pesa, mtu anayeishi nchi za nje anapaswa kutembelea tovuti yahttps://www.worldremit.com/en/tanzania/tigo-mobile-wallet - au kupakua kiunga cha WorldRemit kwenye OS au simu za android .

No comments: