Tuesday, August 18, 2015

STARS KUONDOKA NCHINI JUMAMOSI


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajiwa kuondoka nchini siku ya jumamosi usiku kuelekea Muscat Oman, kucheza mchezo wa kirafiki kabla ya kuunganisha kuelekea Istambul Uturuki kwa kambi ya wiki moja.
Taifa Stars imepata mwaliko wa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Oman tarehe 24 Agosti, 2015 usiku, ambapo baada ya mchezo huo timu itasafiri kuelekea nchini Uturuki katika jiji la Istambul.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Oman (OFA) liliomba kucheza mchezo wa kirafiki na Taifa Star kabla ya kuwavaa Turkemebistan katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia Septemba 03, 2015 kwa bara la Asia, ambapo kocha wake mkuu Mfaransa Paul Leguen aliomba kucheza na vijana wa Charles Mkwasa kujiandaa na mechi hiyo.
Mara baada ya mchezo huo Taifa Stars itaelekea Istambul katika mji wa Kocael hoteli ya Kartepe kwa kambi ya wiki moja, ikiwa nchini Uturuki Stars inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki kabla ya kurejea nchini kucheza na Nigeria Septemba 05, 2015 mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa anatarajiwa kutoa orodha ya kikosi chake cha wachezaji 22 mwishono mwa wiki watakaosafiri kuelekea nchini Uturuki kwa kambi ya hiyo ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria.
Mshambuliaji Adi Yussuf anayechezea klabu ya Mansfield Towny ya Uingereza alitarajiwa kujiunga na timu nchini Uturuki, lakini kutokana na majeruhi aliyoyapata hivi karibuni katika michezo ya ligi, uongozi wa Mansfield umeomba mchezaji huyo kutojiunga na timu ya Taifa kwa ajili ya kupata mataibabu zaidi.
Adi aliumia wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Nottingham Forest ambapo kwa sasa anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa klabu hiyo, na pindi atapokuwa fit atapata nafasi ya kujumuika na kuitumika timu ya Taifa ya Tanzania.


No comments: