TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
Ofisi ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, imepata msiba wa
kuondokewa na mmoja wa viongozi wake Estomih
Jonas Mallah (Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Raslimali Taifa) aliyefariki usiku wa kuamkia Oktoba 9 mwaka huu
katika Hospitali ya KCMC mkoani
Kilimanjarao alipokuwa akipatiwa
matibabu.
Kiongozi wa Chama Ndugu
Zitto Zuberi Kabwe anatoa pole kwa
familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama kwa ujumla kwa kuondokewa na kiongozi
mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na aliyekuwa na mapenzi mema na nchi yake.
Amemuelezea Marehemu Mallah
kuwa mbali na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Raslimali Taifa pia alikuwa
mgombea Ubunge wa jimbo la Arusha
mjini kwa tiketi ya Chama cha
ACT-Wazalendo, Mwenyekiti wa kwanza wa Ngome ya wazee Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa.
Kutokana na Msiba huo
Kamati ya Uongozi Taifa, imeagiza
kusimama kwa kampeni za ACT-Wazalendo kwa muda wa siku tatu kuanzia leo
tarehe 09 Oktoba hadi Jumapili tarehe 11 Oktoba 2015. Aidha bendera za chama kwa
nchi nzima zitapepea nusu Mlingoti kwa siku tano kuanzia leo Oktoba 9 – 13,
2015.
Akimuelezea Marehemu Mallah,Zitto, alisema “Nilimtambua
Mzee Estomih Mallah kwa misimamo yake ya kupigania usawa na amani tokea akiwa
katika CHADEMA na hakuogopa kupoteza nafasi ya udiwani aliyokuwa akiishikilia
kwa sababu ya kukataa kuyumbishwa”
Amesema Mallah amefariki akiwa anapigania
ukombozi wa watu wa jimbo la Arusha mjini na kwamba ACT-Wazalendo itamuenzi kwa kukemea yale maovu yote aliyoanza kukemea
na kuendeleza mema yote aliyoyaacha.
“ACT-Wazalendo itaendelea kumkumbuka daima kwa busara zake na
uongozi wake uliotukuka, alijitoa kulitumikia taifa bila ubaguzi wala upendeleo
wowote, hivyo Chama kitamuenzi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni,
Taratibu na Miongozo mbalimbali aliyoshiriki kuiasisi wakati wa uhai wake”
Oktoba 6 mwaka huu, Mzee Mallah alishindwa kupanda jukwaani katika
mkutano wa kampeni za mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, katika eneo la
Ngaramtoni baada ya kujihisi kizunguzungu na kichwa kumuuma.
Baada ya hali hiyo alipelekwa katika hospitali ya St.
Thomas alipopata mapumziko hadi jana Oktoba 8 alipohamishiwa hospitali ya KCMC.
Mzee Mallah alifariki dunia wakati madaktari na
wauguzi wakiendelea kumpatia huduma. Taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani
kwa marehemu.
Bwana ametoa, Bwana ametwaa, Jina la Bwana
lihimidiwe.
Samson
Mwigamba,
KATIBU MKUU.
No comments:
Post a Comment