Thursday, November 19, 2015

KOCHA MKWASA AWASHUKURU WATANZANIA


Kocha Mkuu wa timuya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Charles Boniface Mkwasa amewashukuru watanzania kwa kuwapa sapoti katika michezo miwili ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, Mkwasa amesema pamoja na kupoteza nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya makundi kuwania kufuzu kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018, anawashukuru watanzania wote kwa ujumla kwa sapoti waliyowapatia.

“Tumepotezea mchezo wa mwisho dhidi ya Algeria, wenzetu walituzidi kiufundi, uwezo wa wachezaji binafsi ulikua chachu ya kuweza kuibuka na ushindi nyumbani kwzo, lakini bado watanzania waishio Algeria na washabiki waliokuja uwanjani walitusapoti katika mchezo huo” alisema Mkwasa.
“Tupo katika kipindi cha kujenga timu, tuna vijana wengi wanaochipukia, hivyo wanahitaji muda wa kucheza zaidi na kupata uzoefu, tuendelee kuwapa sapoti vijana hawa kwa ajili ya kujenga kikosi bora cha baadae” ameongeza Mkwasa.
Mkwasa amewaomba watanzania kuendelea kuwasapoti vijana, pamoja na matokeo mabaya dhidi ya Algeria, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri katika michezo inayofuata ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.
Naye nahodha msaidizi wa Taifa Stars, John Bocco ameishukuru TFF kwa kuwapatia huduma bora za maandalizi na wakati wa michezo yao yote, amewashukru watanzania na vyombo vya habari kwa kuwapa sapoti na kuwaomba kuendelea kuwaunga mkono pindi wanapokua na majukumu ya kuiwakilisha nchi katika michuano mbalimbali.
“Matokeo ya juzi (dhidi ya Algeria) sisi wachezaji yametusikitisha, tulikua na malengo na mtazamo tofauti wa kupata ushindi, lakini katika mpira kuna matokeo matatu, tumepoteza mchezo huo kikubwa ni kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo na watanzania muendelea kutusapoti timu ya Taifa kama ambavyo mmekua mkifanya kwa sasa” alisema Bocco.
Stars imerejea leo alfajiri ikitokea nchini Algeria ilipokua na mchezo wa marudiano dhidi ya Algeria, Jumanne katika uwanja wa Mustapher Tchaker mjin Bilda ambapo ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 7 -0.


No comments: