Thursday, April 21, 2016

MHANDISI MANISPAA YA ILALA JIJINI DAR ES SALAAM NA WASAIDIZI WAKE WATUMBULIWA MAJIPU

 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, akizungumza na wanahabari kuhusu kumvua madaraka Mhandisi wa Manispaa hiyo kwa kufanyakazi chini ya kiwango pamoja na wasaidiziwake wawili.
 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, akizungumza na wanahabari kuhusu kumvua madaraka Mhandisi wa Manispaa hiyo, Japhery Bwigane na wasaidizi wake wawili kwa tuhuma za kusimamia ujenzi wa barabara za manispaa hiyo kwa kujengwa chini ya kiwango . Kulia ni Msaidizi wa Meya, Semmy Mbegha.
Na Dotto Mwaibale

MANISPAA ya Ilala jijini Dar es Salaam imemvua madaraka Mkuu wa Idara ya ujenzi, Mhandisi Japhery Bwigane na wasaidizi wake wawili kwa tuhuma za kusimamia ujenzi wa barabara za manispaa hiyo kwa kujengwa chini ya kiwango.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam wakati akitoa taarifa hiyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko aliwataja maofisa wengine wa idara hiyo waliosimamishwa kuwa ni Siajari Mahili na Daniel Kirigiti ambao wamehamishwa idara hiyo ili kupisha uchunguzi unaoendelea.

Kuyeko alisema  kikao cha Baraza la Madiwani kimefikia uamuzi huo baada ya manispaa kujiridhisha kuwa maofisa hao wamechangia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa barabara mbovu ndani ya manispaa hiyo.

Alisema baada ya kuingia madarakani kwa miezi mitatu walijaribu kutafuta kero ndani ya manispaa ya Ilala ambapo walibaini idara ya ujenzi ina malalamiko mengi kutoka kwa madiwani wa kata mbalimbali kwa sababu ya kusimamia ujenzi wa barabara chini ya kiwango na hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa na maofisa hao.

Alisema madiwani hao walimlalamikia Mhandisi Bwigane kuwa amekuwa akikaidi wito wao wa kujadili ujenzi wa barabara mbovu pindi zinapobainika jambo ambalo limesababisha manispaa hiyo kuwa na barabara nyingi mbovu.

Jitihada za gazeti hili za kumtafuta Mhandisi Bwigane ili kuzungumzia kusimamishwa kwake kazi hazikuzaa matunda baada ya kupigiwa simu yake na wakati wote kuwa imefungwa.


No comments: