TAMKO KUTOKA LHRC--SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI NA HALI YA UHURU WA VYOMBO HIVYO HAPA NCHINI


Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni siku ambayo huadhimishwa tarehe 3 Mei kila mwaka. Kwa mwaka huu siku hii itaadhimishwa kwa mara ya 19 tangu ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998, ikiwa na kauli mbiu ya “Uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa haki za binadamu.” Siku hii iliwekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama siku ya uhuru wa vyombo vya habari; na lengo lake ni kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na kuzikumbusha serikali kuhusu wajibu wao wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza, ambao unajumuisha uhuru wa kupata taarifa, kama unavyobainishwa katika Ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948.  
Siku hii pia inalenga kuwakumbuka wanahabari waliopoteza maisha katika utekelezaji wa kazi zao na kushinikiza mataifa kutengeneza sheria rafiki ambazo zitaviwezesha vyombo vya habari kutafuta na kutoa taarifa kwa uhuru.

Uhuru wa kujieleza pia unapatikana katika mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia na kuahidi kuitekeleza, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kijamii na Kisiasa wa mwaka 1966 na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981. Haki ya uhuru wa kujieleza pia inapatikana katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
 Ibara hii inasema kila mtu yuko huru  kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,  kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa  mawasiliano yake kutoingiliwa kati” kulingana na sheria zilizopo.
Kwa mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanabebwa na kauli mbiu “Kupata taarifa ni haki yako ya msingi: Idai.” Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu kinaungana na vyombo vya habari na wadau wengine wa habari katika kuadhimisha siku hii muhimu.Pamoja na uhuru wa vyombo vya habari kuwepo kikatiba katika Ibara ya 18 na kulindwa na mikataba ya kimataifa, vyombo hivi vimekuwa havifanyi kazi zake kwa uhuru hapa Tanzania. Tumeshuhudia matukio mbalimbali ambayo yanakikuka uhuru wa vyombo vya habari katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo kutishiwa ama kufungiwa kwa vyombo vya habari, wanahabari kushambuliwa wakiwa wanatekeleza majukumu yao, kuendelea kuwepo na kutumiwa kwa sheria mbalimbali kandamizi zinazominya uhuru wa vyombo vya habari, na kutungwa kwa sheria mpya kandamizi kama sheria ya makosa ya Kimatandao.  Taarifa ya Haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2015 inaonyesha kwamba uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania umeendelea kuminywa na kusababisha wananchi kukosa haki yao ya msingi ya kupata taarifa mbalimbali. Kubwa ni kutungwa kwa sheria mbili ambazo zinakandamiza na kunyima haki ya uhuru wa kujieleza, kutafuta na kupata habari. Sheria hizi ni Sheria ya Mtandao na Sheria ya Takwimu.
Sheria ya Mtandao inaminya kwa kiasi kikubwa haki ya kupata na kusambaza habari na haki ya faragha. Sheria hii ina vifungu mbalimbali ambavyo vinatoa makosa ya jinai kwa kubadilishana taarifa mbalimbali na kuwapa askari polisi nguvu kubwa ya kukagua na kukamata vifaa vya kielekroniki pale ambapo wanahisi vimetumika kufanya kosa la mtandao au vina ushahidi. Vifungu ambavyo vinaminya haki ya kupata habari na haki ya faragha ni pamona na vifungu vya 7,8,14, 16, 31,32,37,41 na 45. Kwa mfano kifungu vha 16 kinakataza na kutoa adhabu kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi, lakini hakikuweka bayana taarifa zipi zinaweza kuwa sahihi na zipi sio sahihi.
Sheria ya Takwimu inaminya uhuru wa vyombo vya habari na asasi za utafiti  kutoa taarifa kwa umma kwa kuzuia kutolewa kwa taarifa kwa kigezo cha “taarifa ambazo zinapotosha”; kosa ambalo mtu akikutwa na hatia anaweza kulipa faini ya million 10 au/pamoja na kwenda jela kwa miaka 3. Hili linaleta uoga na hofu kwa upande wa watafiti, vyombo vya habari na asasi za kiraia kufanya tafiti na kuziwasilisha kwa uhuru. Sheria hii pia inahimiza tafiti zote zinazofanywa kutotolewa kwa umma kabla hazijapitiwa na kupitishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jambo ambalo linalorudisha nyuma uhuru wa kupokea taarifa tofauti za utafiti na mawazo mdala.
Ukiacha Sheria za Makosa ya Mtandao na Sheria ya Takwimu, bado zipo sheria nyingine kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 zinaendelea kutumika bila kufanyiwa mabadiliko, zikiminya uhuru wa vyombo vya habari na habari. Sheria ya Magazeti ilitokana na sheria kama hiyo ambayo iliwekwa na wakoloni kwa dhumuni la kukwamisha harakati za ukombozi, ikiwanyima uhuru waandishi wa habari kwa kuwa na vifungu vinavyowabana katika kutafuta na kutoa taarifa fulani, hasa zinazoigusa serikali. Kwa upande wa Sheria ya Usalama wa Taifa, vyombo vya habari vinazuiwa kuandika kuhusu mambo ambayo ni kwa maslahi ya kulinda usalama wa taifa, lakini sheria haijaweka bayana ni mambo gani hayo.  Pia Sheria ya Utumishi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma zinawabana watumishi kutoa taarifa kwa umma.
Pia hivi karibuni kuzuia vyombo vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya majadiliano Bunge ni kuvinyima uhuru na kuwanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata taarifa. Hatua hii inapaswa kupingwa kwa nguvu zote, kwani inawanyima wanachi haki yao ya msingi ya kupata habari moja kwa moja bila kuhaririwa wala kuchujwa. Wananchi wana haki ya kujua ni nini wawakilishi wao (wao) waliowachagua wanafanya na namna wanavyowawakilisha Bungeni.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza na kuhimiza utekelezwaji wa haki za binadamu. Vyombo vya habari vimekua ni wadau wakubwa katika kusambaza elimu na hali ya haki za binadamu Tanzania, na Kituo kimekuwa kikifanya navyo kazi kwa karibu katika hilo.
Uhuru wa vyombo vya habari umeendelea kupata changamoto kwa kutokuwepo kwa sheria inayoongoza vyombo vya habari. Sote tunajua kuwa mchakato wa upatikanaji wa sheria hizi umekwama wa muda mrefu sasa.
Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kwa mustakabali wa taifa letu la Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapendekeza yafuatayo:
1.      Kituo kinatambua na kupongeza juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya ofisi. Vyombo vya habari vinaweza kusaidia sana  katika mapambano haya iwapo havitaminywa na sheria na mazingira. Hivyo serekali haina budi kurekebisha sheria na kufuta vifungu kandamizi vyenye kuminya uhuru wa habari na wanahabari na kuwapa wanahabari uwanja mpana wa kutafuta na kutoa habari kwa uhuru, kama; Sheria ya Magazeti,  Sheria ya Usalama wa Taifa, Sheria ya Utumishi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
2.      Sheria za makosa ya  mitandao na takwimu ni vizuri sheria hizi zikaangaliwa upya na kurekebishwa ili kutoathiri haki za msingi za binadamu na utendaji kazi wa vyombo vya habari na asasi za kiraia. Kituo kinatoa wito kwa serikali kuimarisha nguvu ya vyombo hivi na asasi za kiraia kufanya tafiti na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuongeza uwajibikaji na uheshimuji wa haki za binadamu na sheria.
3.      Serikali kuanzisha upya mchakato wa kupata Sheria ya Vyombo vya Habari,  wanahabari na haki ya kupata habari ili tuweze kupata sheria nzuri  na zinazoenda na wakati zitakazolinda na kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari.

1.      Pia Kituo kinatoa rai wa wanahabari na vyombo vya habari kuzingatia uweledi na maadili ya kazi yao kwa kutoa taarifa sahihi, zenye uchunguzi na zenye lengo la kuelimisha, kuendeleza na kujenga jamii yenye kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na utawala wa sheria nchini.
Mwisho, Watanzania wana haki ya kupata taarifa mbalimbali, kutoa na kupokea maoni mbali mbali na mbadala kuhusu mambo yote yanayo wahusu. Hivyo  uhuru wa vyombo vya habara ni msingi muhimu wa kujenga jamii ya kidemokrasia, yenye kuheshimu haki za binadamu,  utawala wa sheria na kwa  maendeleo endelevu yetu sote.

Imetolewa na;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
  

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.