SIASA

ACT WAZALENDO WAZUNGUMZIA UTEKAJI NA MAUAJI NCHINI

Katika siku za hivi karibuni, nchi yetu imeshuhidia mlolongo wa matukio ya watu kutoweka na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Mnamo Novemba mwaka jana kuliripotiwa taarifa za kutoweka kwa kijana Ben Rabiu Saanane, mtanzania na mkazi wa jiji la Dar es salaam.

Tukio hilo lilifuatiwa na kuripotiwa upatikanaji wa miili ya watu  saba huko Bagamoyo maeneo ya mto Ruvu, katika vyombo mbalimbali vya habari. Mpaka tunatoa taarifa hii, ni zaidi ya miezi minne sasa Ben Saanane hajulikani alipo, na wala haijulikani ikiwa angali hai au amekufa.

Wakati wananchi wakiendelea kugubikwa na sintofahamu hiyo, hivi juzi  6 Aprili, 2017 majira ya usiku, pia kuliripotiwa tukio la kuvamiwa na kutekwa kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya Ibrahim Mussa maarufu kwa jina la ‘Roma Mkatoliki’ akiwa na wenzake watatu katika studio ya Tongwe Records, Masaki jijini Dar es salaam, na mpaka sasa hawajulikani walipo.  

Duru za matukio ya watu kutoweka, kupotea na wengine kupatikana wakiwa wamekufa limekuwa ni jambo la kawaida katika nchi yetu na linaloelekea kuzoeleka masikioni mwa watanzania.
 Wakati umma wa watanzania ukiendelea kushuhudia taarifa za namna hiyo, mamlaka zinazohusika na ulinzi na usalama wa raia zimekuwa hazitoi maelezo, na pale zinapotoa maelezo, yamekuwa ni maelezo ambayo hayaonyeshi kutoa ufumbuzi wa matatizo wala kueleweka kimantiki. 
Chama cha ACT Wazalendo tumeshtushwa na kusikitishwa na matukio hayo ya watu kupotea au kupotezwa hovyo katika nchi ambayo hakuna vita . Tunalaani kwa nguvu zote matukio hayo yenye sura ya uwepo wa hali ya kuogofya na kuitia hofu jamii.  
Ikumbukwe kuwa, Chama cha ACT Wazalendo, kinaongozwa na misingi mikuu kumi. Miongoni mwa misingi hiyo ni pamoja na Uwajibikaji, Uhuru wa Mawazo na Matendo, na Utu. Chama chetu kinawajibika kuhakikisha kinashiriki kikamilifu katika ulinzi wa haki za kibinadamu na kiraia. 
Matukio ya raia kutekwa, kutoweka na wengine kupatikana wakiwa wameuwawa katika mazingira yasiyoeleweka, yanakwenda kinyume na utu na yanakiuka haki za binadamu.


Kwa kuzingatia hali hii tete ya usalama na uhai wa watu katika nchi yetu, Chama cha ACT Wazalendo kinaitaka serikali kupitia mamlaka husika;-

i. Kueleza kinagaubaga, ni nini sababu na kiini cha matukio hayo ya watu kutoweka, kutekwa na kuuawa hovyo;
ii. Kuchukua hatua za maana, na za makusudi katika hali ya udharura na yenye uzito mkubwa ili kuhakikisha watanzania waliopotea wanapatikana mara moja;
iii. kutoa maelezo ni kwa nini haiwajibiki ipasavyo katika kutoa uzito kwa miili ya watu wanaookotwa na kukutwa wamekufa (wameuawa?!) katika maeneo mbali mbali hapa nchini, mfano watu waliookotwa Bagamoyo eneo la mto Ruvu,  na badala yake miili hiyo inatelekezwa  kinyemela na kutupwa hovyo bila kufuata na kuzingatia hatua makini za kiuchunguzi ili kubaini vyanzo na sababu za vifo hivyo;
iv. Kueleza kwa umma ina mikakati gani mahsusi ya kuzuia matukio ya utekwaji na upotezwaji wa raia ili watanzania waishi kwa amani na utulivu, huku wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Mwisho, Chama cha ACT Wazalendo tunaieleza serikali kuwa jambo la kwanza na la muhimu kwa wananchi ni Uhai na usalama wao. Tunamtaka Rais John Magufuli, aliyekabidhiwa dhamana ya maisha ya watanzania, atueleze watanzania ikiwa kama serikali yake imeshindwa kusimamia ulinzi wa watu wake hasa wakati huu ambao maisha yetu ya kila Mtanzania  yako rehani.
 Tunaiambia serikali ya Rais Magufuli sisi ACT wazalendo hatutanyamaza mpaka matendo haya ya utekaji na ukamataji usiofuata sheria vikome

 Tunamkumbusha kwamba, dhamana ya msingi aliyokabidhiwa siku anakula kiapo cha kuongoza nchi, si nyingine bali ni dhamana ya kuwalinda watanzania, awajibike kufanya hivyo sasa. 

Janeth Rithe
Katibu, Kamati ya Maendeleo ya Jamii
Aprili 8, 2017
Dar es salaam

About HABARI24 TV

Post a Comment
Powered by Blogger.