Thursday, April 27, 2017

UNAKUMBUKA TAMKO LA MWAKYEMBE LA VYETI VYA KUZALIWA KWENYE NDOA,RITA WAMEMFANYIA HAYA LEO

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini nchini- RITA umempa tuzo ya heshima aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria mhe. Dkt Harrison  Mwakyembe kutambua mchango wake katika kuboresha hali ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu nchini.

Tuzo hiyo ya RITA alikabidhiwa Dkt Mwakyembe na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba  Kabudi katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za Wizara mjini Dodoma

Akimkabidhi tuzo hiyo Prof. Kabudi alimpongeza DKT Mwakyembe kwa jinsi alivyojitoa na kuhakikisha hali ya usajili inaboreka na hivyo kuinua mwamko wa wananchi na kuona umuhimu wa kujisajili na kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Aliwataka watumishi wa RITA na wa Wizara waliokuwepo katika hafla hiyo kuiga moyo wa Dkty Mwakyembe wa kujitoa ili kuhakikisha kazi yake inakuwa na mafanikio.

Akizungumza baada ya kupokea Tuzo hiyo Dkt .Mwakyembe aliwaahidi RITA na Wizara kwa ujumla kuwa ataendelea kuwaunga mkono kupitia Wizara yake mpya ya Habari na kuwataka waendeleze jitihada zao katika usajili ili kuwafanya Watanzania wote wapate vyeti vya kuzaliwa.

“Sina neno  kubwa la kuwaambia zaidi ya asante, asanteni sana,niwaahidi kwamba nitaendelea kuwaunga mkono huko nilikoenda, nanyi lazima muendeleze kazi ya kuhamasisha usajili kwa nguvu zenu zote, mjue kwamba mna kazi kubwa mbele yenu na ni lazima ifanikiwe”, alisema Dkt Mwakyembe.

Alisema kazi ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu ina umuhimu mkubwa kwa jamii yetu, hii ni kwa ajili ya usalama, uchumi , kijamii na kwa ajili ya maendeleo ya nchi na hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha watanzania wote wanasajiliwa ili tuweze kuilinda vyema Tanzania yetu.  Kila Mtanzania lazima asajiliwe, lazima ajulikane, hili litasaidia nchi kuhakikisha mgawanyo wa rasilimali zake unakuwa ipasavyo”, alisisitiza Dkt Mwakyembe.


No comments: