Sunday, June 25, 2017

FUTARI YA MSTAHIKI MEYA WA KINONDONI - SHEIKH MKUU WA MKOA ATOA UFAFANUZI KUHUSU KUANDAMA KWA MWEZI

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa niaba ya Muft Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuber ametoa taarifa kwa umma leo jijini Dar es Salaam katika futari iliyoandaliwa na Meya wa Kinondoni Benjamini Sita na kueleza kuwa mpaka sasa hakuna taarifa za kuandama kwa mwezi hivyo waislamu nchini watatakiwa kuendelea na mfungo wa mwezi wa Ramadhan kwa siku ya kesho.

Sheikh Alhad amefafanua kuwa sikukuu ya Eid El Fitr itaswaliwa siku ya Jumatatu, ambapo kitaifa swala ya Eid itaswaliwa Mkoani Kilimanjaro na kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, huku kwa Mkoa wa Dar es Salaam itaswaliwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuongozwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaj Ally Hassan Mwinyi.
Kwa upande wake kiongozi wa dhehebu la SHIA Ithna Shariya Sheikh Hemed Jalala ameelza kuwa ni vyema waislamu wakayaendeleza mema ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwani hiyo ndiyo dhamira ya mwezi huo na siyo vinginevyo.
Huku Mjumbe wa Baraza la Ulamaa ambaye alikuwa anamuwakilisha Muft Abubakar Zuber Sheikh Ally Ngeruko aliwataka watanzania kuendelea kuhubiri amani na kuwapuuza wanaofanya uchochezi, ambapo amewaomba waislamu na watanzania kwa ujumla kuungana na kumuombea Rais Magufuli ili aendelee kutetea rasilimali za taifa kwa maslahi ya wanyonge.
Mwenyeji wa hafla hiyo Mstahiki Meya Benjamini Sita aliwashukuru viongozi wa dini na watu mbalimbali kwa kuhudhuria huku akiwaomba waumini wa dini zote kuyazingatia mawaidha yaliyotolewa na viongozi hao ya kuendeleza uchamungu hata baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
   

No comments: