Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari, kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Kituo hicho, Bw. Ezekiel Massanja. |
KITUO CHA SHERIA na haki za binadamu (LHRC) kimepongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano kwa kupambana na mafisadi, ikiwamo hatua ya kuundwa kwa kamati mbili za Rais zilizokuwa na lengo la kuchunguza thamani halisi ya madini yaliyomo katika makasha ya mchanga wa madini (makinikia) na ile ya kuwafikisha viongozi waandamizi wa kampuni ya IPTL mbele ya vyombo vya sharia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi. Anna Henga amesema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hatua za serikali ya awamu ya tano hususani katika suala zima la uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za Nchi, na kusema wamebaini kuwa serikali inapaswa kuungwa mkono ili vita hiyo ya uchumi iweze kufanikiwa.
Amesema ukiangalia maamuzi makubwa yanayochukuliwa na Mh. Rais yote yamelenga kurudisha hadhi ya Taifa ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi walio wengi hivyo kuna kila sababu ya kuumunga mkono ikiwemo kutoa ushauri mbalimbali.
“Ikumbukwe mnamo Juni 9 mwaka 2017 kituo cha sharia na haki za binadamu kilitoa tamko hapa mbele yenu kupinga kusudio la mamlaka ya udhibiti wa nishati na madini (EWURA) kuiongezea muda wa kuzalisha umeme kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa muda wa miezi 55” na kuanzia hapo tulishuhudia hatua ambazo zilichkuliwa na serikali kama kituo tunapongeza hatua iliyochukuliwa ya kuwapeleka mahakamani wahusika wakuu wa kashfa ya Tegeta Escrow ambao ni zao la kampuni ya IPTL.
Amesema hatua zinazochukuliwa sio tu zinaleta heshima katika Taifa lakini pia zinarejesha Imani ya Watanzania kwa serikali yao kwani wanaona kumbe dhana ya uwazi na uwajibikaji inawezekana na pia inafuta dhana ambayo imejengeka kuwa viongozi wanalindana.
Licha ya kuwepo kwa pongezi hizo lakini kituo cha sharia pia kimetoa angalizo kama kweli tunahitaji kuwa na vita ya uchumi yenye mafanikio katika Taifa la Tanzania lazima yafuatayo yakafanyika.
…YAKUMBUSHA YAFUATAYO KUFANYIKA
Kuundwa kwa mamlaka kamili ya madini; Kituo cha sharia na haki za binadamu kimeishauri serikali kuunda Mamlka kamili ya Madini itakayokuwa inafanya kazi ya uratibu wa shughuli zote za madini Tanzania kama zilivyo Mamlaka ya hifadhi ya Jamii. Mamlaka ambayo itakuwa na dhima ya kushughulika na mikataba yote ya madini, mapato ya madini, kuidhinisha leseni (vibali), kuratibu soko la madini ambapo madini yote yatauzwa hapa Nchini ili kupata fedha za kigeni.
Waliotajwa katika kamati zote mbili kuchukuliwa hatua, Pia kituo kimeshauri kuwa wale wote waliotajwa katika ripote zote mbili za Rais wachukuliwe hatua ikiwamo kuwafikisha katika vyombo vya sharia kujibu tuhuma zao.
Waitaka bunge kubadilika Kituo cha sharia kimetaka Bunge kubadilika kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya awamu ya tano, lisiendeshe mijadala kisiasa bali kwa lugha za kibunge na kutanguliza maslahi ya Nchi mbele.
“Tumefika hapa na kashfa hizi ambazo zimedumu kwa miongo kadhaa kwa sababu ya kuwa na bunge dhaifu lisiloweza kuisimamia serikali kwa dhati hususani katika mambo makubwa ya kitaifa. Sasa kila hoja inayowasilisha katika bunge ipewe uzito unaostahili pasipo kujali itikadi ya vyama ambazo kwa kiasi kikubwa imechangia kwa kashfa hizi kuendelea kudumu kwa miongo kadhaa” Alisema.
Mambo mengine ni pamoja na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo, serikali kuheshimu misingi ya haki za binadamu, serikali kuheshimu na kulinda demokrasia pamoja na serikali kuwachukulia hatua watu wote waliohusika katika miamala ya Tegeta Escrow. Pia imeitaka serikali kuchukua hatua katika kashfa zingine ambazo zimesababisha Serikali kupata hasara ikiwamo kashfa ya ununuzi wa rada, kashfa inayohusishwa na Kampuni ya Lugumi, kashfa ya Richmond, kashfa ya uwepo wa harufu ya rushwa katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na mifuko ya hifadhi ya jamii …mathalani mradi wa NSSF kigamboni pamoja na suala la Vitalu vya uwindaji na umiliki wake
No comments:
Post a Comment