Sunday, October 22, 2017

WAFANYA BIASHARA WA MIPAKANI WAMETAKIWA KUTUMIA URAGHBISHI KATIKA KUTOA MAFUNZO KWA WAFANYA BIASHARA WENZAO

Ikiwa ni siku ya tatu ya semina kwa wafanya biashara wa mipakani, wafanyabiashara hao wametakiwa kutumia mbinu ya Uraghibishi katika kufikisha elimu kwa wafanya biashara wenzio ambao hawajapata nafasi ya kuhudhuria semina hiyo.
Hayo yamesemwa na muwezeshaji wa semina hiyo dada beatrice Hezekiel alipokuwa akiongoza semina hiyo mapama jana makao makuu ya mtandao wa jinsia Tanzania(TGNP).

Dada Beatrice alisema kuwa uraghbishi ni njia nzuri ya kuelimisha hasa watu wazima kwani mnabadilishana uzoefu kati ya muwezeshaji na wawezeshwaji  kwa kuchangia mada na kutoa shuhuda mbalimbali ambazo na wao wamezipitia katika ufanyaji wao wa biashara katika mipaka na maeneo mengine mengi.
Uraghbishi ni mchakato au njia shirikishi ya kupata au kuibua taarifa baina ya watu waliowekwa kando, lakini pia njia hii inasaidia kufikia malengo ya kuendeleza vuguvugu la jinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Paulo Freire mwanaharakati na mwanafalsafa wa nchi ya Brazili yeye alikuwa akipinga dhana ya elimu inayopelekea ukandamizaji kwa kuonekana mwanafunzi anayefundishwa basi ubongo wake unakuwa mtupu na mwalimu anayemfundisha ndio anamuwekea vitu kichwani mwanafunzi huyo, wakati si kweli mwanafunzi anayejifunza anahitajika kushirikishwa kwani na yeye ana uzoefu na mchango wake na njia hii inaitwa ni ukandamizaji wa akili.
Lakini pia Mwalimu Nyerere baada ya ukoloni alikuja na falsafa ya kujikomboa kiuchumi hivyo kuachana na ukoloni mambo leo na kusisitiza elimu inayozingatia mazingira/muktadha kwa mwanafunzi anayepewa elimu basi apate na elimu ya kujitegemea, kwa kuwa mwalimu aliamini Mtanzania yeyote ataweza kujikomboa kupitia elimu hiyo.

Dada Beatrice aliendelea kusisitiza kuwa wakufunzi hao wanatakiwa kuwa Waraghbishi na sio wahamasishaji kwani mraghbishi anatoa elimu kwa njia ya vitendo na kushirikisha wanafunzi wake, lakini Muhamasishaji anaongea yeye kila kitu na kutegemea asikilizwe tu bila kuwasikiliza na anaowafundisha.
Aidha muwezeshaji huyo aliwataka washiriki kutumia mbinu nzuri na za kisasa katika kufikisha ujumbe huo kwa walengwa kama maigizo, Majadiliano katika vikundi, kudadisi, midaharo, mafunzo shuhuda na njia nyingine nyingi nzuri zitakazowarahisishia kazi zao.

                               

No comments: