Watanzania
wametakiwa kuwa ni watu wenye upendo, mshikamano na umoja ili kuendelea
kuidumisha Amani tuliyonayo ambayo ni kama Tunu tuliyojaliwa Watanzania.
Hayo yamesemwa
mapema leo jijini Dar es salaam na Sheikh Mkuu wa dhehebu la Shia ithanasheria
Maulana Hemed Jalala, ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya kumuenzi Mtume Mohammad S.A.W.
Maadhimisho hayo
yaliyoadhimishwa kwa kuwa na mtembezi ya hiari yaliyoanzia kituo cha mabasi cha
Ilala Boma na kwenda mpaka makao makuu ya Dhehebu la Shia Tanzania yaliyopo eneo
la Kigogo Posti jijini Dar es salaam.
Sheikh Jalala
alisema kuwa lengo la matembezi hayo ni kukumbuka na kumuhenzi Mtume Mohammad
ambaye alifariki miaka takribani 1400 iliyopita, lakini leo hii anakumbukwa kwa
mengi mazuri aliyoyatenda akiwa hapa duniani.
Aidha Sheikh
Jalala alisema kuwa licha ya kuwa mtume alikuwa ni Nabii na kiongozi wa Waislamu
lakini alipendwa na watu wa dini zote kwa kuwa alishirikiana nao na hakuwabagua
kutokana na dini zao, kabila, rika wala rangi na alishirikiana nao watu hao
katika maisha yake yote mpaka kufa kwake.
Lakini pia
hii inatufundisha sisi kama watanzania kupendana kushirikiana kuondoleana
visasi pamoja na chuki zisizo na msingi au kutengana kutokana na itikadi za
kidini, kuwekea na vikwazo kati ya wakristo na waislamu au watu wa dini
nyingine ila tunatakiwa tupendane, tushirikane na tulinde amani yetu kwani sisi
sote ni watanzania.
Sheikh huyo
aliendelea kwa kusema kuwa mtume alikuwa hapendi kuona mtu yeyote akionewa
aidha awe Muislamu, Mkristo, Muyahudi hata Mpagani bali yeye alimtetea kwa kuwa
ni mwanadamu, lakini pia alionyesha kuwajari yatima na wajane na kuwapa utetezi
ili na wao wawe na amani na furaha kama watu wengine katika dunia.
Na mwisho
kabisa Maulana Jalala alipenda kuwashauri viongozi wa dini zote ikiwemo Masheikh,
Maimamu, Mapadri, Wachungaji na maaskafu kote nchini kufundisha na kuubiri
amani na mshikamano kwa taifa letu ili tuendelee kuilinda Amani yetu
tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kama Tunu yetu.
No comments:
Post a Comment