Sunday, June 14, 2015

Bima ya Taifa ya Afya yatoa mikopo kwa ajili ya maboresho ya huduma za kiafya

Afisa wa Bima ya Afya makao Makuu, Isaya Shekifu wakati akiwasilisha mada zake kwa washiriki,kushoto ni meneja wa mfuko huo mkoa wa mtwara, Joyce Sumbwe.
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya katika juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma zake na kuhakikisha wanachama wake na wananchi wanapata huduma bora imehamasisha viongozi na wadau wa sekta ya Afya Mkoani Mtwara kuchangamkia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo toka Bima ya Afya.
Akizungumza katika warsha iliyokutanisha wadau wanaohusika na utoaji wa huduma hiyo, Afisa wa Bima ya Afya makao Makuu, Isaya Shekifu alisema kuwa mpango huu wa mikopo ya vifaa tiba ulianza tangu mwaka wa fedha 2007/2008 na umekuwa ukiboreshwa kila wakati kutokana na mahitaji ya wadau na nia ya mfuko ya kuboresha huduma za afya.
 baadhi ya wadau wanaohusika na utoiaji wa huduma .

Alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa mikopo ya vifaa tiba mwaka 2008 hadi kufikia Disemba mwaka jana kiasi cha 10.24 bilioni ziliidhinishwa kwaajili ya vituo 194 na kati yake vituo 146 vilikidhi masharti na kuchukua mkopo wa Sh. 5.34 bilioni.
Aidha alieleza kuwa kwa upande wa mikopo kwaajili ya ukarabati wa vituo vya kutolea huduma kiasi cha Sh. 6.8 bilioni ziliidhinishwa na walioweza kukidhi masharti waliweza kuchukua kiasi cha Sh. 2.14 bilioni.
 “Kwa mkoa wa Lindi na Mtwara mwamko umekuwa mkubwa na wameupokea vizuri ,wengi wao wameomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea kuboresha mpango huu ”alisema Shekifu na kuongeza

“Iko mikopo ya aina nne wa kwanza ni wa vifaa tiba ambao marejesho yake ni kwa kipindi cha  miezi 24 mpaka 60, wa pili ni mkopo wa vifaa vya Tehama ambao nao ulipaji wake ni miezi 24 mpaka 60,mkopo wa dawa na vitendanishi ambao marejesho yake ni kwa  kipindi cha miezi 15,”alisema Shekifu
Aidha alieleza kuwa mkopo na marejesho yake yatategemea madai ya kila mwezi ya mkopaji kwa huduma za matibabu zitolewazo kwa wanachama wa Mfuko na vyanzo vingine ambavyo kituo kitabainisha kutumika kulipia mkopo na mkopaji anatakiwa kujaza fomu ya maombi kama Mwongozo wa Serikali kwa Vituo vya Afya unavyoainisha na fomu ya maombi itatozwa kiasi cha Sh. 20,000
Akizungumza Meneja wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoa wa Mtwara, Joyce Sumbwe alisema kuwa kwa mkoa wake hali si  mbaya na tayari baadhi ya watoa huduma wameweza kukopa hadi mara ya pili na kiasi cha Sh.170 milioni zimeweza kutolewa kwaajili ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo.
“Hali si mbaya sana kwa mkoa wa Mtwara baadhi  ya watoa huduma  washaanza kukopa hadi kwa mara ya pili na kiasi cha Sh.170 milioni  zishatolewa kwaajili ya vifaa na kwa wilaya za Masasi,Tandahimba na ,Newala zimeweza kukopa pamoja na zahanati ya Fajma,Likombe, na hospitali ya mkoa,”alisema Sumbwe

Aidha aliendelea kubainisha kuwa  kwa sasa wanaendelea kusajili maduka ili watu watakapohitaji huduma za dawa katika vituo na kukosa basi waweze kuzipata katika maduka ya dawa ikiwa ni sambamba na kuendelea kuwaelimisha watu waone umuhimu wa Bima ya afya.

No comments: