Saturday, July 23, 2022

Waziri Ndalichako Atoa Maagizo kwa Mifuko ikiwemo NSSF na PSSSF Kuwalipa wastaafu mafao yao.

Na Muandishi wetu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira ,Vijana na Watu wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako ameagiza Mifuko ya mafao kwa wastaafu ikiwemo NSSF na PSSSF kuhakikisha wanawalipa Wastaafu wote wanaodaia  ikiwemo wanaodai kiinua mgongo,fidia,na Waliopunjwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira ,Vijana na Watu wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wazee waliyofika katika ukumbi wa NSSF Ilalal Boma jijini Dar es salaam.

Agizo hilo amelitoa leo Dar es salaam katika Mkutano aliouandaa Kwa ajili yakukutana na wastaafu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa lengo ni kusikiliza malalamiko yao ,ambapo amedai kuwa tangu ameingia kwenye Wizara hiyo takribani miezi sita  amebaini wastaafu wengi wamestaafu  lakini bado hawajalipwa stahiki zao na wanaishi maisha magumu hivyo waje na vielelezo ili wafanyiwe mchakato wa kulipwa.

"Wastaafu hawa wanaodai madai yao wapo katika makundi tofautitofauti ikiwemo mapunjo ambapo mafao ya mtu yamekokotolewa kwa kutumia mshahara ambao ni mdogo kuliko mshahara halisi wa mfanyakazi alipostaafu na kusababisha mafao ya mkupuo anayopewa ni kidogo kuliko ilivyotakiwa"amesema Profesa Ndalichako.

Hata hivyo Waziri Ndalichako amesema kwamba amefuatilia na kubaini kuwepo kwa kesi za wastaafu ambazo  ziko wazi nakwamba suala lililopo  nikwenda tu kurekebishiwa mapunjo yao na kulipwa kwa kuzingatia mshahara wake wa mwisho ,nakusisitiza wastaafu  hao warudishiwe stahiki zao zote walizokuwa wanapunjwa.

Aidha amesema kwamba kuna baadhi ya Wastaafu vikokotoo vyao viko sawa lakini walikuwa hawana Elimu juu ya Vikokotoo hivyo,ambapo wamepatiwa Elimu na kujiridhisha kwamba hawajapunjwa mafao yao.
Zoezi la kuwasikiliza wazee likiendelea.

Kadhalika  Waziri Ndalichako amesema kumekuwa na makosa ya kiutendaji kutoka kwa baadhi ya watendaji wa mifuko ya pensheni kutokusikiliza malalamiko ya wastaafu wanaokuja kudai stahiki zao hivyo ameagiza watendaji hao kuacha tabia hiyo kwani wao ni watishi wa Umma.
 
Kwa upande wake Kassim Mafanya Mkazi wa Dar es salaam ambaye alikuwa Mtumishi  Chuo cha askari  Magereza Ukonga  amesema anashukuru kupata nafasi kusikilizwa kwani wastaafu wengi wamekuwa wanaishi kwa msongo wa mawazo na maisha yao hayaeleweki hawajui kesho yao  wamekuwa wakiahidiwa kupata nyongeza lakini hakuna kinachoendelea wengine wanafariki bila hata ya kufaidi chochote kutokana na jasho lao.

Naye Mtumishi Mstaafu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Chuki Kashaija mwenye ulemavu wa miguu  amesema alianza kazi tangu mwaka 1973 nakustaafu mwaka 2014,ambapo  amesema mpaka sasa hajapata mafao yake takribani miaka 8 sasa.

Wizara hiyo imepanga kufanya zoezi la kusikiliza malalamiko ya Wastaafu nchi nzima ikiwa ni Utekelezaji wa  agizo la rais Samia Suluhu Hassan aliloliagiza siku ya wafanyakazi Duniani( Mei mosi) iliyofanyika mwaka huu Jijini Dodoma.

Wednesday, July 20, 2022

Chuo kikuu cha Arusha chawashauri vijana kusoma kozi zitakazowawezesha kujiajiri.

Chuo Kikuu cha Arusha kinachomilikiwa na kanisa la Waadventista (Wasabato)kimewashauri wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na Elimu ya  juu kusoma huku wakitambua changamoto ya ukosefu wa ajira siyo ya Tanzania pekee bali ya dunia nzima hivyo wanapswa kupata maarifa ya kujiajiri kupitia fursa za masomo wanazozipata.

Mwenyekiti wa jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Askofu Mark Malekana ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Arusha akizungumza na wanahabari kwenye banda la chuo hicho katika maonesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Askofu Mark Malekana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye  Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa Wizara ya Elimu Sayansi na teknolojia kupitia tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es  salaam. 

"Chuo chetu kina  falsafa yakipekee katika utoaji wa Elimu, tunamtayarisha Mwanafunzi  kiroho,kisaikolojia,kiuchumi na katika nyanja zote za maisha  kwa kufanya hivyo tunategemea mhitimu hata akikosa ajira atajiajiri mwenyewe bila kutegemea kuajiriwa"amesema Askofu Malekana.

Aidha amesema kwamba kupitia maonesho hayo wameamua kuzungumzia kwa kina na wazazi au walezi wanaofika kwenye Banda la chuo hicho kwenye viwanja vya Mnazi ili kuwashauri waweze kujiunga na masomo chuoni hapo wapate maarifa mazuri yatakayoweza kuwasaidia kujiajiri.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Chuo Kikuu cha Arusha Elisha Lomay ( wa kwanza kulia) akiwa na maafisa udahili wa chuo hicho katika Banda la Maonesho la chuo hicho .
Awali Mkuu wa Kitengo Cha Masoko wa Chuo hicho  Elisha Lomay  amewambia waandishi wa habari kwamba chuo hicho kinatumia falsafa ya kumjenga mwamanafunzi akue katika maadili ya kiroho ,Kimwili, pamoja na kitaaluma ambapo wahitimu wengi wamekuwa wakifanikiwa kufanya kazi Kwa weledi mkubwa.

Amendelea kufafanua kuwa  chuo hicho ambacho kipo Wilayani Meru Mkoani Arusha kimekua kikidahili wanafunzi bure kupitia njia ya mtandao,nakwamba baada ya wanafunzi kujiunga na chuo hicho wanalipia ada ambazo Wanaweza kuzimudu ambapo zinalipwa kwa awamu.

" Chuo chetu kinatoa ufadhili( Scholarship ) Kwa wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi kwa kushirikiana na wasabato wenzetu wanaoishi nje ya nchi ikiwemo Marekani,hivyo tunawakaribisha wazazi na walezi kuwaleta watoto wao kujiunga na chuo chetu kwani kina mazingira rafiki yakujisomea na gharama za ada na malazi ni nafuu" amesema Lomay.

Aidha amesema kwamba program wanazofundisha chuoni hapo ni pamoja na  Shahada za kidini,Utawala wa Biashara na Uhasibu,Sanaa ,Ualimu  pamoja na ngazi ya cheti na Astashahada ya Elimu ya Dini(Diploma) katika nyanja mbalbali.

Monday, July 18, 2022

Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) kimekuja na mambo haya mazuri katika maonyesho ya 17 ya Vyuo vikuu.

Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizokuwa za Shahada wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha( RUCU) Dkt Wille Migodela (wakatikati) akifuatilia maelekezo yanaoyotolewa na mmoja wa maafisa wa udahili wa Chuo hicho Kwa mwanafunzi aliyetembelea banda hilo kwenye maonyesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini( TCU), yanayofanyika Viwanja vya  Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizokua za Shahada wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha( RUCU) Dkt Wille Migodela (wa kwanza kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa baadhi ya Wanafunzi waliotembelea banda la Chuo hicho kwenye maonesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) yanafofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) katika kuhakikisha kinakabiliana na changamoto zinazoikabili Jamii kimejikita kutoa Elimu kwa wanafunzi Kwa kufanya ubunifu wa tafiti mbalimbali Kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kimazingira Kama vile Mbu wanaoambukiza Ugonjwa wa Malaria.

Magonjwa Mengine ni magonjwa ya ngozi( Fangasi) na Kikohozi,ambapo wanafunzi wanafanya tafiti kupitia mimea ya asili nakutengeneza dawa ambazo zinasaidia kukabiliana na magonjwa hayo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizo za Shahada wa Chuo hicho Dakt Wille Migodela wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye maonyesho ya 17 ya Elimu y juu Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini ( TCU).

Aidha amesema kwamba chuo hicho kinatoa program za Kozi mbalimbali lakini Elimu ya utafiti wa Ubunifu imekua ikipewa kipaumbele ili kumsaidia mwanafunzi anaehitimu kuondokana na zana ya kutemea kuajiliwa na badala yake aweze kujiajiliwenyewe.

Hata hivyo amendelea kusema kwamba Wanafunzi hao wamefanikiwa kubuni kifaa kinachopima uzito wa mizigo inayobebwa na magari ambapo kifaa hicho kinafungwa kwenye gari na gari hiyo haitapita kwenye mzani Kwa ajili ya kupimwa, badala yake kifaa hicho kitaonyesha ukomo wa  uzito kamili unaohotajika kubebwa na gari hilo.

"Magari yanatumia muda mrefu kukaa kwenye foleni ya mzani kupima uzito wa mzigo,sisi kama RUCU tumekuja na suluhisho la kubuni kifaa Cha kisayansi kitakachoonyesha ukomo wa uzito wa mzigo unaotakiwa kupakiwa" amesema Dkt Migodela

Nakuongeza kuwa "kuhusu Faculty of Arts and Social  science ,tumetengeneza kifaa kinaitwa "Analogy wheel" kazi yake ni kupima umbali kwenye tambarare(horizontal distance) wakati wa kufanya Survey(upembuzi).
Kifaa kinafanya kazi mbadala wa Chain(mnyororo) ambao kwa mda mrefu umekuwa ukishindwa kutupa vipimo halisi kwasababu ya masikio(oval shape) yanayo uunganisha na pia chain inatumia mda mrefu kupima urefu ardhini.

Amesema kwamba Kwa mwaka huu wa masomo 2022/ 2023 wanatarajia kudahili  wanafunzi wapatao 1400 ambapo wanafunzi wa Cheti na Diploma ni 700 na wengine 700 ni Shahada(Digree),ambapo amesisitiza kwamba mazingira ya kujisomea Kwa wanafunzi ni mazuri.

Chuo kikuu SUZA kuja na Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Teknolojia ya Habari(IT)

Mkuu wa Kitengo Cha Uhusiano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Taifa Cha  Zanzibar( SUZA) Khadija Sadiq Mahumba ( mwenye kitambaa cheupe kichwani)akitoa maelekezo Kwa baadhi ya Wanafunzi waliotembelea Banda la chuo hicho kwenye maonyesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini ( TCU) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya watu waliotembelea Banda la Chuo kikuu cha Tifa Zanzibar SUZA wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Maafisa Udhahili wa chuo hicho wenye Tshirt za rangi ya bluu.

Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar(SUZA) kinaendelea kuunga mkono sekta ya elimu nchini Kwa kuanzisha kozi mpya ambazo ikiwemo ya  Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Teknolojia ya Habari(IT) katika mwaka wa Masomo 2022/ 2023.

Ameyazungumza hayo Mkuu wa Kitengo Cha Uhusiano na Masoko wa SUZA Khadija Sadiq Mahumba wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Maonyesho ya 17 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Time ya Vyuo Vikuu Nchini( TCU) Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.  

Aidha amesema kwamba chuo hicho kinatarajia kudahili wanafunzi wapatao 2000 Kwa programu mbalimbali zikiwemo za Elimu,Afya,Kilimo kwa ngazi mbalimbali ikiwemo  Cheti,Astashahada( Diploma) Shahada(Degree),Shahada ya Uzamili na Uzamivu.

Amesema kuwa kwa mwaka huu wa masomo chuo hicho pia kinatarajia kutoa programu ya Shahada ya Uzamivu( Phd) ya Lugha ya kiswahili ,na kwamba amewaomba wanafunzi wanaotaka kujiunga na SUZA wachangamkie fursa hizo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Uhusiano na Masoko SUZA amesema kwamba Chuo hicho kinatoa programu za Kozi za Utalii ambapo wanafunzi watakaosoma kozi hizo watapata fursa ya kusoma lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo lugha ya Kireno,Kichina ,Kifaransa,Kijerumani,na kwamba chuo hicho pia kinatarajia kuanza kufundisha Programu ya lugha ya Kikorea.

Hata hivyo amebainisha kuwa wakati wa udahili wa dirisha la pili wanatarajia kudahili wanafunzi kwa program mpya za Shahada ya Uzamili ya Benki na Fedha( MSc Benking & Finance) pamoja na Shahada ya Uzamili ya  Utawala wa Fedha na Biashara ( MBA-Finance).

" Ningependa kuwaomba wazazi wawalete wanafunzi  kwenye banda letu hapa Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wajionee kozi tunazofundisha ili wafanye maamuzi sahihi yakujiunga na chuo chetu chenye fursa ya kupata ajira nje na ndani ya nchi" amesema Khadija.

Wednesday, July 13, 2022

MAKAMU WA RAIS AKIFUNGA MAONESHO YA SABASABA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) mhandisi Prof. Fredrick Kahimba juu ya mtambo maalum wa kuchakata zao la Chikichi ili kuweza kupata mafuta ya Mawese wakati Makamu wa Rais alipotembelea Banda la Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba. Julai 13 ,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisiliza maelezo kutoka kwa washiriki mbalimbali katika Banda Maalum la Zanzibar wakati alipotembelea na kufunga Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam tarehe 13 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisiliza maelezo kutoka kwa washiriki mbalimbali katika Banda Maalum la wajasiriamali wanawake la Mama Anna Mkapa wakati alipotembelea na kufunga Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam tarehe 13 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa kilele cha Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam tarehe 13 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi zawadi kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuwa kinara wa Banda bora la Maonesho ya Sabasaba kwa mwaka 2022 wakati wa kilele cha Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam tarehe 13 Julai 2022.

Mwenyekiti wa Bodi wa Tantrade Dkt. Ng’wanza Soko akimkabidhi zawadi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kwa ushiriki wake katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam  wakati wa ufungaji wa maonesho hayo leo tarehe 13 Julai 2022.

Tuesday, July 12, 2022

TIC YATOA TATHIMINI YA MAONESHO YA SABASABA 2022, YATANGAZA MAFANIKIO YA MFUMO MPYA WA ‘ELECTONICS INVESTIMENT WINDOW’

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) John Mnali ametoa rai kwa wawekezeji wote wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa ya Mfumo mpya wa Kielectonic kupata huduma mbalimbali ikiwemo kuomba Vibali na Leseni za Biashara ikiwemo ya uwekezaji na kwamba mfumo huo umelenga kuwawezesha wawekejazi kupata huduma zote kwa wakati mmoja.
 
Mnali ameyasema hayo Julai 12,2022 alipokuwa akitoa tathimini ya maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayotarajiwa kufungwa rasmi Julai 13,2022 katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambao amesema kuwa Mfumo huo ujulikanao kama ‘TANZANIA ELECTONICS INVESTIMENT WINDOW’ umewezesha kuunganisha taasisi 6 kwa awamu ya kwanza na kwamba baadae wanatarajia kuongeza taasisi nyingine 11 zitakazofanya kazi kwa pamoja.
 
Ameeleza kuwa katika mfumo huo mwekezaji anaweza kuleta maombi yake kwa njia ya mtandao au kutoa taarifa ya kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, au kurekebisha cheti chake na kwamba kwa kupitia mfumo kunamfanya  mwekezaji kuondokana na usumbufu wa kutembea katika kila ofisi kufuata huduma.
 
“Huduma ziko kwa wawekezaji wote wa ndani na wa nje hivyo itakuwa vizuri kutumia fursa hii kuweza kuandikisha miradi yao, na kufanya maombi yao katika maeneo mambalimbali yanayohitaji huduma katika taasisi husika” 
 
“Kituo cha Uwekezaji tunafahamu kuna miradi mingi sana ambayo inafanyika na wawekezaji wa ndani ambayo haina cheti cha uwekezaji ukizingatia hali ya miradi yao jinsi ilivyo na ukubwa wake inastahili kupata cheti cha uwekezaji.
 
“Elimu hii tuliyoitoa hapa kwa siku zote hizi za maonesho ni vizuri sasa wananchi wanaotaka kuleta maombi mbalimbali watumie mfumo huu kuleta maombi yao, hii itawarahisishia sana kupata huduma kwa haraka” amesema 
Ameongeza kuwa ushiriki wao katika maonesho ya mwaka huu umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na kuwa na maeneo matatu waliyoshiriki ikiwemo Kliniki ya Biashara, uwepo wa eneo maalum la kuonesha utendaji kazi wa mfumo mpya wa ‘ELECTONICS INVESTIMENT WINDOW’, pamoja na ushiriki wao wa jumla ndani ya Banda la Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara lililojumuisha taasisi zote zinazofanyakazi chini ya Wizara hiyo.
Amewataka wananchi wote kutembelea katika ofisi zao za Kanda zilizowekwa kwaajili  ya kutatua changamoto mbalimbali za wawekekezaji waliopo nje ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo amezitaja Ofisi hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya  Kaskazini,  Nyanda za juu Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa.

MTENDAJI MKUU BRELA AKABIDHI VYETI VYA USAJILI KWA WAFANYABIASHARA SABASABA

 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Majina ya Biashara na Leseni (BRELA) Bw.Godfrey Nyaisa kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bi. Latifa Khamis wakimkabidhi Cheti cha Usajili wa Jina la Biashara Bw.Hussein Mustaali Lukmanjee jana kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Afisa MtendajiMkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Majina ya Biashara na Leseni (BRELA) Bw.Godfrey Nyaisa akimkabidhi Cheti cha Usajili wa Jina la Biashara Bi. Mariam Kihelelo jana kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Majina ya Biashara na Leseni (BRELA) Bw.Godfrey Nyaisa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Majina ya Biashara na Leseni (BRELA) Bw.Godfrey Nyaisa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo kwenye maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

MAGEUZI MAKUBWA YA KILIMO NDIO YATAKAYOWAINUA WANANCHI WA KIBAKWE

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene akizungumza katika mkutano wa Hadhara katika Kijiji cha Kirusi jimbo la Kibakwe Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene akikagua maendeleo ya ujenzi katika kituo cha afya Ipera kilichotengewa na serikali million 500 katilka jimbo la Kibakwe Halmashauri ya Mpwapwa.

Wananchi wakimsikilza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George Simbachawene katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kikuyu kata ya Ipera jimbo la Kibakwe Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa.

…………………………….

Na mwandishi wetu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri mkuu, Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amehimiza watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa kufanya mageuzi makubwa ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya kimkakati iltakayoongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.

“Lazima tuwekeze fedha kwenye miundo mbinu ya uzalishaji wa kilimo, wataalam wa kilimo wanaojengewa uwezo na wizara ya kilimo, wafanye kilimo shambani nawatumie maarifa waliyopata kwa kushirikisha wakulima”

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu (Mb) Mhe. George simbachawene wakati alipofanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kinusi Jimbo la Kibakwe katika Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa.

“Kata ya Malolo na kata Ipera ni eneo ambalo limejikita katika kilimo cha umwagiliaji, Halmashauri itizame namna ya kuimarisha miundo mbinu ya maji ili maji yasipote alisema Waziri”

Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika bajeti yake ya 2022-2023 imejikita katika maeneo ya uzalishaji, bajeti ya kilimo imeongezwa kutoka billion 200 mpaka billion 900, hivyo fedha nyingi zitaletwa kijijini katika miradi ya kimkakati ya kilimo.

“Amefafanua serikali imeleta pembejeo za ruzuku, baadhi ya gharama zitalipwa na serikali ili mwananchi wapate pembejeo kwa bei nafuu ni lazima maafisa kilimo wajue hiyo mifumo ili waweze kuwasaidia wakulima”

Awali diwani wa kata ya Ipera Mhe. Festo Myuguye ameomba serikali kupimia wananchi maeneo yao na viwanja vyao, ili wananchi waweze kupata fursa ya kutumia hati za viwanja vyao kupata mikopo.

“ tunaomba pia serikali itusaidie kujenga miundo mbinu ya maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo ili kuwafikia watu wengi, miundo mbinu iliyopo ilijengwa kabla ya Kijiji kuwa kikubwa”

RC SINGIDA APIGA MARUFUKU WANANCHI KUCHOMA MKAA NDANI YA MSITU WA MGORI

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mughanga kilichopo Tarafa ya Mgori Wilaya ya Singida, kuhusu uharibifu unaofanyika katika Hifadhi ya Msitu wa Mgori waakati wa ziarayake ya siku moja ya kutembelea msitu huo ambapo aliambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na wilaya hiyo.
Dk. Mahenge akiangalia uharibifu wa msitu huo uliofanywa na wavamizi kwa kukata miti.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Mulagiri akizungumza wakati wa ziara hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha akizungumza katika ziara hiyo.
Muhifadhi wa Misitu wa Wilaya ya Singida, Uswege Mwasumbi akitoa taarifa ya operesheni mbalimbali zilizofanyika za kuwaondoa wavamizi wa msitu huo.
Pikipiki yenye namba za usajili  T 869 CZR ikiwa na magunia ya mkaa baada ya mwendeshaji wake kukamatwa katika hifadhi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakijadiliana wakati wa ziara ya kukagua msitu huo.
Ziara hiyo ikifanyika.
Mifugo ikiwa ndani ya hifadhi hiyo.
Dk. Mahenge akiangalia wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama walivyokuwa wakibomoa moja ya nyumba isiyo rasmi iliyojengwa ndani ya hifadhi hiyo.
Ukaguzi wa msitu huo ukiendelea.
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wakiingia ndani ya nyumba isiyo rasmi iliyojengwa ndani ya hifadhi hiyo kabla ya kuibomoa.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiondoa gogo lililowekwa na wavamizi wa msitu huo kuzuia magari yasipite ili wasiweze kukamatwa.
Msafara wa magari ya wajumbe hao wakati wa ziarahiyo.
Baadhi ya wananchi wakiwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukutwa ndani ya msibu huo.
Diwani wa Kata ya Mughanga, Nassoro Hassan akizungumzia msitu huo mbele ya mkuu wa mkoa.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho akielezea msitu huo na jinsi walivyo ondolewa kwenye hifadhi hiyo baada ya kulipishwa fedha ambapo alidai hawana sehemu ya kulima wala kujenga.

Ukaguzi wa msitu huo ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk. Binilith Mahenge amepiga marufuku wananchi kuingia ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mgori  kufanya shughuli za kilimo, kuchoma mkaa na kuchunga mifugo bila kibali kutoka kwa mamlaka zinazohusika na uhifadhi wa msitu huo uliopo Wilaya ya Singida.

Ametoa onyo hilo leo Julai 13, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha  Mughanga baada ya Kamati ya Ulinzi na Usama ya Mkoa ilipotembelea msitu huo kujionea uharibifu uliofanywa na wavamizi huku wengine wakijenga nyumba za kuishi ndani ya hifadhi hiyo.

“Kwa sababu elimu tulikwishatoa na DC (Mkuu wa Wilaya) alipita vijiji vyote kutoa elimu ni marufuku kuingia ndani ya msitu huo na waambie yule mzee mwenye muvi (Dk.Mahenge) amekuja hana mzaha katika hili,” alisema.

Dk.Mahenge alisema mtu yeyote atakayekutwa ndani ya msitu huo atakamatwa na kama ana mifugo nayo itakamatwa kutaifishwa na kuuzwa.

Alisema kuendelea kuharibu misitu ya hifadhi ni laana kubwa ambayo wajukuu zetu wataweza kuja kutuchapa tukiwa ahela.

“DC alipita Novemba 2021 na akatoa elimu watu wasiingie kwenye msitu,wasilime wala kufugia mifugo lakini cha kushangaza leo watu wameuvamia na wanagawana kama mashamba na wamejiwekea mipaka baada ya kugawana ekari zaidi ya 200 hadi 300 kwenye msitu huo wenye miti aina ya Mininga,” alisema.

Mkuu wa Mkoa aliongeza kuwa baadhi ya maeneo wananchi wanahama na kwenda kuishi eneo jingine ili kupisha uhifadhi ili wanyama waendelee kuwepo na hivyo kuingizia serikali mapato ya fedha za kigeni kutokana na kutembelea hifadhi.

” Leo tunapata fedha kwasababu wazungu wanatoka kwao kuja kuangalia wanyama ambao kwao hawapo na sisi babu zetu waliwatunza wanyama ndio maana tumewakuta,” alisema.

Dk.Mahenge aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wanaohujumu msitu wa hifadhi wa Mgori ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Awali Muhifadhi wa Misitu Wilaya ya Singida, Uswege Mwasumbi, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida kuwa nyumba  704 za wananchi waliovamia msitu huo ambao upo mpakani mwa Wilaya ya Singida Vijijini na Mkoa wa Manyara zimebomolewa wakati wa operesheni iliyofanywa na askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Mwasumbi alisema kati nyumba hizo zilizobomolewa 557 ni za ukanda wa eneo la kitongoji cha Kazamoyo ambalo ndilo lililoathirika zaidi na uharibifu wa ukataji miti ovyo kutokana na kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji wa mifugo na uchomaji mkaa.

Alisema nyumba hizo zilibomolewa katika operesheni iliyofanyika mwezi Disemba mwaka jana ambapo eneo lililolengwa ilikuwa ni kitongoji cha Kazamoyo ambacho sio rasmi na hakitambuliwi na Serikali.

“Mifugo imebaki kuwa changamoto ndani msitu wa hifadhi Mgori na jeuri ya wafugaji ni kwamba wao wana nguvu ya pesa wanaweza kuwalaghai viongozi wa vijiji ili waendelee kuwepo ndani ya hifadhi hiyo,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Mulagiri, alisema kaya zaidi ya 200 ziliondolewa ndani ya hifadhi hiyo baada ya wananchi kuuziwa na viongozi wa Serikali za vijiji wasio waaminifu kwa kuwatoza fedha na kuwapa stakabadhi ambazo serikali ilikuja kubaini zilikuwa ni feki.

Mulagiri alisema baada ya kubaini hilo, serikali iliwachukulia hatua za kisheria viongozi wa Serikali za vijiji ambao walihusika na udanganyifu huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha, alisema wavamizi wa msitu huo wengi wao sio wenyeji wa vijiji vinavyouzunguka bali wanatoka mikoa jirani.