Showing posts with label ELIMU. Show all posts
Showing posts with label ELIMU. Show all posts

Wednesday, July 20, 2022

Chuo kikuu cha Arusha chawashauri vijana kusoma kozi zitakazowawezesha kujiajiri.

Chuo Kikuu cha Arusha kinachomilikiwa na kanisa la Waadventista (Wasabato)kimewashauri wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na Elimu ya  juu kusoma huku wakitambua changamoto ya ukosefu wa ajira siyo ya Tanzania pekee bali ya dunia nzima hivyo wanapswa kupata maarifa ya kujiajiri kupitia fursa za masomo wanazozipata.

Mwenyekiti wa jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Askofu Mark Malekana ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Arusha akizungumza na wanahabari kwenye banda la chuo hicho katika maonesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania Askofu Mark Malekana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye  Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa Wizara ya Elimu Sayansi na teknolojia kupitia tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es  salaam. 

"Chuo chetu kina  falsafa yakipekee katika utoaji wa Elimu, tunamtayarisha Mwanafunzi  kiroho,kisaikolojia,kiuchumi na katika nyanja zote za maisha  kwa kufanya hivyo tunategemea mhitimu hata akikosa ajira atajiajiri mwenyewe bila kutegemea kuajiriwa"amesema Askofu Malekana.

Aidha amesema kwamba kupitia maonesho hayo wameamua kuzungumzia kwa kina na wazazi au walezi wanaofika kwenye Banda la chuo hicho kwenye viwanja vya Mnazi ili kuwashauri waweze kujiunga na masomo chuoni hapo wapate maarifa mazuri yatakayoweza kuwasaidia kujiajiri.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Chuo Kikuu cha Arusha Elisha Lomay ( wa kwanza kulia) akiwa na maafisa udahili wa chuo hicho katika Banda la Maonesho la chuo hicho .
Awali Mkuu wa Kitengo Cha Masoko wa Chuo hicho  Elisha Lomay  amewambia waandishi wa habari kwamba chuo hicho kinatumia falsafa ya kumjenga mwamanafunzi akue katika maadili ya kiroho ,Kimwili, pamoja na kitaaluma ambapo wahitimu wengi wamekuwa wakifanikiwa kufanya kazi Kwa weledi mkubwa.

Amendelea kufafanua kuwa  chuo hicho ambacho kipo Wilayani Meru Mkoani Arusha kimekua kikidahili wanafunzi bure kupitia njia ya mtandao,nakwamba baada ya wanafunzi kujiunga na chuo hicho wanalipia ada ambazo Wanaweza kuzimudu ambapo zinalipwa kwa awamu.

" Chuo chetu kinatoa ufadhili( Scholarship ) Kwa wanafunzi wanaotaka kusoma nje ya nchi kwa kushirikiana na wasabato wenzetu wanaoishi nje ya nchi ikiwemo Marekani,hivyo tunawakaribisha wazazi na walezi kuwaleta watoto wao kujiunga na chuo chetu kwani kina mazingira rafiki yakujisomea na gharama za ada na malazi ni nafuu" amesema Lomay.

Aidha amesema kwamba program wanazofundisha chuoni hapo ni pamoja na  Shahada za kidini,Utawala wa Biashara na Uhasibu,Sanaa ,Ualimu  pamoja na ngazi ya cheti na Astashahada ya Elimu ya Dini(Diploma) katika nyanja mbalbali.

Monday, July 18, 2022

Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) kimekuja na mambo haya mazuri katika maonyesho ya 17 ya Vyuo vikuu.

Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizokuwa za Shahada wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha( RUCU) Dkt Wille Migodela (wakatikati) akifuatilia maelekezo yanaoyotolewa na mmoja wa maafisa wa udahili wa Chuo hicho Kwa mwanafunzi aliyetembelea banda hilo kwenye maonyesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini( TCU), yanayofanyika Viwanja vya  Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizokua za Shahada wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha( RUCU) Dkt Wille Migodela (wa kwanza kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa baadhi ya Wanafunzi waliotembelea banda la Chuo hicho kwenye maonesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) yanafofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) katika kuhakikisha kinakabiliana na changamoto zinazoikabili Jamii kimejikita kutoa Elimu kwa wanafunzi Kwa kufanya ubunifu wa tafiti mbalimbali Kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kimazingira Kama vile Mbu wanaoambukiza Ugonjwa wa Malaria.

Magonjwa Mengine ni magonjwa ya ngozi( Fangasi) na Kikohozi,ambapo wanafunzi wanafanya tafiti kupitia mimea ya asili nakutengeneza dawa ambazo zinasaidia kukabiliana na magonjwa hayo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizo za Shahada wa Chuo hicho Dakt Wille Migodela wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye maonyesho ya 17 ya Elimu y juu Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini ( TCU).

Aidha amesema kwamba chuo hicho kinatoa program za Kozi mbalimbali lakini Elimu ya utafiti wa Ubunifu imekua ikipewa kipaumbele ili kumsaidia mwanafunzi anaehitimu kuondokana na zana ya kutemea kuajiliwa na badala yake aweze kujiajiliwenyewe.

Hata hivyo amendelea kusema kwamba Wanafunzi hao wamefanikiwa kubuni kifaa kinachopima uzito wa mizigo inayobebwa na magari ambapo kifaa hicho kinafungwa kwenye gari na gari hiyo haitapita kwenye mzani Kwa ajili ya kupimwa, badala yake kifaa hicho kitaonyesha ukomo wa  uzito kamili unaohotajika kubebwa na gari hilo.

"Magari yanatumia muda mrefu kukaa kwenye foleni ya mzani kupima uzito wa mzigo,sisi kama RUCU tumekuja na suluhisho la kubuni kifaa Cha kisayansi kitakachoonyesha ukomo wa uzito wa mzigo unaotakiwa kupakiwa" amesema Dkt Migodela

Nakuongeza kuwa "kuhusu Faculty of Arts and Social  science ,tumetengeneza kifaa kinaitwa "Analogy wheel" kazi yake ni kupima umbali kwenye tambarare(horizontal distance) wakati wa kufanya Survey(upembuzi).
Kifaa kinafanya kazi mbadala wa Chain(mnyororo) ambao kwa mda mrefu umekuwa ukishindwa kutupa vipimo halisi kwasababu ya masikio(oval shape) yanayo uunganisha na pia chain inatumia mda mrefu kupima urefu ardhini.

Amesema kwamba Kwa mwaka huu wa masomo 2022/ 2023 wanatarajia kudahili  wanafunzi wapatao 1400 ambapo wanafunzi wa Cheti na Diploma ni 700 na wengine 700 ni Shahada(Digree),ambapo amesisitiza kwamba mazingira ya kujisomea Kwa wanafunzi ni mazuri.

Chuo kikuu SUZA kuja na Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Teknolojia ya Habari(IT)

Mkuu wa Kitengo Cha Uhusiano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Taifa Cha  Zanzibar( SUZA) Khadija Sadiq Mahumba ( mwenye kitambaa cheupe kichwani)akitoa maelekezo Kwa baadhi ya Wanafunzi waliotembelea Banda la chuo hicho kwenye maonyesho ya 17 ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini ( TCU) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Baadhi ya watu waliotembelea Banda la Chuo kikuu cha Tifa Zanzibar SUZA wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Maafisa Udhahili wa chuo hicho wenye Tshirt za rangi ya bluu.

Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar(SUZA) kinaendelea kuunga mkono sekta ya elimu nchini Kwa kuanzisha kozi mpya ambazo ikiwemo ya  Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Teknolojia ya Habari(IT) katika mwaka wa Masomo 2022/ 2023.

Ameyazungumza hayo Mkuu wa Kitengo Cha Uhusiano na Masoko wa SUZA Khadija Sadiq Mahumba wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Maonyesho ya 17 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia Time ya Vyuo Vikuu Nchini( TCU) Mnazi mmoja jijini Dar es salaam.  

Aidha amesema kwamba chuo hicho kinatarajia kudahili wanafunzi wapatao 2000 Kwa programu mbalimbali zikiwemo za Elimu,Afya,Kilimo kwa ngazi mbalimbali ikiwemo  Cheti,Astashahada( Diploma) Shahada(Degree),Shahada ya Uzamili na Uzamivu.

Amesema kuwa kwa mwaka huu wa masomo chuo hicho pia kinatarajia kutoa programu ya Shahada ya Uzamivu( Phd) ya Lugha ya kiswahili ,na kwamba amewaomba wanafunzi wanaotaka kujiunga na SUZA wachangamkie fursa hizo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Uhusiano na Masoko SUZA amesema kwamba Chuo hicho kinatoa programu za Kozi za Utalii ambapo wanafunzi watakaosoma kozi hizo watapata fursa ya kusoma lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo lugha ya Kireno,Kichina ,Kifaransa,Kijerumani,na kwamba chuo hicho pia kinatarajia kuanza kufundisha Programu ya lugha ya Kikorea.

Hata hivyo amebainisha kuwa wakati wa udahili wa dirisha la pili wanatarajia kudahili wanafunzi kwa program mpya za Shahada ya Uzamili ya Benki na Fedha( MSc Benking & Finance) pamoja na Shahada ya Uzamili ya  Utawala wa Fedha na Biashara ( MBA-Finance).

" Ningependa kuwaomba wazazi wawalete wanafunzi  kwenye banda letu hapa Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wajionee kozi tunazofundisha ili wafanye maamuzi sahihi yakujiunga na chuo chetu chenye fursa ya kupata ajira nje na ndani ya nchi" amesema Khadija.

Tuesday, July 12, 2022

WAZIRI MKENDA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI JENGO LA MAKTBA CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa jengo la Maktaba la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kivukoni Jijini Dar es Salaam, mradi ambao utagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 14 ili kuboresha mazingira ya Kufundishia na kujifunzia.

Jiwe la Msingi lililowekwa na Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof, Adolf Mkenda mapema leo Mkoani Dar es salaam. 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo Profesa Mkenda alisema mpango wa sasa wa Serikali katika Sekta ya Elimu ni kuzalisha wasomi watakaokuwa na Elimu ya Kujitegemea kwa kuboresha mitaala ambayo mpaka sasa zaidi ya wadau laki moja wamekwisha toa maoni yao.

Prof. Mkenda amesema ubora wa Elimu ni ajenda ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambayo inahitaji mageuzi ili kuongeza ubora na iakisi mahitaji ya nchi, utandawazi kwa lengo la kuongeza uwekezaji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Maiko amekipongeza Chuo hicho kwa kutenga bajeti kiasi cha asilimia arobaini ambazo ni  fedha za ndani kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.

“Hiki kilichofanywa na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinatakiwa kiwe mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine ili kuwezesha Serikali kuendelea kutumia bajeti zinazotengwa kwa lengo la kuboresha zaidi Miundombinu ya Kufundishia na kujifunzia,”alisisitiza Prof Mkenda.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema ujenzi wa jengo hilo utakuwa na Maktaba, Ukumbi wa Mihadhara pamoja na ofisi za wafanyakazi.

“Tumekusanyika leo hapa kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa jengo la Maktaba lenye uwezo kuchukua wanafunzi 2500, Ukumbi wa Mihadhara wa kutosha Wanafunzi 1000 pamoja na ofisi za Wafanyakazi,”alisema Prof. Mwakalila.

Aidha Mchakato wa Mradi huo waa Maendeleo ulianza katika bajeti yam waka 2018/2019, hata hivyo pamoja na kutengewa bajeti ya Maendeleo lakini fedha za miradi ya Maendeleo hazikutolewa hivyo katika bajeti yam waka 2021 Chuo kiliamua kutenga bajeti ya asilimia 40 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Prof. Mwakalila aliitaja miradi mimngine inayosimamiwa na Chuo hicho kuwa ni mradi wa ujenzi wa jengo la hosteli ya Wanafunzi katika Kampasi ya karume Zanzibar lenye uwezo wa kulaza Wanafunzi 1536 ulioanza Julai 18, 2021 na utagharimu zaidi ya bilioni 15.

Msimamizi wa mradi huo kutoka Wizara ya Ujenzi  Mhandisi Mwesigwa Ichwekeleza alisema mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 5 na utakuwa ni wa ghorofa 3 ambao utakamilika ndani muda wa miezi 30 kama ilivyopangwa.

                                                               Habari Picha..

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiongea na Wanafunzi Pamoja na Wageni mbalimbali waliyofika kushuhudia Zoezi la Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba na Kumbi za Midahalo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere leo Mkoani Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Maiko Akiongea mbele ya Wageni mbalimbali waliyofika kushuhudia Zoezi la Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba na Kumbi za Midahalo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere leo Mkoani Dar es salaam.
Waziri Mstaafu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mh. Stephen Wasira akiongea na Wageni katika tafrija ya uwekaji jiwe la Msingi Chuoni hapo, mapema leo Mkoani Dar es slaam.
Mkuu wa Chou cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Makalila, akiongea na Wanafunzi Pamoja na Wageni mbalimbali waliyofika kushuhudia zoezi la Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba na Kumbi za Midahalo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mapema leo Mkoani Dar es salaam.
Meza kuu ikipatiwa maelezo ya picha na Mkandarasi namna jengo litakavyokuwa baada ya kukamilika.
Zoezi la Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba na Kumbi za Midahalo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere likiendelea leo Mkoani Dar es salaam.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia matukio katika zoezi la Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Maktaba na Kumbi za Midahalo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere leo Mkoani Dar es salaam.


Monday, July 11, 2022

Prof. MKENDA: WAOMBAJI MIKOPO 2022-2023 SOMENI MWONGOZO.

 Waziri wa ElLmu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi HESLB, Prof. Hamisi Dihenga. Hafla hiyo imefanyika leo Jumanne Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta (TPC), Macrice Mbodo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Angela Anatory akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Prof. Hamisi Dihenga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHELB) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uombaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka wa masomo 2022/2023. Hafla hiyo imefanyika leo Julai 12, 2022 Jijini Dar es Salaam.

(PICHA NA HESLB)

******************************

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa 2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi.

Prof. Mkenda ameyasema hayo katika hafla fupi ya kuzindua mwongozo huo iliyofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB Prof. Hamisi Dihenga na wadau wengine wa HESLB.

Prof. Mkenda amesema: “Kuanzia leo (Jumanne, Julai 12), mwongozo huu utapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na ya Wizara (www.moe.go.tz) katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza … na kuwapa fursa waombaji kuusoma.  Dirisha la kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 hadi Septemba 30, 2022,” amesema na kuongeza:

“Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 litakuwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, hivyo tunawasihi wanafunzi waombaji wasome mwongozo kabla ya kuomba mkopo kwa kuwa ndiyo unataja sifa, vigezo na utaratibu wa kuomba mkopo,” amesema Prof. Mkenda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe amewakumbusha waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyomo kwenye mwongozo ili kuondokana na changamoto ambazo hujitokeza kwa waombaji.

“Uzoefu unaonesha kuwa wanafunzi waombaji wamekuwa hawazingatii taratibu wakati wa kufanya maombi. Tunawasii mzingatie maelekezo ya mwongozo. Wakati wa dirisha la maombi kumekuwepo na changamoto nyingi zinazojitokeza kwa waombaji”, amesema Prof. Mdoe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kila mwaka mwezi Julai, HESLB huanza kupokea maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo unaofuata ambapo mwongozo huo hutoa maelezo ya kina kuhusu sifa na utaratibu wa kupanga mikopo kwa mwaka husika.

“Mwongozo huo umekamilika na kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi. Kuanzia wiki ijayo, tutaanza kuendesha programu za elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, mikutano katika Kambi za JKT na mitandao ya kijamii” amesema Badru.

Katika mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha TZS 573 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na skolashipu kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.