Showing posts with label MICHEZO. Show all posts
Showing posts with label MICHEZO. Show all posts

Thursday, April 26, 2018

TIGO YAZINDUA PROMOSHENI YA ‘JIGIFTISHE’ AMBAPO SHILINGI MILIONI 600 ZITATOLEWA KWA WATEJA NA KUWAFANYA MAMILIONEA MSIMU HUU WA SIKUKUU

Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed (kushoto), Meneja Uhusiano wa Tigo Woinde Shisael (kati) pamoja na Balozi wa promosheni ya Tigo Jigiftishe, Lucas Mkenda almaarufu Joti (kulia) wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa promosheni ya Jigiftishe itakayowapa wateja wote watakaotumia huduma za Tigo katika msimu wa sikukuu fursa ya kushindania jumla ya shilingi 600 milioni. 
Mkuu wa Masoko wa Tigo, Tarik Boudiaf (kushoto), Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed (wa pili kushoto), Balozi waTigo Lucas Mkenda almaarufu Joti (katikati), Meneja Mawasiliano Woinde Shisael (wa pili kulia) pamoa na Mkuu wa Bidhaa za Tigo Pesa, James Sumari (kulia) wakizindua promosheni ya Jigiftishe itakayowapa wateja wa Tigo fursa ya kushinda hadi TSH 50 milioni katika msimu huu wa sikukuu.

Wateja watakaoongeza salio au kuweka Pesa Kwenye Tigo Pesa au Kutumia huduma yoyote ya Tigo watapata nafasi ya kushinda zawadi nono za hadi TSH milioni 50!  
Dar es Salaam, 15 Novemba 2018; Tigo Tanzania - kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali, itawezesha wateja wake kuwa mamilionea baada ya kuzindua promosheni kubwa zaidi itakayogawa kiasi cha TSH milioni 600 katika msimu huu wa sikukuu.

Promosheni hiyo ya kipekee ya ‘JIGIFTISHE’ kutoka Tigo katika msimu huu wa Krismasi na Mwaka Mpya itawafanya zaidi ya wateja 450 kuwa mamilionea ndani ya siku 45, kutokana na kutumia huduma za Tigo pekee. Ni rahisi na hakuna kujiunga kwenye promosheni hii.

‘Wateja wa Tigo watakaoweka pesa kwenye akaunti zao za Tigo Pesa, kuongeza salio au kununua simu janja kwenye maduka yote ya Tigo au kutumia huduma zozote za Tigo katika kipindi hiki cha sikukuu watapata fursa ya kujishindia TSH milioni 1 kila siku au TSH milioni 10 kila wiki. Pia kutakuwa na zawadi kubwa za TSH milioni 15, TSH milioni 25 au TSH milioni 50 zitakazotolewa mwishoni mwa promosheni hii ya JIGIFTISHE!’ Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.

Akibainisha vigezo vya ushiriki katika promosheni hiyo ya JIGIFTISHE, James Sumari, Mkuu wa Bidhaa za Huduma za Tigo Pesa wa Tigo alisema kuwa ili kupata fursa ya kushinda, wateja wa Tigo wanahitaji kununua kifurushi chochote kwa njia yoyote (ikiwemo kupitia *147*00#, *148*00# au kuongeza muda wa maongezi kwa njia ya kielektroniki, kadi au kupitia Tigo Pesa) au kufanya miamala ya Tigo Pesa kupitia *150*01# katika msimu huu wa sikukuu.

‘‘Ni rahisi sana! Hakuna kufanya kitu chochote maalum ili uweze kushinda. Unachohitaji kufanya ni kuendelea kutumia huduma au kununua bidhaa za Tigo ili upate nafasi ya kuwa milionea!” Woinde alisisitiza.

Kila muamala utakaofanyika utampa mteja nafasi moja ya kushiriki katika droo, na wateja wanaweza kutazama nafasi zao za kushinda kwa kupiga *149*22#. Kadri unavyofanya miamala zaidi ndivyo unavyojiongezea nafasi za kushinda.

Promosheni hii ya JIGIFTISHE itakayojaza mifuko ya wateja na manoti na kubadilisha maisha yao  inathibitisha kuwa Tigo ndio mtandao unaotoa huduma bora zaidi za kidigitali kwa wateja wake na kuwawezesha kufurahia msimu huu wa sikukuuu huku wakimaliza au kuanza mwaka mpya kwa mtindo tofauti.

‘Hii ndio njia yetu ya kuwashukuru wateja wetu wote kwa kuendelea kutumia huduma zetu bora, zenye kasi ya juu na rahisi. Tunachukua fursa hii kuongeza tabasamu katika nyuso za wateja wetu,’ Woinde alisema.
Tayari wateja wa Tigo wanafurahia unafuu na urahisi wa kutumia huduma bunifu za Tigo kama vile kufanya miamala ya Tigo Pesa (kutuma na kupokea pesa ikiwemo kutoka mitandao mingine na benki), kulipia huduma mbali mbali kama vile LUKU, kufanya manunuzi kutoka kwa wafanyabiashara tofauti, kukamilisha malipo ya Kiserikali na pia kufurahia huduma bora za maisha ya kidigitali kwenye mtandao mkubwa zaidi wa 4G nchini. 

Wednesday, April 18, 2018

SOMA HAPA KUJUA FAINALI YA KOMBE LA AZAM ITACHEZWA LINI NA WAPI..

Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inatarajia kuchezwa Juni 2,2018 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid,Arusha.
Katika mashindano ya ASFC mwaka huu kumefanyika maboresho ya kuongeza zawadi ambapo awali mshindi wa pili alikuwa hapati zawadi na katika msimu huu wa mashindano hayo mshindi wa pili atajikusanyia kiasi cha shilingi Milioni Kumi huku bingwa akibeba kitita cha shilingi Milioni Hamsini.

Zawadi nyingine zitakazotolewa ni pamoja na Mchezaji bora wa mashindano atakayezawadiwa shilingi milioni Moja,Kipa Bora atapata shilingi Milioni Moja huku mfungaji Bora pia akipata shilingi Milioni Moja wakati mchezaji Bora wa mchezo wa fainali akijizolea shilingi Laki Tano.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF

QNET INASHEREHEKEA ARI YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI KWA KULETA FARAJA KWA WENYE UHITAJI NA KUSAIDIA JAMII AFRIKA IKIWEMO TANZANIA

Watoto wa vituo mbalimbali kumi vya kulelea watoto wenye uhitaji mkoani Dodoma, wakipata futari iliyoandaliwa na Kampuni ya QNET jana. Hafla hiyo ilihudhuriwa na zaidi ya watoto 200 kutoka vituo hivyo na kuongozwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma , Mustapha Shaaban, Wawakilishi wa QNET na wawakilishi toka Bakwata.

Watoto kutoka vituo mbalimbali kumi vya kulelea watoto wenye uhitaji mkoani Dodoma wakisherehekea na  Mshauri wa QNET Tanzania, Edward Mkony




    
QNET INAUNGANA NA YATIMA JIJINI DODOMA KWA KUANDAA FUTARI KWA ZAIDI YA WATU 200

Tarehe 2 June 2019..... Dodoma. QNET, kampuni ya biashara ya mtandao duniani, sambamba na tamaduni zake na jitihada za kusaidia jamii, kusambaza upendo, huruma na ukaribu kwa kutoa msaada na kuleta faraja kwa jamii nyingi zisizo na uwezo barani Afrika. Katika zoezi ambalo lilifanyika katika nchi zote ambako kampuni hii inaendesha shughuli zake barani Afrika, QNET sambamba na wawakilishi wake wa kujitegemea (IRs), mawakala na wafanyakazi imeleta faraja, tumaini na tabasamu kwenye nyuso za wengi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kampuni ya QNET inaendeshwa na falsafa ya RYTHM - Jiinue Kusaidia Wanadamu ('Raise Yourself to Help Mankind’) imeandaa kampeni hii ya mwaka kusaidia kuboresha maisha ya familia na watoto wengi wasio na uwezo kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama vile chakula, vinywaji na msaada wa kifedha kwa madhumuni ya elimu na  kibinadamu. 
Hafla ya Futari Jijini Dodoma imewaleta pamoja zaidi ya watoto yatima 200 kutoka katika wilaya kumi za mkoa huo. Pamoja na hafla hiyo ya Iftar kampuni ya QNET imetoa zawadi za mbuzi, kilo 100 za mchele, kilo 50 za unga, kilo 25 za maharage, kilo 25 za sukari na lita 20 za mafuta ya kula kwa kila vituo kumi vya watoto yatima mkoani humo.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Shaaban alitoa wito wa amani na kuihamasisha jamii kuiga mfano uliofanywa na QNET katika kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani. Sheikh Shaaban ameipongeza kampuni ya QNET kwa kutayarisha Iftar kwa vituo vya watoto yatima Jijini Dodoma, chaguo ambayo inaunga mkono mkakati wa serikali ya kuhamisha makao yake Jijini humo. Pia alishukuru kampuni ya QNET kwa moyo wa msaada na ushirikiano hasa katika mwezi  huu wa Ramadhan.
Akiongea katika hafla hiyo, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Mwanahamisi Mukunda alisema ‘Tendo hili la Iftar imesaidia serikali ya mkoa katika utekelezaji wa majukuku yake pamoja na kuwaangalia watoto yatima’.
Hafla ya Iftar Jijini Dodoma iliudhuriwa  pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma, wawakilishi wa baraza la kislamu Tanzania-BAKWATA, viongozi wa dini la kislamu wa mkoa pamoja na wawakilishi wa kampuni ya QNET.
Katika nchi za Senegali, Cameroon, Kenya, Niger, Mali, Burkina Faso, Togo, Guinea, Ivory Coast na Ghana, QNET imetoa magunia ya mchele, magaloni ya mafuta ya mboga, vinywaji baridi, vifaa vya usafi na fedha taslimu kwa yatima, jamii za waisiliamu, vituo vya kutoa msaada wa kielimu na ofisi ya misaada ya Imamu mkuu.
Biram Fall, Meneja Mkuu wa QNET Kanda ya Afrika chini ya jangwa la Sahara, wakati akitoa maoni kuhusu CSR ya Ramadhani ya QNET kwa  mwaka huu, alisema:
 "QNET imekuwa ikifanya hivi kwa miaka mingi. Kampeni ya kutoa msaada katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan ni moja ya njia tunazotumia kuzifikia jamii kusaidia watu. Kadri tunavyoendelea katika biashara yetu, tunaamini katika kusambaza faraja na utoshelevu unaokuja pamoja nao. Kwa kweli ni muhimu sana, inatia moyo na inakamilisha jitihada za QNET. Inawezesha watu, inaonyesha upendo kwa jamii na pia inahamasisha wafanyakazi wetu na Wawakilishi wetu wa Kujitegemea (IRs), kadri wanavyoshiriki wao binafsi katika kuboresha maisha ya wengine.  Malengo yetu ya kibiashara pia ni kuhusu kutengeneza fursa kwa watu, kufanya maisha ya watu kuwa bora na kuwawezesha watu kuwasaidia waweze kuishi maisha ya ukamilifu.   Tunaita hiyo kuwa ni kuishi kikamilifu"
Mwaka jana, Kituo cha Uwajibikaji wa Mashirika kwa jamii cha Afrika ya Kusini kiliitunukia QNET kuwa kampuni bora ya mwaka ya kimtandao ya uwajibikaji kwa jamii (E-Commerce CSR Company of the Year) kwa uwajibikaji wake katika kusaidia jamii na kuleta mabadiliko bora.

Tuesday, April 17, 2018

QNET yatoa fursa ya ‘kufanya kazi kwa bidii na kuleta mabadiliko chanya’

Meneja wa QNET, kanda kusini ya Afrika  Biram Fall (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa maonesho ya bidhaa za QNET 2019 jijini Dar Es Salaam jana. Wengine kwenye picha  ni  Mkuu wa Elimu ya Mtandaoni wa QNET Bernie Gaksh (kushoto) na Mshauri wa Biashara wa QNET Tanzania, Edward Mkony

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Paul Makonda akizungumza na wawakilishi, wafanyakazi na waalikwa  wa QNET kuhusu maadili ya kazi kwenye uzinduzi wa maonesho ya bidhaa za QNET jijini Dar Es Salaam jana.

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Paul Makonda (katikati) na Meneja wa QNET, kanda kusini ya Afrika  Biram Fall (kushoto) wakikata utepe kuzindua rasmi maonesho ya bidhaa za QNET 2019 jijini humo.  Kulia ni Mshauri wa Biashara wa QNET Tanzania, Edward Mkony.


·        Maelfu wa hudhuria maonyesho ya QNET  Dar es salaam
·        Watanzania kunufaika na bidhaa mbalimbali pamoja na fursa za biashara
Tarehe 16 Machi 2019, Dar es Salaam: Kampuni yenye asili ya Asia ya mauzo ya moja kwa moja QNET imeendesha maonyesho ya bidhaa na huduma zake jijini Dar es salaam siku ya tarehe 16 na 17 Machi 2019. 
Maonyesho yenye jina la Absolute Living, (Kuishi kikamilifu) sambamba na falsafa ya bidhaa za kampuni ya mauzo ya moja kwa moja, huwa yanafanyika kila mwaka katika nchi mbalimbali duniani kote ikiwa na lengo la kuonyesha bidhaa zake na huduma kwenye masoko mapya.  Onyesho hilo pia ilikuwa kama jukwaa kwa wateja na wadau wengine wanaotaka kufahamu kuhusu QNET na mtindo wake wa biashara. 

Nadharia ya Absolute Living (Kuishi kikamilifu) inaakisi juhudi za QNET za kukuza mwendendo wa kujali afya, mtindo wa maisha wenye uwiano sahihi, ikiwa inatilia mkazo katika Afya, ustawi na elimu.
 
Mgeni rasmi katika hfla hiyo, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda alisema ‘Maisha yangu ni mfano wa kufanya kazi kwa bidi na kujiamini katika kitu chochote unachokifanya. Hii ndiyo njia pekee yakuleta mabadiliko na maendeleo kwa mtu, familia na jamii”.

Akizungumza kwenye mkutano na vyombo vya habari Meneja Mkuu wa QNET kwa Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika, Biram Fall alisema kwamba, "Tunatoa aina mbalimbali za bidhaa za kiwango cha juu na huduma kwa wateja wetu kuwasaidia waweze kuishi maisha yenye uwiano sahihi, na pia kutatua tatizo la msingi kama vile elimu, ufahamu, na maendeleo binafsi kupitia program za mafunzo yetu, ambayo yanawasaidia katika safari yao ya kujiajiri mwenyewe.  Kutoka katika kozi za elimu kwa njia ya mtandao kama vile SELI/qLearn, mpaka katika vifurushi vya sikukuu kama vile Tripsavr, mpaka bidhaa za kuongeza nguvu kama vile Bio Disc3, virutubisho kama EDGE, na saa za mkononi kama Bernhard H. Mayer, QNET ina aina mbalimbali za kukidhi mahitaji mbalimbali ya watu.  Katika kitovu cha yote haya, ni hamu yetu ya kutoa fursa ya Kuishi Kikamilifu "Absolute Living”

Zaidi ya watu elfu mbili walipata fursa ya kuona bidhaa za mfano katika onyesho hilo na kufundishwa namna ya matumizi ya bidhaa na faida zake kwa wateja na watumizji wa mwisho.  Kwa kuongezea, wataalamu wa bidhaa na biashara walikuwepo kwaajili ya kujibu swali lolote kutoka kwa wageni ili kuelewa vizuri ulimwengu wa QNET.

Maonyesho ya Dar es salaam yanafuata mfululizo wa maonyesho kama hayo yaliyofanikiwa nchini Togo, Guinea, Ivory Coast, Senegali, Burkina Faso na Cameroon mwaka jana.
Msafara wa maonyesho utasisimama katika mji wa Kumasi, Ghana, baada ya Dar es salaam kuanzia tarehe 23 mpaka 24 Machi mwaka 2019.

Sunday, April 15, 2018

TIGO FIESTA 2018 – VIBE KAMA LOTE KURINDIMA MOROGORO


Msanii wa  bongo flava Boniventure Kabogo – Stamina (aliyesimama) akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote mjini Morogoro leo. Tigo imetangaza punguzo la bei kwa tiketi zitakazonunuliwa kupitia Tigo Pesa Masterpass QR pamoja na kuzindua shindano la Tigo Fiesta 2018 Chemsha Bongo. Pamoja naye ni (kuanzia kushoto), Mtangazaji wa kituo cha Clouds FM Gardner Habash, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Morogoro, Stephen Kunambi, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Tigo – William Mpinga, Afisa Michezo wa Manispaa ya Morogoro - Asteria Mwang’ombe , msanii wa bongo flava Abednego Daniel – Belle 9, na mtangazi wa Clouds FM Kenneth Frank – Kennedy the Remedy.

Wasanii wa Bongo Flava (kuanzia kushoto) Z Anto, Mr Blue Kabayser na Ben Pol wakisalimiana wakati wa hafla ya uzinduzi wa  uzinduzi wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote mjini Morogoro leo. Tigo imetangaza punguzo la bei kwa tiketi zitakazonunuliwa kupitia Tigo Pesa Masterpass QR pamoja na kuzindua shindano la Tigo Fiesta 2018 Chemsha Bongo. Tamasha la kwanza la msimu huu wa Tigo Fiesta 2018l inatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro siku ya Jumamosi. 
Punguzo kabambe la bei ya tiketi kwa watakaonunua kupitia Tigo Pesa Masterpass QR

Morogoro, Septemba 28, 2018 - Huku nchi nzima ikisubiri kwa hamu kuanza kwa msimu wa Tigo Fiesta 2018- Vibe Kama Lote, mdhamini mkuu Tigo Tanzania pamoja na waandaaji Clouds Media Group wameanza maandalizi rasmi ya tamasha hilo litakalorindima Jumamosi hii tarehe 29 Septemba katika viwanja vya Jamhuri, mjini Morogoro..

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Tigo Fiesta 2018 – Viba Kama Lote, Gardner G. Habash aliwahakikishia wote watakaohudhuria tamasha hilo usalama na mapokezi mazuri. ‘Tunawakaribisha nyote kwenye shamrashamra za mwanzo wa msimu wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote,’ Gardner alisema.  

‘Tigo inatoa punguzo kubwa la bei kwa tiketi za tamasha la Tigo Fiesta 2018 zitakazonunuliwa kupitia Tigo Pesa Masterpass QR. Kwa Morogoro, tiketi zitakazonunuliwa kwa mfumo wa Tigo Pesa Masterpass QR zitagharimu TSH 5,000 pekee badala ya TSH 7,000 kwa watakaonunua kwa pesa taslim,’ Mkuu wa Huduma za Masoko wa Tigo, William Mpinga alisema. Wateja wanapaswa kupiga *150*01#  na kuchagua 5 (lipia huduma) kisha kuchagua namba 2 (lipa Masterpass QR) na kutuma kiasi husika kwenda namba ya Tigo Fiesta 78888888.

Wateja wa Tigo pia watapata faida zaidi kupitia shindano la Tigo Fiesta 2018 – Chemsha Bongo Trivia linalotoa zawadi za kila siku za TSH 100,000, zawadi za kila wiki za TSH 1 milioni, simu janja za mkononi zenye thamani ya TSH 500,000 kila moja, pamoja na donge nono la TSH milioni 10 kwa mshindi wa jumla. Kushiriki wateja wanapaswa kutuma neno MUZIKI kwenda 15571 au kutembelea tovuti ya  http://tigofiesta.co.tz na kuchagua Trivia.

‘Katika miaka ya hivi karibuni, tumetambua mchango mkubwa wa kiuchumi na kijamii unaotokana na tamasha la Tigo Fiesta. Bali na kutoa fursa ya kuutangaza mkoa husika, pia inaongeza idadi ya wageni na kusababisha ongezeko kubwa la fursa za biashara kwa wamiliki wa hoteli, migahawa, mama nitilie, vyombo vya usafiri kama vile bodaboda, kumbi za starehe na biashara nyinginezo,’ Gardner aliongeza.

Huu ni mwaka wa 17 wa tamasha la muziki na kitamaduni la Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote ambapo mwaka huu litashirikisha 100% wasanii wa nyumbani watakaozuru mikoa 15 ya nchi ikiwemo; Morogoro, Sumbawanga, Iringa, Singida, Songea, Mtwara, Moshi, Tanga, Muleba, Kahama, Mwanza, Musoma, Arusha na Dodoma, huku kilele kikifanyika Dar es Salaam

Friday, April 13, 2018

Vibe la Tigo Fiesta lapagawisha Sumbawanga

 Wakazi wa manispaa ya Sumbawanga na vitongoji vyake usiku wa kuamkia leo walipata burudani ya aina yake ya msimu wa tamasha kubwa nchini la Tigo Fiesta Vibe Kama Lote.
Hili ni tamasha la pili kwa mkoa huo baada ya ufunguzi uliofanyika mkoa wa Morogoro.
Msimu huu si kwa burudani tu, bali huwa na fursa mbalimbali kwa wafanyabiasha na waendesha bodaboda.
Kwenye steji ndio kunaacha gumzo kwa wakazi wa miji mbalimbali ambapo tamasha linafanyika.
Akifungua pazia la tamasha hili msanii Nedy Music alianza kuwapasha joto mashabiki akifuatiwa na msanii WhoZu ambaye aliwapagawisha kwa kibao chake kiitwacho "uendi mbiguni".

Msanii mkongwe Farid Kubanda Fid Q nae alichota hisia za mashabiki kwa kushusha nyimbo zake tofauti tofauti ukiwemo Fresh.
Ben Pol ambaye miaka yote huwa mbunifu kwenye jukwaa, alipanda na wenyeji 6 wa mji huo kwa kuonyesha namna ya wakaazi wa Sumbawanga wanaishi katika mazingira tofauti kulingana na anachofanya kwa siku.

Kwa upande wa mdhamini mkuu wa Tigo Fiesta 2018, Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini, Henry Kinabo alisema msimu kampuni ya Tigo imekuja ofa kabambe kwa wateja wao. " Huu ni msimu wa aina yake kama utannunua tiketi kwa Tigo Pesa Master Pass QR utaweza kupata tiketi kwa shilingi elfu tano ambapo ukinunua kawaida unapata kwa elfu saba, kadhalika wateja wa Tigo waingia kwenye shindano la Tigo Fiesta 2018 Chemsha Bongo Trivia, ambapo zawadi za kila siku za shilingi laki moja na za will za milioni 1 utolewa. Pia wateja wa Tigo wataweza kufutahi Huduma ya intaneti kupitia promosheni ya Data Kama Lota kwa kununua kifurushi na kupata mara mbili ya ulichonunua kupitia menu ya *147*00#.

Kesho jumapili Vibe la Tigo Fiesta litahamia mkoani Iringa kwenye uwanja wa Samora na itapandisha wasanii akiwemo Fid Q, Ben Pol,Maua Sama, WhoZu, Marioo, Nandy, Chege,Barnaba, Billinas, Weusi na wengine wengi.

Tuesday, April 10, 2018

MICHUANO YA COPA COCA-COLA UMISSETA YAPOKELEWA KWA SHANGWE MKOANI TANGA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella akipokea zawadi ya mpira kutoka kwa Meneja wa chapa ya Coca-Cola nchini, Sialouise Shayo
 Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella akipiga danadana katika uzinduzi huo
 Wanafunzi wakipokea vifaa vya michezo. Wanafunzi wakichuana katika mchezo wa soka siku ya uzinduzi.
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali wakifuatilia matukio ya uzinduzi.

Na Mwandishi Wetu. 
Mashindano ya shule za sekondari ya Copa Umisseta yanayoendelea ngazi ya mikoa, yamezinduliwa mkoani Tanga, katika uwanja wa Mkwakwani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali , wadau wa michezo na mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella. 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye alimwakilisha Waziri wa TAMISEMI, aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kutoa udhamini wa mashindano ya ngazi za chini na aliipongeza kampuni ya Coca-Cola kwa kudhamini mashindano haya na kuahidi kuwa serikali itafanya kila jitihada kuunga mkono jitihada za kufufua michezo ya mashuleni ili kuhakikisha inashirikisha wanafunzi wengi. 

 “Serikali itahakikisha inajenga miundombinu ya michezo sambamba na kuhakikisha walimu wanapatiwa mafunzo ya taaluma ya michezo,pia tutahakikisha ratiba za vipindi vya michezo mashuleni zinafuatwa badala ya kutumia muda wa vipindi hivyo kufundisha masomo mengine”Alisema Shigella. 

Kwa upande wake Meneja wa chapa ya Coca-Cola nchini, , Sialouise Shayo alisema kampuni ya Coca-Cola kupitia udhamini wake inahakikisha wanafunzi wanaoshiriki mashindano haya wanapatiwa vifaa vya michezo. 

 “Kampuni ya Coca-Cola imekuwa ikidhamini mashindano haya ya Copa Umisseta kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, lengo letu kubwa ni kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya chini, tunaamini kuwa michezo mbali na kujenga afya pia ina fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi”alisema Shayo.

Kampuni ya Coca-Cola inatarajia kutoa vifaa vya michezo kwa shule za sekondari 4,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Uzinduzi wa mashindano haya mkoani Tanga ni wa pili kufanyika baada ya kuzinduliwa mkoani Dodoma na unatarajiwa kufanyika katika mikoa mingine sita nchini kabla ya kufanyika katika ngazi ya Taifa mwezi Juni mwaka huu mkoani Tanga.

Thursday, April 5, 2018

TIGO FIESTA 2018 – VIBE KAMA LOTE YAJA NA PROMOSHENI YA DATA KAMA LOTE

Mkuu wa Huduma na Bidhaa wa Tigo, David Umoh (kulia) akizungumza na waandishi wa Habari leo  katika uzinduzi wa promosheni ya Data Kama Lote inayowapa wateja bonasi ya hadi mara mbili kwa vifurushi vya intaneti watakavyonunua kupitia menu iliyoboreshwa ya Tigo *147*00#, katika msimu huu wa Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote. Kulia ni Mkuu wa Huduma za Masoko wa Tigo, William Mpinga

Mkuu wa Huduma za Masoko wa Tigo, William Mpinga  (kulia) akizungumza na waandishi wa Habari leo  katika uzinduzi wa promosheni ya Data Kama Lote inayowapa wateja bonasi ya hadi mara mbili kwa vifurushi vya intaneti watakavyonunua kupitia menu iliyoboreshwa ya Tigo *147*00#, katika msimu huu wa Tigo Fiesta 2018 - Vibe Kama Lote. Kushoto ni Mkuu wa Huduma na Bidhaa wa Tigo, David Umoh


Kwa mara ya kwanza msimu wa Tigo Fiesta 2018 waja na promosheni murwa inayompa mteja bonasi la uhakika lenye  thamani ya hadi mara mbili ya kifurushi cha intaneti papo kwa hapo.

Kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali, Tigo Tanzania leo imetangaza promosheni murwa kwa wateja wote watakaonunua vifurushi vya intaneti kupitia menu iliyoboreshwa ya *147*00#. Mteja atapokea bonasi la uhakika papo kwa hapo lenye thamani hadi mara mbili ya kifurushi cha intaneti atakachonunua katika msimu huu wa Tigo Fiesta 2018.
Akitangaza promosheni hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Bidhaa na Huduma wa Tigo, David Umoh alisema, “Kuendana na msimu wa Tigo Fiesta 2018 – Vibe Kama Lote, promosheni hii ya Data Kama Lote itahakikisha kuwa wateja wote wa Tigo wanafurahia maisha ya kipekee ya kidigitali huku wakisambaza matukio ya Tigo Fiesta 2018 mubashara kutoka sehemu yoyote ile ya nchi kupitia mtandao wenye kasi ya juu zaidi wa 4G+.”

Hali kadhalika, Tigo inatoa punguzo kubwa la bei kwa tiketi za tamasha la Tigo Fiesta 2018 zitakazonunuliwa kupitia Tigo Pesa Masterpass QR. Katika mikoa yote ya Tigo Fiesta 2018, wateja wanapaswa kupiga *150*01#  na kuchagua 5 (lipia huduma) kisha kuchagua namba 2 (lipa Masterpass QR) na kutuma kiasi husika cha bei ya tiketi kwenda namba ya Tigo Fiesta 78888888.

Wateja wa Tigo pia watapata faida zaidi kupitia shindano la Tigo Fiesta 2018 – Chemsha Bongo Trivia linalotoa zawadi za kila siku za TSH 100,000, zawadi za kila wiki za TSH 1 milioni, simu janja za mkononi zenye thamani ya TSH 500,000 kila moja, pamoja na donge nono la TSH milioni 10 kwa mshindi wa jumla. Kushiriki wateja wanapaswa kutuma neno MUZIKI kwenda 15571 au kutembelea tovuti ya  http://tigofiesta.co.tz na kuchagua Trivia.

Tigo ni mtandao unaojulikana kwa promosheni kabambe na ubunifu wa kipekee unaoendana na mahitaji halisi ya soko, hivyo kuifanya Tigo kuwa mtandao unaowaelewa wateja wake zaidi.  

Kwa hiyo tumejizatiti kuwapa wateja wetu promosheni bora zaidi katika msimu huu wa Tigo Fiesta 2018. Tunawakaribisha wateja wetu kufurahia ofa hizi murwa.

Tuesday, March 27, 2018

MICHUANO YA COPA COCA-COLA UMISSETA 2018 YAZINDULIWA MKOANI DODOMA

Waziri Jafo akigawa zawadi ya mipira kwa baadhi ya shule za sekondari zitakazoshiriki. Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo akihutubia wakati wa uzinduzi huo.
Meneja wa chapa ya Coca-Cola, Sialouise Shayo, akiongea wakati wa uzinduzi huo. Waziri Jafo akikagua moja ya timu na kugawa vifaa kwa baadhi ya shule za sekondari
Waziri Jafo katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa UMISSETA baada ya uzinduzi.
Wakazi wa Dodoma walijitokeza kushuhudia uzinduzi.

Mashindano ya shule za sekondari ya UMISSETA ngazi ya mkoa yamezinduliwa mkoani Dodoma, na mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa ni Waziri wa TAMISEMI,Selemani Jafo.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wanafunzi wa shule za sekondari,walimu, viongozi mbalimbali wa mkoa na michezo.

Mbali na uzinduzi,Waziri alikabidhi vifaa vya michezo kwa timu za sekondari zilizokuwepo kwenye uzinduzi huo.Vifaa hivyo vya michezo vimetolewa na kampuni ya Coca-Cola ambayo ni mdhamini mkuu wa mashindano haya,ambapo mwaka huu imepanga kutoa vifaa vya michezo kwa shule 4,000 za sekondari zilizopo sehemu mbalimbali nchini.

Waziri Jafo, alisema kampuni ya Coca-Cola kwa kudhamini mashindano hayo kutafanikisha jitihada za kuendelea kuibua vipaji vya wachezaji chipukizi wa michezo ya soka ,mpira wa kikapu na pia kupitia mashindano haya kutaibuliwa vipaji vya wanariadha watakaotamba katika kipindi cha miaka ijayo. 

 “Nafahamu kuwa udhamini wa Coca-Cola wa mashindano haya unamalizika mwishoni mwa mwaka huu,lakini natoa ombi maalum iangalie uwezekano wa kuendelea kuongeza kipindi cha kutoa udhamini .

Mashindano haya ya UMISSETA ni tanuru ya kuibua vipaji na rekondi ipo ya wachezaji wazuri wa soka waliofanya vizuri na wanaoendelea kufanya vizuri katika michezo mbalimbali,vipaji vyao viliibuliwa katika mashindano haya wengi pia wamechezea baadhi ya klabu kubwa za soka za Yanga na Simba”alisema. 

Waziri Jafo,alitoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza kudhamini mashindano ya michezo kuanzia ngazi za chini,na kusisitiza kuwa sekta ya michezo inazidi kukua ambapo hivi sasa lengo lake sio burudani bali ni biashara kubwa na ushahidi wa suala hili upo wazi. 

Jafo pia alishauri kamati ya maandalizi ya mashindano haya ya UMISSETA ,kwa miaka ijayo ihakikishe uzinduzi wake ngazi ya kitaifa unafanyika mkoani odoma badala ya mkoani Mwanza ili yaendane na mkakati wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kuhamishia shughuli za serikali katika mji wa makao makuu ya nchi. 

Kwa upande wake Meneja wa chapa ya Coca-Cola, Sialouise Shayo,alisema kampuni ya Coca-Cola inajivunia kuwa mdhamini wa mashindano haya kwa kipindi cha miaka 3 mfulilizo na inaamini vipaji vingi vimeibuliwa na vitaendelea kuibuliwa .

”Udhamini wetu katika mashindano haya tumejikita katika kutoa vifaa vya michezo kwa wachezaji wanaoshiriki kuanzia ngazi ya mkoa hadi ngazi ya taifa,kutoa mafunzo kwa makocha wanaofundisha timu na zawadi kwa timu zinazofanikiwa kufanya vizuri”,alisisitiza 

Shayo alisema mbali na uzinduzi wa UMISSETA ngazi ya mkoa uliofanyika mkoani Dodoma utafanyika katika mikoa ya Kagera,Tanga,Mtwara,Singida na Zanzibar ambapo uzinduzi kwa ngazi ya taifa utafanyika mkoani Mwanza ambapo pia mashindano haya yatafanyika.

MECHI YA MBEYA CITY NA YANGA YAPIGWA TAREHE SOMA HAPA KUJUA ..


Tokeo la picha la mbeya city vs yanga
Mechi namba 199 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mbeya City na Yanga iliyopangwa kufanyika Mei 1, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya itapangiwa tarehe nyingine.

Uamuzi wa kuipangia tarehe nyingine ni kukidhi matakwa ya Kanuni inayotaka nafasi kati ya mechi moja na nyingine isiwe chini ya angalau saa 72.

Kwa mujibu wa ratiba, Yanga itakuwa na mechi dhidi ya Simba itakayofanyika Aprili 29, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

IMETOLEWA NA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

Saturday, March 17, 2018

Thursday, March 15, 2018

KAMATI YA MAADILI YAMFUNGIA MAISHA MICHAEL WAMBURA

Tokeo la picha la michael wambura
Kamati ya Maadili ilikutana tarehe 14/3/2018 kupitia shauri linalomhusu Ndugu Michael Richard Wambura, Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ambaye anashtakiwa na Sekretarieti ya TFF kwa makosa matatu ya kimaadili.

TUHUMA ZILIZOWASILISHWA
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha mbele ya Kamati mashtaka matatu (3) ambayo ni;
1.    Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo  hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
2.    Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
3.    Kufanya vitendo vinavyoshusha Hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)
MAELEZO YA KOSA
Ndugu Michael Richard Wambura alichukua fedha isivyo halali kwa kughushi barua ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED ya kujipa mamlaka ya kulipwa kwa kula njama na waliokuwa Viongozi Wakuu wa TFF; Rais na Katibu Mkuu waliopita. Kitendo hiki ni kuvunja maadili na kushusha hadhi ya Taasisi ya TFF.



SHAURI LILIVYOENDESHWA
Ndugu Wambura alipelekewa wito wa kufika mbele ya Kamati siku ya tarehe 14/3/2018 ili awasilishe utetezi kuhusu tuhuma zinazomkabili. Ndugu Wambura alipewa hiari ya kutoa utetezi huo kwa mdomo, kutuma kwa maandishi, kuleta mashahidi au kutuma mwakilishi kama kifungu cha 58 cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013 kinavyoelekeza. Ndugu Wambura alimtuma mwakilishi wake, Wakili Emanuel Muga, aliyefika na kuthibitisha kuwa ametumwa na mteja wake (Ndugu Michael Richard Wambura) kuwasilisha utetezi wake mbele ya Kamati.

Baada ya kuelezwa mashtaka yanayomkabili mteja wake, Wakili Muga aliiomba Kamati kuwa mteja wake anaomba kupewa muda wa kupitia shauri hilo ili aandae utetezi, vielelezo, na mashahidi. Mara baada ya kutoa ombi hilo Kamati ilimruhusu asubiri ili ipitie kabla ya kufanya uamuzi. Baada ya majadiliano wajumbe walikubaliana kuwa suala hili si geni kwa Ndugu Wambura; hivyo siyo kweli kuwa hana ufahamu nalo. Pia moja ya vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati ni utetezi wa maandishi wa Ndugu Wambura kuhusiana na suala hilo ulioandikwa 4/12/2017. Hivyo Kamati ilijiridhisha kuwa Ndugu Wambura anao ufahamu wa kutosha wa suala hilo na alikuwa na uwezo wa kufika mbele ya Kamati ili kutoa maelezo ya ziada.

Kamati ilimjulisha Wakili Muga kuhusiana na uamuzi huo na kumtaka aanze kujikita katika kujibu mashtaka yaliyowasilishwa mbele yake. Hata hivyo Wakili Muga hakutaka kufanya hivyo na badala yake aliomba apewe muda zaidi wa kuandaa utetezi, vielelezo, na mashahidi. Kamati ilimkumbusha Wakili Muga kuwa wito wake ulijieleza vizuri hivyo ilikuwa ni wajibu wake kumshauri mteja wake ipasavyo na kumsaidia katika kujibu mashtaka yaliyofikishwa mbele yake. Baada ya maelezo hayo Kamati ilimuuliza Wakili Muga kama yuko tayari kuendelea na shauri au vinginevyo na yeye akaridhia kuwa shauri liendelee.

Baada ya makubaliano hayo, Wakili Muga alipewa nafasi ya kujibu mashtaka matatu yanayomkabili mteja wake.

Shitaka la kwanza:
“Kupokea/kuchukua fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo  hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Michael Richard Wambura alipokea malipo kutoka Chama cha Miguu Tanzania (FAT) na baadaye TFF ikiwa ni marejesho ya mkopo ambao FAT ilikopeswa dola la kimarekani $30,000 kutoka katika kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2002. Mkataba wa deni hilo ulisainiwa na Ndugu Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT. Hata hivyo Kamati haikupata nyaraka wala kumbukumbu zozote zile zinazoonyesha kuwa Ndugu Wambura alipata idhini ya kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka katika Kamati Tendaji ya FAT. Vilevile Kamati haikuona uthibitisho wa kiasi hicho kupokelewa kwenye akaunti za FAT zaidi ya Mkataba ambao ulisainiwa na Ndugu Wambura peke yake bila kuwa na shahidi mwingine kutoka FAT kinyume na taratibu za kawaida za mikataba. Vile vile Kamati imeshangaa ni taratibu gani zilitumika kwa taasisi kama FAT kuchukua mkopo mkubwa kama huo kwenye kwenye kampuni hiyo badala ya taasisi za fedha kama vile benki ambazo ndizo zinazojishughulisha na masuala hayo.

Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa Ndugu Wambura, kwa nyakati tofauti, alipokea jumla ya sh.84,000,000.00 kutoka FAT na baadaye TFF kama marejesho ya mkopo kwa niaba ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED. Hata hivyo Kamati haikupata uthibitisho wa kisheria kutoka kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED unaomuidhinisha Bw. Wambura kupokea malipo ya mkopo huo kwa niaba yake zaidi ya barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo. Hata hivyo barua hiyo, licha ya kuandikwa miaka 10 baada ya Bw. Wambura kuchukua nusu ya mkopo huo, haikuwahi kupokelewa TFF na wala haikidhi matakwa ya kisheria ambayo ni kuwa na Power of Attorney iliyosajiliwa kwa Msajili wa Hati na Nyaraka.
Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na Sekretarieti malipo ya mkopo huo yalifanyika kwa awamu ambapo mara ya kwanza Ndugu Wambura alilipwa $15,000 alizopokea tarehe 29/4/2004. Hata hivyo Kamati ilibaini mapungufu katika fomu hiyo kwani maombi ya kulipwa fedha hiyo yalitolewa na Ndugu Wambura na kuidhinishwa na yeye mwenyewe, kinyume na taratibu za fedha.

Malipo hayo ya mkopo hayakufanyika kwa kipindi cha miaka 10, chini ya Uongozi wa Ndugu Leodgar C. Tenga, mpaka alipoondoka madarakani na kuingia uongozi mpya chini ya Ndugu Jamal Malinzi ndipo yalipoanza kufanyika tena. Kamati inapata mashaka juu ya uhalali wa deni na malipo hayo kwani hakukuwa na madai wala malalamiko yoyote yaliyowasilishwa kudai au kukumbushia deni hilo kwa kipindi chote hicho. Katika hali ya kawaida siyo rahisi kulipa deni hilo bila kujiridhisha uhalali wake.

Shitaka la pili
Kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Sekretarieti iliwasilisha nakala ya barua ya tarehe 21/6/2016 kutoka kwa Bibi Irene W. Maganga ambaye ni  mke wa mmiliki wa kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED, Marehemu Enock Maganga na mmoja wa wasimamizi wa mirathi ya marehemu walioteuliwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam. Barua hiyo inakanusha kuwa kampuni hiyo haikuwahi kupokea malipo yoyote ya deni hilo. Hii inaonyesha kuwa Ndugu Wambura hakuwahi kupewa mamlaka ya kupokea fedha hizo na pia hakuwahi kuziwasilisha kwa wamiliki wa kampuni hiyo fedha alizopokea kutoka FAT na TFF. Kwa msingi huo hata uhalali wa barua Kumb. Na. JKC/CONT/TFF/2014 ya tarehe 13/1/2014 kutoka kwa kampuni hiyo aliyoiwasilisha kuonyesha kuwa ameidhinishwa kupokea malipo hayo unatia shaka. Ndugu Wambura hajawahi kukanusha maelezo yaliyomo kwenye barua hiyo licha ya kupewa nafasi akiwa Makamu wa Rais wa TFF.

Shitaka la tatu:
“Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015)”

Kamati imejiridhisha bila shaka kuwa vitendo vya Ndugu Wambura vinashusha hadhi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF). Kitendo cha Ndugu Wambura kuiingiza FAT na baadaye TFF katika mkopo wa $30,000 bila kufuata taratibu zozote ni ukiukwaji mkubwa wa maadili. Vile vile kitendo hicho kimelipaka matope shirikisho hilo mbele ya umma kwani mambo aliyoyafanya hayaakisi ukubwa na umuhimu wa taasisi hiyo. Kwa nafasi yake ya Makamu wa Rais, Ndugu Wambura ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, hivyo vitendo hivyo haviendani na hadhi na majukumu ya nafasi yake hiyo.


HUKUMU
Kosa la kwanza:
Kulingana na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, Ndugu Michael Richard Wambura, amefanya kosa la kifisadi ambalo adhabu zake ni;
  1. (i) faini isiyopungua shilingi 10,000,000.
    (ii) kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5

  1. Kama suala ni zito na limekuwa likijirudia rudia, kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha.




    Kosa la pili:
    Kwa kosa la kughushi kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, kinatoa adhabu ya kifungo cha cha kutojihusisha na mpira wa miguu kwa miaka isiyopungua 5.

    Kosa la tatu:
    Kwa kosa la kushusha hadhi ya Shirikisho ni kwenda kinyume na Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015).Hili ni kosa la kimaadili ambalo adhabu zake zinaenda sambamba na adhabu nyingine zinazotolewa na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

    Baada ya kupitia shauri hili na kuridhika pasipo na shaka kuwa Ndugu Michael Richard Wambura ametenda makosa hayo yote, Kamati imemfungia Ndugu Michael Richard Wambura kifungo cha kutojihusisha na mpira wa miguu maisha. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia uzito wa kosa lake kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013.

    Kwa kuwa suala hili linahusisha masuala ya rushwa, Kamati inaielekeza Sekretarieti, kwa kupitia kifungu cha 6(3) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013, ilifikishe suala hili la Ndugu Michael Richard Wambura katika vyombo vya dola ili vifanye uchunguzi. Aidha Kamati inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Ukaguzi kuwa waliokuwa viongozi wakuu wa TFF wakati malipo hayo yanafanyika, Ndugu Jamal Malinzi (Rais) na Ndugu Celestine Mwesigwa (Katibu Mkuu) nao waunganishwe katika uchunguzi huo.

    HITIMISHO
    Kamati haikupendezwa na taarifa zilizowasilishwa na Sekretarieti kuhusu juhudi zilizofanywa na vyombo mbalimbali kuizuia isifanye kazi yake kwa mujibu wa Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015) na Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013. Kamati inaviasa vyombo hivyo kutoingilia mambo ya mpira wa miguu, hasa vyombo vya kimaamuzi, kwani athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa ustawi wa mpira wa miguu nchini.

    IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF