Tuesday, October 2, 2012

Sumaye kupasua bomu keshokutwa

Wakati wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea kutafakari kubwagwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), yeye (Sumaye), ameibuka na kueleza kuwa siku tatu zijazo ataeleza kilichojitokeza katika uchaguzi huo.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka 10 cha awamu ya tatu ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa, aliangushwa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mary Nagu, katika kinyang’anyiro cha Mjumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara.

Akizungumza na NIPASHE jana kwa simu, Sumaye alisema atakapokutana na waandishi ataeleza kwa kina kilichojitokeza kwenye uchaguzi huo siku tatu zijazo atakapowasili jijini Dar es Salaam.

“Nimepigiwa simu na waandishi wengi wakinitaka nizungumze suala la kuangushwa kwangu kwenye nafasi ya NEC, lakini nimewaeleza kuwa nitaeleza suala hilo siku tatu zijazo nitakapokuwa Dar es Salaam,” alisema Sumaye.

Dk. Nagu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanang, aliibuka kidedea kwa kupata kura 648 dhidi ya kura 481 alizopata Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

Kuangushwa kwa Sumaye katika kinyang’anyiro hicho kumezua maswali mengi nchini ambayo baadhi ya watu wanaeleza kuwa hiyo ni ishara mbaya kwa mwanasiasa huyo mkongwe ambaye amekuwa akihusishwa na mipango ya kugombea urais mwaka 2015 kupitia chama hicho kikongwe.

No comments: