SAKATA LA SHULE HII YA MSINGI JIJINI DAR ES SALAAM WANAFUNZI
KULAWITIANA... INAISKITISHA
TUHUMA zinazohusisha madai ya baadhi ya wanafunzi wa kiume wa shule ya msingi Mbuyuni ya jijini Dar es Salaam kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja miongoni mwao yamechukua sura mpya.
Kubainika kwa vitendo hivyo kulikosababisha uongozi wa shule hiyo iliyoko katika manispaa ya Kinondoni kuwahamisha wanafunzi sita wa darasa la sita wanaotajwa kujihusisha na makosa hayo ya kimaadili kumesababisha kuibuka kwa mtafaruku na mtanzuko mkubwa.
Kuibuka kwa mtafaruku huo kumewaweka njia panda mwalimu mkuu wa shule hiyo, Doroth Malecela, walimu, wanafunzi, baadhi ya wazazi na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni.
Katika hatua moja, kundi la walimu 14 wa shule hiyo ya Msingi ya Mbuyuni, wakiongozwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Elizabeth Mwandiko jana walifika katika ofisi za gazeti hili eneo la Sinza na kueleza kusikitishwa na taarifa zilizokuwa zikiipaka matope shule yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda kuhusu kadhia hiyo, walimu hao walikiri kuhusu kuhamishwa kwa watoto sita katika shule hiyo kutokana na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.
Mwandiko ambaye aliwaongoza walimu hao kukanusha taarifa zilizokuwa zikimhusisha mwalimu wao mkuu na vitendo vya kuwahamisha wanafunzi hao sita kwa sababu za kiuonevu, alisema kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo ulifanyika uchunguzi wa kina kuhusu mienendo isiyofaa ya wanafunzi hao.
“Ni kweli wanafunzi sita wamehamishwa shule kutokana na makosa hayo ya kimaadili. Wakati uamuzi huo ukifikiwa Mwalimu Mkuu hakuwapo shuleni.,” alisema Mwandiko.
Mwalimu Mwandiko ambaye awali alikuwa akizungumza kwa kupokezana na mwalimu mwenzake, Paschal Mwenda alisema uchunguzi walioufanya kwa kuwahusisha wanafunzi wenyewe, uliwawezesha kubaini kuwa vitendo hivyo vilikuwa vikifanyika chooni.
“Kuvuja kwa taarifa hizi kulianza baada ya mwalimu mmoja kushitushwa na tabia ya wanafunzi fulani kuomba ruhusa kwenda kujisaidia ambayo ilikuwa ikiwahusisha zaidi ya mwanafunzi mmoja na kisha wanafunzi hao wakakaa chooni kwa muda wa zaidi ya dakika 15,” alisema Mwandiko akielezea kuhusu vitendo hivyo.
Baada ya maelezo ya walimu hao wawili, uongozi wa gazeti hili ulikutana na walimu wengine 12 waliokuwa katika msafara huo wa kumtetea mwalimu wao mkuu sambamba na wao wenyewe kupinga taarifa zozote ambazo zilikuwa zikiwahusisha wao na kuvuja kwa habari hizo katika vyombo vya habari.
Wakati walimu hao wakizungumza na gazeti hili, jana hiyo hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Fortunatus Fwema alikuwa akikutana na mmoja wa wazazi ambao watoto wao walihamishwa wakihusishwa na vitendo hivyo.
Mzazi huyo ambaye amekuwa akipinga uamuzi huo wa mwanaye kuhamishwa, mbali ya kumrushia lawama mwalimu Malecela, alikwenda kuonana na DED baada ya sakata hilo kushindwa kutatuliwa na ofisi ya Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa Wilaya ya Kinondoni (DEO).
Akizungumza mbele ya DED, mzazi huyo Neema Daud aliyekuwa ameandamana na mwanaye, Lucas Charles alimwelezea kiongozi huyo namna alivyokuwa akisumbuliwa na uongozi wa shule hiyo.
Baada ya kusikiliza hoja za mzazi huyo, DED huyo aliamuru mwanafunzi Lucas arejeshwe shuleni Mbuyuni wakati uchunguzi zaidi kuhusu sakata hilo ukiendelea.
“Nilikuwa likizo na nimeingia leo Jumatatu (jana) ofisini, lakini suala la Shule ya Msingi Mbuyuni nimelipata mezani kwangu na kwa haraka haraka naliona kama lina mlolongo mrefu sana. Kwa upande wa Mbuyuni naomba huyu mwanafunzi arudi shuleni kwao aendelee na masomo yake wakati muafaka ukitafutwa. Kitendo cha wanafunzi kutangatanga barabarani si jambo la uungwana,” alisema DED.
No comments:
Post a Comment