Monday, April 29, 2013

MAAJABU FAILI LA LUDOVIKI RWAZAURA JOSEPH LAPOTEA KUSIKOJULIKANA


 


 















Lwakatare na Ludovic


SASA kuna kila dalili zinazoonyesha kuwa faili la mtuhumiwa namba mbili katika kesi ya ugaidi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ludovick Joseph, limeyeyuka baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, kudai kuwa hajaliona.





Dalili hizo zilianza tangu wiki iliyopita, wakati MTANZANIA Jumapili lilipoanza kufuatilia taarifa za kuwepo kwa utata wa tukio zima la kutekwa kwa Ludovick pamoja na utata wa taarifa alizodai kuzitoa katika Kituo kidogo cha Polisi Kigogo.





MTANZANIA Jumapili lilianza uchunguzi wa taarifa hizo na wiki iliyopita likiripoti kwa kina utata huo kwa kuweka wazi mkakati wa kumshitaki Ludovick kuwa ni mpango mahususi unaodaiwa kuratibiwa na Serikali kufichua njama za kigaidi, ambazo zinadaiwa kutekelezwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.








Hata hivyo, Polisi wamekuwa wakishindwa kuthibitisha taarifa hizo za kutekwa kwa Ludovick, ikiwa ni pamoja na kushindwa kutoa RB namba ambayo Ludovick alidai kuifungua katika kituo cha polisi cha Kigogo.





Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, ambaye alitupiwa mpira huo kutoka kwa maofisa wa chini yake kuwa ndiye anayeweza kutoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo la Ludovick, ikiwemo pia namba ya RB, mara kadhaa ameshindwa kufanya hivyo.





Gazeti hili lilifika ofisini kwake, lakini hakuweza kupatikana na kuambiwa kuwa yuko katika harakati za sherehe za miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini alipotafutwa kwa namba yake ya simu alisema kuwa bado hajafanikiwa kupata RB hiyo.





Kamanda Kenyela alipoulizwa kuwa imekuwa ni muda mrefu tangu aseme kuwa anafuatilia taarifa hizo na hakuna majibu ya kuridhisha, bado aliomba apewe muda.





“Naomba muda bado sijaipata, ni siku nyingi ...lakini ndiyo shughuli yenyewe maandalizi ya Muungano … hivi sasa niko kwenye sherehe Ikulu,” alisema.





Danadana hizo za polisi zilianza wiki iliyopita, wakati MTANZANIA Jumapili lilipopata taarifa kuwa tukio la kutekwa kwa Ludovick aliloliripoti katika kituo cha Kigogo ni feki.





Gazeti hili lilikumbana na vikwazo vya kutoelezwa ukweli kuhusu tukio hilo la Ludovick wakati likifuatilia taarifa hizo tangu Kituo Kidogo cha Polisi Kigogo.





Mwandishi wa gazeti hili alipofika kituo cha Kigogo alielezwa na askari aliyemkuta hapo kuwa taarifa za matukio mbalimbali hufunguliwa hapo, lakini huhamishiwa Kituo cha Polisi cha Magomeni kutokana na udogo wa kituo hicho.





Hivyo kumtaka mwandishi kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni. Gazeti hili lilipofika Kituo cha Polisi Magomeni, kwa askari mpelelezi liliyeelekezwa kuwa anahusika na kesi ya Ludovick aliyetajwa kwa jina moja la Afande Chuki, hakupatikana kituoni hapo, bali lilipewa namba yake ya simu, alipotafutwa alikana kuhusika na suala hilo kwa kuelekeza atafutwe Askari Polisi aliyetajwa kwa jina la Lukwamba Sanga.





Afande Sanga alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu sakata hilo, kwanza alikiri kuwa yeye ndiye mpelelezi wa kesi hiyo na kuwa ni kweli Ludovick alifungua RB katika kituo cha Polisi cha Kigogo, lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote juu ya tukio hilo.





Alieleza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa namba hiyo ni Mkuu wa Upelelezi wa Kituo ambaye hata hivyo hakupatikana.





Ofisa mwingine kituoni hapo alisema namba hiyo inaweza kutolewa kwa idhini ya Kamanda wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela, ambaye hata hivyo alipotafutwa kwa namba yake ya simu alisema anahitaji muda kuipata namba hiyo kwa sababu ana majukumu mengi hivyo atafutwe baadaye.





Hata alipotafutwa tena simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani na ilipokuwa hewani iliita pasipo majibu.





Baada ya wiki moja kupita, gazeti hili lilipomtafuta tena Kenyella, alisema bado hajaliona faili la Ludovick kutokana na kutingwa na mambo mengi ya kikazi.





Kurushiana mpira kwa askari hao pamoja na Kamanda Kenyela kushindwa kutoa taarifa sahihi za RB hiyo ndiko kunakozidisha maswali kuhusu utata wa tukio la kutekwa kwa Ludovick.





Wapasha habari wetu walilidokeza gazeti hili wiki iliyopita kwamba taarifa za kutekwa kwa Ludovick na kunyang’anywa vitu vyake vyote alivyokuwa navyo, zikiwemo nguo alizokuwa amevaa siyo za kweli, bali zimetengezwa ili kufanikisha mkakati wa kuwatia nguvuni watuhumiwa halisi wa sakata la ugaidi.





Ludovick alidai kutekwa usiku wa Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, akiwa eneo la Sinza, ambako alisema alitoa taarifa zake katika Kituo cha Polisi cha Kigogo na kufunguliwa RB yenye namba KIG/RB/318/2013.





Source:JF




 

No comments: