Thursday, May 9, 2013

WANAJESHI WENGINE WAAGWA KWENDA KUUNGANA NA WENZAO HUKO CONGO



Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi bendera kiongozi wa batalioni ya wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania ( JWTZ), wanaokwenda kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
 ------------

Wanajeshi wa Tanzania wanaokwenda kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wametakiwa kudumisha utamaduni  wa askari wa kulinda amani wa Tanzania katika maeneo mbali mbali duniani kwa kuifanya kazi hiyo kwa heshima, nidhamu na utii ili kulinda heshima yao wenyewe na ile ya Tanzania.

Askari hao wamekumbushwa utamaduni huo wa askari wa kulinda amani wa Tanzania katika maeneo mbali mbali duniani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais na Amiri Jeshi Mkuu alikuwa akiwaaga wanajeshi wa Tanzania wanaokwenda kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa katika DRC katika hafla iliyofanyika leo, Jumatano, Mei 8, 2012, kwenye Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu la Tanzania yaliyoko Msangani, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na askari hao, Rais Kikwete amewaambia kuwa hana wasiwasi kuhusu uwezo wao wa kutelekeza majukumu yao yanayowapeleka DRC isipokuwa tu kwamba waifanye kazi hiyo vizuri na kulingana na utamaduni wa majeshi ya kulinda amani ya Tanzania katika sehemu mbali mbali duniani.


“Tunakwenda kutelekeza majukumu ya Umoja wa Mataifa, sina shaka kuwa majukumu yenu mnayaelewa vizuri. Kazi yetu ni kulinda amani na wala hatuendi kupigana na yoyote. Kazi ya kijeshi mnaijua vizuri vile vile na kwa hili pia sina wasiwasi hata kidogo,” amesema Amiri Jeshi Mkuu na kuongeza:

“Kubwa ambalo lazima tulikumbuke ni kwamba nchi yetu kila ilikopeleka majeshi ya kulinda amani imejenga utamaduni wa pekee. Imejenga utamaduni wa askari wetu kuifanya kazi ya kulinda amani kwa heshima, kwa nidhamu na kwa utii wa kiwango cha juu. Hii ni heshima kwetu binafsi na heshima kwa taifa letu. Nawashukuruni na nawatakie kila la heri”

Kama ishara ya kuagana na askari hao, Rais na Amiri Jeshi Mkuu amemkabidhi Bendera ya Taifa Luteni Kanali Orestess Cassian Komba, Kamanda wa Kikosi cha Tanzania katika DRC ambacho kitajulikana kwa jina la TANZBATT 1-DRC, akimwambia “Bendera na Ikapepee”.

Katika jukumu la kulinda amani Mashariki mwa DRC, Kikosi cha Tanzania chenye askari 1281, kitajiunga na vikosi vya Malawi na Afrika Kusini ambavyo vyote vitakuwa chini ya Kamanda wa Brigedi hiyo, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa wa Tanzania pia. Kundi la kwanza la askari hao Tanzania linaondoka nchini kesho.

Majeshi hayo ya Tanzania yatalinda amani katika DRC chini ya Azimio Nambari 2098 (2013) la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
8 Mei, 2013

No comments: