UFAFANUZI WA MASWALI MBALIMBALI YA WADAU WA ELIMU KUHUSU MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2013
Baraza la Mitihani la Tanzania lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2013 tarehe 21/02/2014. Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Baraza limekuwa likipokea maswali mbalimbali yanayoashiria kuwa baadhi ya wadau wa elimu hawakuelewa vizuri kuhusu Viwango vya Ufaulu (grade ranges), alama ya chini ya ufaulu (pass mark) na Ufaulu wa jumla wa mtahiniwa (overall performance).
Baraza la Mitihani linapenda kutoa ufafanuzi katika mambo hayo kama ifuatavyo:
Viwango vya ufaulu (grade ranges) ni makundi ya alama yanayopangwa ili kuwaweka pamoja watahiniwa wenye uwezo unaofanana katika somo husika na kuwatofautisha na watahiniwa waliopo katika kundi jingine.
Makundi haya hupangwa ili kuwawezesha wadau kutambua namna watahiniwa walivyotawanyika katika viwango mbalimbali vya umahiri wa somo husika. Baraza la Mitihani la Tanzania, limekuwa likitumia makundi Matano (5) kwa kipindi kirefu hadi mwaka 2012. Aidha, Kuanzia Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2013, Baraza limeanza kutumia utaratibu wa Makundi Saba (7) ambayo ni A, B+, B, C, D, E na F. Utaratibu huu umelenga kupunguza mlundikano mkubwa wa alama katika kundi moja. Mgawanyo wa makundi hayo ni kama inavyoonekana kwenye Jedwali la 1.
Jedwali Na 1: Viwango vya ufaulu vilivyotumika katika Matokeo ya CSEE 2013.
Kundi Gredi Alama Idadi ya Pointi
1 A 75 - 100 1
2 B+ 60 - 74 2
3 B 50 - 59 3
4 C 40 - 49 4
5 D 30 - 39 5
6 E 20 - 29 6
7 F 0 - 19 7
Aidha, Idadi ya makundi ya ufaulu hutofautiana kati ya nchi na nchi kulingana na mahitaji ya nchi husika. Kwa mfano; Kenya wana makundi Kumi na mbili (12), Malawi Tisa (9), Uganda Tisa (9), Nchi za Afrika magharibi (Nigeria, Ghana, Siera Leone na Liberia) makundi Tisa.
Kwa kuzingatia viwango vya ufaulu vilivyoainishwa katika makundi saba yaliyopo kwenye Jedwali na 1, kiwango cha chini cha ufaulu ni gredi D na kiwango cha juu cha ufaulu ni Gredi A. Mtahiniwa atakuwa amefaulu somo husika iwapo atapata gredi D na kuendelea. Aidha, mtahiniwa aliyepata gredi E na F atakuwa hajafaulu somo husika.
Madaraja ya ufaulu yamepangwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1)-(6) cha Kanuni za Mitihani kinachoelekeza kuwa Ufaulu katika daraja la Kwanza hadi la Tatu upangwe kwa kuzingatia jumla ya alama (Points) na Ufaulu katika Daraja la Nne unapangwa kwa kuzingatia ufaulu wa chini aliopata mtahiniwa ambao ni gredi D katika masomo yasiyopungua mawili au ufaulu kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C katika somo moja. Hivyo, madaraja yaliyotumika ni kama yanavyoonekana kwenye Jedwali la 2.
Jedwali 2: Madaraja yaliyotumika katika CSEE 2013
Daraja Pointi
I 7 – 17
II 18 – 24
III 25 – 31
IV 1. Ufaulu katika somo moja kwa kiwango kisichokuwa chini ya Gredi C au
2. Ufaulu katika masomo yasiyopungua mawili katika Gredi D
0 Alama chini ya D mbili
Kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani, ufaulu wa somo katika Gredi A hadi C utakuwa ni ufaulu wa “Credit” na Gredi D itahesabika kuwa ni “pass”. Aidha Gredi E na F zitakuwa alama za kufeli.
Baraza la mitihani la Tanzania linapenda kutoa taarifa kwamba ufafanuzi wa sifa za kujiunga na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa kutumia mfumo huu mpya wa madaraja utatolewa na mamlaka husika ambapo Kamishna wa Elimu atalitolea ufafanuzi zaidi.
Imetolewa Na:
KAIMU KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment