Saturday, April 12, 2014

TAARIFA FUPI YA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA MKOA WA DAR ES SALAAM KUHUSU MADHARA YALIYOTOKANA NA MVUA KUBWA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.



          Katika siku chache zilizopita pamekuwa na mvua kubwa zinaendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kuanzia usiku tarehe 11/04/2014 hadi hivi leo ambazo zimesababisha athari/madhara kwa maisha ya watu na mali zao. Mvua hizi zilitarajiwa kunyesha na zitaendelea kunyesha kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa hapa nchini.

    Kufuatia mvua hizi tayari zimesharipotiwa athari kadhaa zinazogusa maisha ya watu na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi. Madhara hayo ni pamoja na vifo kadhaa, nyumba kubomoka huku nyumba nyingine zikiwa zimezingirwa ma maji jambo ambalo ni hatari endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kwa wakati.
Baadhi ya madhara yaliyoripitiwa hadi hivi sasa ni kama ifuatavyo:
1.     
   Watu wapatao kumi (10) wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mvua hizi. Kati ya watu hao, watu wazima ni watano na watoto ni watano. Pia miongoni mwa watu hao kumi mtoto mmoja mdogo haijafahamika ni wa jinsia gani.


2.    Nyumba nyingi katika meneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam zimezingirwa na maji kwa kiasi kikubwa jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya binadamu na mali zao.

3.    Madaraja takribani kumi na moja (11) yameathirika kutokana na mvua hizi. Baadhi yamefunikwa na maji na mengine yamesombwa na maji kabisa likiwemo daraja la mto MPIJI mpakani wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani katika barabara iendayo Bagamoyo ambalo kingo zake upande wa Dar es Salaam zimesombwa na maji na kusababisha mawasiliano kati ya Bagamoyo na Dar es Salaam kukatika. Kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano baina ya mikoa hii miwili tayari Waziri wa Ujenzi Mh. John Magufuri akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Dar es Salaam ameshatoa maelekezo kwamba matengenezo yaanze mara moja na kazi hiyo ifanyike usiku na mchana. 
\
                               HATUA ZILIZOCHUKULIWA.
Kutoa misaada ya uokoaji kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo hawa wafuatao:
1. 
                           Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa kutumia Kikosi cha wanamaji ambao tayari wameanza kazi hiyo.
2.    Kikosi cha Zimamoto na uokoaji.
3.    Kikosi cha Msalaba Mwekundu.
4.    Wadau mbalimbali wa kujitolea kwa mfano KSIJ, na KIMENEGRO (Polisi Shirikishi wa Soko la Samaki FERRY)

                              WITO/TAHADHARI. 

·       Wito unatolewa kwa watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vya moto kama magari, pikipiki n.k wawe waangalifu pindi wanapotaka kuvuka maeneo yenye mikondo ya maji ili kuepusha madhara yoyote yanyoweza kujitokea ikiwa ni pamoja na vifo.

·       Watu wote wanaoishi maeneo ya mabondeni au waliojenga katika mikondo ya maji wachukue tahadhari za haraka ikiwemo kuondoka maeneo hayo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kufuatia mvua hizi zinazoendelea kunyesha.

·       Kwa watumiaji wa barabara/wanaosafiri ama kwenda au kutoka Bagamoyo wanashauriwa kutumia barabara ya Morogoro kupitia KIBAHA TAMCO hadi shule ya Sekondari BAOBAO iliyopo wilayani Bagamoyo. Hii ni kwa sababu barabara ya Dar es Salaam/Bagamoyo ambayo imezoeleka kwa sasa imefungwa hadi hapo matengenezo yatakapokamilika.

Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuyatembelea maeneo yanayoonekana kuwa hatarishi, kutoa elimu kwa wananchi ili kuepusha madhara zaidi yasiweze kutokea. Wananchi wanashauriwa kuonyesha ushirikiano kwa kuchukua tahadhari mapema na kutoa taarifa haraka mara yanapotokea madhara yaliyosababishwa na mvua hizi.

No comments: