Saturday, June 14, 2014

BOSI ALIYEMCHOMA HAUSIGELI WAKE NA PASI PAMOJA NA KUMNG'ATA APANDISHWA KIZIMBANI KATIKA MAHAKAMA YA KINONDONI

Mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es salaam imesitisha kwa muda shughuli zake baada ya zomeazomea iliyosababishwa na umati mkubwa wa watu waliofika mahakamani hapo kushuhudia kesi inayomkabili Amina Maige aliyeshitakiwa kwa kosa la kumjeruhi binti kwa kumng'ata na kumuunguza kwa pasi.Ndivyo hali ilivyokuwa katika mahakama hiyo mara baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo kabla ya kuteremka kutoka ndani ya gari alifunika uso wake na mtandio hali iliyosababisha umati huo kuanza kupiga kelele wakitaka afunuliwe ili aonekane.
Hata mara baada ya kuhifadhiwa katika chumba cha maabusu ya mahakama hiyo wakati akisubiri kupandishwa kizimbani baadhi ya wanaharakati waliofika mahakamani hapo nao walisikika wakilaani kitendo cha polisi kumsaidia kufunika uso.

Zoezi la kuwatuliza wananchi hao lilionekana kuwashinda askari wa jeshi la polisi hali iliyowalazimu askari magereza kuingilia kati na kusaidiana nao ili shughuli za mahakama ziweze kuendelea kama askari Mmoja alivyosikika akiwaomba waondoke katika eneo hilo.

Akisoma shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo wakili wa serikali Mohamed Salum mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Kinondoni Yohana Yongolo amesema mtuhumiwa Amina Maige anakabiliwa na kosa la kumjeruhi vibaya Binti Eusta Hashim kinyume na kifungu kidogo cha sheria 225, kosa alililolitenda huko eneo la Mwananyamala Manjunju.

Wakili Mohamed amesema upelelezi umekamilika ambapo mshitakiwa amekana shitaka hilo na kurudishwa rumande baada ya mwendesha mashitaka huyo kumuomba hakimu asimpatie dhamana kwa ajili ya usalama wake, ombi ambalo hakimu alikubaliana nalo ambapo mtuhumiwa amerudishwa rumande hadi June 26 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya masikilizo ya awali.

No comments: