BAADA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kumshambulia Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), ukimuita mpangaji katika jimbo hilo, amewajibu akisema kuwa wanaota ndoto za mchana.
Mbilinyi maarufu kama Sugu, alisema vijana hao hawazijui siasa za jimbo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Sugu, alisema vijana hao ndio wapangaji, na kwamba wasitarajie mteremko kwani yeyote atakayesimamishwa katika jimbo hilo kupitia CHADEMA ataibuka mshindi kutokana na wananchi wa Mbeya kuendelea kuwa na imani na chama hicho.
Alisema jimbo hilo alilikuta kama nyumba kuukuu, akaamua kuinunua na baadaye akaivunja na kupandisha ghorofa, halafu aliyemuuzia anarudi na kudai nyumba ni ya kwake.
“Ndugu zangu, Jimbo la Mbeya ni sawa na Mkinga ama Mpemba aliyeenda Kariakoo, amenunua nyumba chakavu akaibomoa na kupandisha ghorofa zaidi ya tatu, halafu aliyeuza nyumba hiyo anaibuka na kusema hao watu ni wapangaji, si atakuwa anachekesha?” alihoji.
Aliongeza kuwa CCM hawana chao katika jimbo hilo kwa sababu sasa CHADEMA wanawaza kuchukua Halmashauri ya Jiji, na kwamba suala la ubunge haliwapi shida tena.
“Mikakati yetu ni kuchuka kata zote, lakini ili kuleta changamoto katika baraza ni vema tukawaachia kata kama nane ili kuleta changamoto katika Baraza la Madiwani,” alisema.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, viongozi hao wa UVCCM wanafanya mikutano hiyo bila kuwa na taarifa kamili za jimbo hilo, kwamba ndio maana wamekuwa wakikurupuka na kutoa shutuma zisizo na ukweli wala utafiti wowote.
Alisema kuwa katika Kata ya Nsalaga kulikuwa na mpango wa kujenga bwawa la samaki, lakini diwani wa kata hiyo kupitia CCM aliwashawishi viongozi wa serikali kugomea mradi huo kwa madai kuwa hitaji lao ni madawati.
Sugu alisema kuwa utafiti alioufanya alibaini mradi huo uligomewa na viongozi wa serikali za mitaa, ambao walipata shinikizo kutoka kwa diwani.
“Unajua watu wanaongea sana, ohoo aliahidi kuwa ataleta mradi wa samaki na mpaka sasa hakuna kitu, wananchi wengi hawajui, utekelezaji ulishaanza, lakini kutokana na ukiritimba wa baadhi ya wanasiasa pamoja na watumishi wa serikali wameukwamisha.
“Pale Uyole tulishachimba bwawa la samaki muda mrefu na nilishaongea na Mkurugenzi wa Jiji tukabaini kuwa maji yanayohitajika katika bili yake ni kama sh 200,000 kwa mwezi, lakini mpaka sasa hakuna kitu, wanazungusha tu bila kutoa sababu za msingi,” alisema Sugu.
Katika mikutano mingi ya CCM, wamekuwa wakijinadi kuwa jimbo hilo limepangishwa kwa muda kwa CHADEMA, hivyo uchaguzi ujao watalirejesha bila ugumu wowote.
Wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuwaapisha makamanda wa UVCCM kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe mwishoni mwa wiki, vijana hao wa CCM walisema kuwa Sugu ni mpangaji katika jimbo hilo, hivyo ajiandae kuondoka katika uchaguzi ujao
Chanzo ni Gazeti makini la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment