Sunday, September 14, 2014

HIVI NDIVYO YANGA YA JAJA ILIVYOIGARAGAZA AZAM TAIFA LEO

Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche akienda chini baada ya kudhibitiwa na mabeki wa Yanga SC
 YANGA SC imetwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.

Mshambuliaji wa Kibrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ alifunga mabao mawili katika mchezo huo, wakati Simon Msuva alifunga la tatu, yote kipindi cha pili.
Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na timu zote zilishambuliana kwa zamu.

Azam ilitawala mchezo dakika 30 za mwanzoni, lakini Yanga ilichangamka baada ya kocha Marcio Maximo kumpumzisha chipukizi Said ‘Kizota’ Juma na kumuingiza Hassan Dilunga aliyekwenda kufanya kazi nzuri.
Beki wa Yanga SC, Juma Abdul akimdhibiti mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche
 Safu ya ulinzi ya Yanga SC leo ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kufanikiwa kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Azam FC, akina Leonel Saint Preux, Didier Kavumbangu na Kipre Herman Tchetche.

Kipindi cha pili, Azam FC walikianza kwa kasi wakifanya mashambulizi mawili mfululizo- lakini safu ya ulinzi ya Yanga SC ilisimama imara kudhibiti hatari zote.
Winga Simon Msuva aliyeingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan ndiye aliyekwenda kuimaliza Azam FC.

Msuva aliseti bao moja na kufunga moja- kwanza akitia krosi ambayo ilimbabatiza beki wa Azam na kumkuta Jaja aliyefunga dakika ya 56 na baadaye akafunga mwenyewe bao la tatu.    
Jaja akiwa na medali yake ya kwanza yanga
 Lakini kabla ya Msuva kufunga la tatu, Jaja alifunga tena baada ya kupokea pasi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa na kumchambua vizuri kipa Mwadini Ali dakika ya 65.
Msuva alifunga bao la tatu baada ya kupokea pasi ndefu ya Hussein Javu na kukutana na kipa Mwadini Ali aliyetoka langoni ambaye alimlamba chenga na kwenda kuukwamisha mpira nyavuni dakika ya 87.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick alimkabidhi Nahodha wa Yanga SC Ngao baada ya mechi hiyo na baada ya hapo, wachezaji, viongozi na makocha wa timu hiyo wakaanza kushangilia.
Hii ni mara ya pili mfululizo Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya mwaka jana pia kuifunga Azam FC 1-0, bao pekee la Salum Telela. 
Maximo akimpongeza yanga
 Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Said ‘Kizota’ Juma/Hassan Dilunga dk37, Haruna Niyonzima/Hussein Javu dk79, Genilson Santana ‘Jaja’/Hamisi Kiiza dk79, Mrisho Ngassa/Omega Seme dk72 na Nizar Khlafan/Simon Msuva dk46.
Azam FC; Mwadini Ali, Erasto Nyoni/Gardiel Michael dk74, Shomary Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Kevin Friday dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Ismaila Diara dk83 na Leonel Saint-Preux/Khamis Mcha dk62.
Kikosi cha yanga wakishangilia baada ya ushindi

No comments: