Friday, October 31, 2014

MPYA KUTOKA CCM LEO

Katibu
wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari
kwenye ukumbi wa Sekretarieti,makao makuu ya Chama Ofisi Ndogo Lumumba
jijini Dar es Salaam.
HABARI KAMILI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa furaha Chama cha Frelimo kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 15, mwaka huu.


Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Frelimo, Mhe Filipe Nyusi ameibuka kidedea na sasa ndiye Rais Mteule wa Msumbiji ambaye baada ya kuapishwa atashika mikoba itaakayoachwa na Rais anayemaliza muda wake, Armando Gwebuza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, katika ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye (Pichani), amesema, CCM imepokea ushindi huo kwa furaha kubwa kutokana na undugu wa damu uliopo baina yake na Frelimo kwa mikaka mingi.

"Chama Cha Mapinduzi kilifuatilia kwa karibu kwa kuwa CCM na Chama cha Frelimo ni vyama ndugu vyenye historia moja na ya pamoja ya Ukombozi Kusini mwa Afrika. Historia hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Mteule wa nchi hiyo Ndugu Filipe Nyusi mara baada ya kuteuliwa kwake na Frelimo kugombea Urais, nchi ya kwanza kuitembelea kuwa Tanzania", alisema Nape na kuongeza;

"Ikumbukwe kwamba huyu si mgeni hapa Tanzania. Kama wanaharakati wengine wa ukombozi, Ndugu Nyusi aliishi Tanzania, anaongea vizuri Kiswahili na anaichukulia Tanzania ni nyumbani".

Alisema kwa mnasaba huo, Chama Cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kushangilia ushindi walioupata ndugu zao wa Frelimo, kwa kuwa ushindi huo ni wa wote.

"Tunampongeza sana Rais Mteule Filipe Nyusi kwa kupeperusha vema bendera ya Frelimo. Matokeo ya Uchaguzi yamedhihirisha imani kubwa waliyonayo wana-Msumbiji kwa Frelimo na kwa Rais Mteule Filipe Nyusi", alisema Nape. 


Nape amesema CCM ina imani kwamba chini ya uongozi imara wa Mwenyekiti wake Dk. Jakaya Kikwete, na Rais Mteule Filipe Nyusi, uhusiano kati ya vyama vya CCM na Frelimo utaimarika na kustawi.

Kadhalika Chama Cha Mapinduzi kimempongeza  Armando Guebuza kwa kuiongoza Frelimo na Taifa lake vema na kukamilisha uongozi wake kwa mafanikio makubwa.

Anapoanza kipindi hiki cha uongozi wa Taifa lake, sisi wana-CCM tunamtakia Ndugu Nyusi afya njema, busara, maarifa na uongozi uliotukuka", alisema Nape. 

Alisema, CCM itasimama pamoja na Frelimo katika kuendeleza urithi ulioachwa na waasisi wa vyama vyao, Mwalimu Julius Nyerere na  Samora Machel. 

No comments: