VIJANA WAHALIFU MAARUFU KWA JINA LA PANYA ROAD
SASA WAFIKIA 1508. WAMEANZA KUFIKISHWA MAHAKAMA MBALIMBALI JIJINI DAR ES
SALAAM.
Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na msako mkali wa
kuwakamata na kuwadhibiti vijana wanaofanya uhalifu wa makundi maarufu kwa jina
la Panya Road.
Msako huo mkali ni endelevu kama ilivyokwishaelezwa tangu awali
mpaka tutakapohakikisha uhalifu wa makundi au jina la panya road litakapofutika
kabisa. Misako hii inafanyika katika mikoa yote ya kipolisi yaani Ilala, Temeke
na Kinondoni na makamanda wa mikoa hiyo wanaendelea kuwa wasimamizi wakuu wa
misako hii.
Misako hii iliyoanza
tarehe 03/01/2015 hadi sasa imefanikisha kuwakamata vijana wapatao 1508 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali
yakiwemo ya kujeruhi,wizi, dawa za kulevya, kupatikana na bhangi, wapiga debe
na kubugudhi abiria, kucheza kamari, biashara ya ukahaba, mirungi, mikusanyiko
isiyo halali katika vijiwe n.k. Uzoefu unaonyesha kwamba maeneo na vitendo
tajwa hapo juu huchochea vijana kufanya uhalifu wa aina mbalimbali ambao pia ni
kero kwa wananchi.
Pamoja na watuhumiwa
hawa wote kukamatwa, hadi sasa
watuhumiwa wapatao 959 tayari
wamefikishwa katika mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa tuhuma
zilizotajwa hapo juu. Mashauri yao yanaendelea katika mahakama hizo kwa hatua
mbalimbali za kutajwa, kusikilizwa, n.k.
Aidha, watuhumiwa
wapatao 430 wameachiwa kwa dhamana kusubiri
kukamilisha upelelezi huku nyendo zao zikifuatiliwa kwa kushirikiana na wazazi
wao na viongozi katika maeneo yao. Watuhumiwa 119 wameachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha
lakini pia nyendo zao zinafuatiliwa na endapo watabainika wanajihusisha na
uhalifu basi watakumbwa na msako unaoendelea.
Natoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa
kutoa taarifa za uhakika kama wanavyofanya hivi sasa ili makundi yanayofanya
uhalifu wa aina ya panya road yatokomezwe kabisa ikiwa ni pamoja na uhalifu
mwingine wa aina yoyote. Nataka wananchi wa jiji la Dar es Salaam na watanzania
kwa ujumla waishi na kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa amani na
utulivu uliozoeleka.
S.H. KOVA,
KAMISHNA WA
POLISI KANDA MAALUM,
DAR ES
SALAAM.
No comments:
Post a Comment